MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara wameipongeza Kampuni ya Orkonorei Maasai Social Initiative (OMASI) iliyopo wilayani humo kwa kuwekeza miradi mikubwa ya maendeleo.
Madiwani hao juzi walifanya ziara ya kujifunza na kujionea uwekezaji na shughuli zinazofanywa na kampuni ya hiyo ya Omasi kwenye kijiji cha Kidamunge kata ya Naberera wilayani humo.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo,Peter Tendee akizungumza kwa niaba ya madiwani hao alisema kupitia kampuni ya Omasi wilaya hiyo imejulikana kupitia bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na Omasi.
Tendee alisema kupitia miradi mikubwa iliyopo eneo hilo ya kiwanda cha maziwa na nyama Orpul,mkaa Nguk,ufugaji,kilimo, utunzaji wa mazingira wa uoteshaji miti umefanya eneo hilo kuwa na thamani kubwa.
Naye,Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Omasi Pol De Greve alisema Omasi siyo asasi isiyo ya kiserikali ila ni kampuni ya biashara jamii yenye wajibu wa kuboresha maisha na kipato cha wenyeji.
De Greve alisema Omasi ilianzishwa mwaka 2006 na dhamira yao ni kuchangia uchumi endelevu na ujasiriamali na kuboresha maisha ya watu vijijini ili wasiamie mijini na kupunguza umaskini.
Alisema kuwa kupitia Omasi wanakuza uchumi na kuleta mabadiliko ya kijamii kwa kuangalia rasilimali zilizopo kwa manufaa ya jamii na ushirikiano wa watu wa wilaya ya Simanjiro.
Kwa upande wake,Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Alhaji Muhammad Nkya alisema wataendelea kushirikiana na kampuni ya Omasi ili kuhakikisha kuwa jamii inafaidika kupitia miradi iliyopo eneo hilo.
“Wote sisi lengo letu ni kuhakikisha jamii iliyopo wilayani Simanjiro inanufaika kwa namna moja au nyingine kupitia rasilimali zilizopo kwenye eneo lao hivyo tuendelee kushirikiana katika kutumikia jamii hiyo,” alisema Alhaji Nkya.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia