ILI kuhakikisha kuwa tatizo la upungufu wa madawati unamalizika kwenye shule mbalimbali za msingi nchini Kampuni ya Tanzanite Foundation ambayo ni kampuni tanzu ya TanzaniteOne imetoa msaada wa madawati 20 Katika shule ya msingi Oloshonyokie iliyopo kata ya Naisinyai Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.
Akikabidhi msaada huo ,Mkurugenzi wa Tanzanite Foundation Hayley Henning alisema kuwa hiyo ni sehemu ya mpango mkakati wa TanzaniteOne kuinua sekta ya elimu kwenye kata zote za Tarafa ya Moipo wilayani Simanjiro.
Henning alisema kampuni yao imekuwa ikitoa misaada mbalimbali kwenye shule za msingi na sekondari za wilaya hiyo hivyo wanaendeleza kutoa msaada huo kwa ajili ya kuunga mkono jamii katika kusaidia kusukuma mbele maendeleo.
Naye,Mwenyekiti wa kitongoji cha Oloshonyokie Michael Laizer,akizungumza kwa niaba ya baadhi ya wazazi na wanafunzi wa shule hiyo aliishukuru Kampuni ya TanzaniteOne na kampuni tanzu ya Tanzanite Foundation kwa kujitahidi kuhakikisha wanachangia maendeleo ya sekta ya elimu.
Laizer alisema misaada inayotolewa na kampuni ya TanzaniteOne sehemu mbalimbali kwa ajili ya wadau wa maendeleo katika kata ya Naisinyai na wilaya huo inarahisisha kuwafanya wapige hatua kubwa ya maendeleo kwenye eneo hilo.
Naye,Rais wa kampuni ya Televisheni ya Liquidation channel ya Marekani Gerald Tempton, ambaye aliambatana na Ofisa uhusiano wa kampuni ya TanzaniteOne,Halfani Hayaeshi aliahidi kusaidia shule hiyo msaada wa vifaa vya shule vyenye thamani ya dola 5,000 za kimarekani.
Tempton alisema hatua hiyo ilifuatia maelezo aliyopewa na Mwenyekiti wa kitongoji hicho Laizer kuwa tayari shule ilishawakilisha maombi ya msaada wa vifaa hivyo kwa kampuni ya Tanzanite One.
“Nimefurahishwa na juhudi za kampuni ya TanzaniteOne kuunga mkono maendeleo ya elimu ya eneo hili na sisi Liquidation channel hatutobaki nyuma naahidi kuchangia msaada wa vifaa vya shule na msaada huo atakuja nao Hayley Hemming mwezi Octoba mwaka huu atakaporudi,” alisema Tempton.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia