BREAKING NEWS

Wednesday, August 29, 2012

WATANO WAKAMATWA MANYARA KWA KUGOMEA SENSA

WAKATI zoezi la sensa ya watu na makazi likiendelea jeshi la polisi Mkoani Manyara limewakamata watu watano wakazi wa kata ya Dosidosi Wilaya ya Kiteto kwa kosa la kugoma na kushawishi watu wasijitokeze kushiriki zoezi hilo.

Inadaiwa kuwa watu hao waligoma kushiriki zoezi la hilo la sensa ya watu na makazi na pia walikuwa wanashinikiza wenye imani ya waislamu kutohesabiwa kutokana na kipengele cha dini kutoingizwa kwenye dodoso refu na fupi.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo,Kamanda wa polisi mkoani Manyara Akili Mpwapwa alisema watu hao walikamatwa juzi kwenye kijiji cha Dosidosi kilichopo mpakani mwa wilaya ya Kiteto na Kongwa mkoani Dodoma.

Kamanda Mpwapwa aliwataja watu hao waliokamatwa kuwa ni Juma Mussa,Abubakary Lendawi,Mbaruku Yusuph na Badinage Hassan wote wakazi wa kijiji hicho cha Dosidosi.

Alisema watu hao waligoma kushiriki zoezi hilo na  wakawa wanashawishi watu wengine wasishiriki zoezi hilo hivyo waliwakamata na kuwashikilia kwenye kituo cha polisi kilichopo eneo hilo.

“Hata hivyo baada ya kuwakamata na kuwahoji walikiri kuwa wataenda kuhesabiwa ndipo tukawaachia wakahesabiwa na wakawaeleza wengine waliogoma nao wasijiandikishe na kuhesabiwa,” alisema Kamanda Mpwapwa.

Kwa upande wake,mkuu wa mkoa wa Manyara,Elaston Mbwilo alisema baadhi ya wakazi wa mji mdogo wa Mirerani nao waligoma kuhesabiwa lakini askari polisi wakishirikiana na maofisa wa Serikali waliwapa elimu ya faida ya sensa.

“Kuna baadhi ya watu walishinikizwa na kushawishiwa wasishiriki zoezi la sensa ya watu na makazi katika eneo la Mirerani lakini tumefanikiwa kutatua tatizo hilo na zoezi limekwenda vyema,”
alisema Mbwilo.

Alisema baadhi ya maeneo ya wilaya ya Simanjiro na Kiteto kulikuwa na mapungufu ya vifaa vya kuandikisha sensa ikiwemo daftari za dodoso refu na fupi ila hivi sasa vimepelekwa na wiki nzima zoezi hilo litafanyika kwa ufasaha.

Alisema jamii ya wahdabe ambao wanaishi porini kata ya Yaeda Chini wilayani Mbulu walishiriki zoezi hilo kwa ukamilifu na Serikali iliwachinjia wanyama pori kwa ajili ya chakula ili kufanikisha zoezi hilo katika eneo lao.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates