SHIRIKA la Hifadhi za Taifa nchini, (TANAPA) ,
imezitaka shule mbalimbali nchini kuacha kuwatoza wazazi fedha nyingi kwa ajili
ya safari za watoto wao kutembelea hifadhi zao kwani wanafunzi hao
huingia bila kulipa viingilio kwenye hifadhi hizo.
Hayo yalisemwa na meneja utalii wa shirika
hilo, Johnson Manase alipokuwa akiongea na libeneke la kaskazini kuhusiana na kuhamasisha utalii wa ndani
iliyofanyika kwenye hoteli ya Salsalnero mjini Moshi.
Alisema kuwa Tanapa imekua ikishangazwa na
kusikitishwa na hatua ya shule hizo kuwabebesha wazazi wa viwango vikubwa
gharama wakati lengo la shirika kutowatoza wanafunzi viingilio ni kuwawezesha
wengi zaidi kutembelea hifadhi hizo kwa lengo la kujifunza.
“Tanapa hatutozi wanafunzi viingilio kwenye
malango yetu lakini kuna baadhi ya shule zinawatoza wazazi mpaka shilingi
70,000 kwa ajili ya kugharamia safari za mtoto kutembelea hifadhi zetu,
haiwezekani gharama za usafiri, malazi na chakula zikawa kubwa kiasi hicho.
Tunawaomba waache kwani viwango kama hivyo vinawashinda wazazi wengine hivyo
kuwanyima fursa watoto kuja kujifunza” alisema Manase.
Aidha alikemea tabia mbaya ya “wadaka
watalii” maarufu kama “flycatcher” waliozagaa kwenye maeneo mbalimbali ya jiji
la Arusha na mkaoni Kilimanjaro ya kuwasumbua watalii pindi wanapopita kwenye
maeneo mbalimbali wakijaribu kuwashawishi kuwaunganisha na makampuni mbalimbali
ya uwakala wa utalii.
Manase aliziomba kamati za ulinzi na usalama
za mikoa hiyo kulishughulikia suala hilo ili kuwaondolea adha watalii hao ambao
kutokana na kubabaishwa na watu hao hupata hofu kubwa juu ya usalama wao jambo
alilodai kuwa halitoi picha nzuri ya Taifa .
Kwa upande wake katibu wa chama cha mawakala
wa utalii nchini, (TATO) , Cyril Akko alisema kuwa ni vema mfumo wa ufundishaji
wanafunzi mashuleni juu ya maliasili zilizopo nchini ukabadilishwa ili
kuwajenga watoto ari na nia ya kujifunza zaidi juu ya maliasili zilizopo
nchini.