BREAKING NEWS

Sunday, August 26, 2012

WAFUGAJI WAFUNGA BARABARA KWA KITENDO CHA NGOMBE WAO KUGONGWA



Mmiliki wa ng'ombe,Mzee Saikon Sanai akiangalia ngombe wake kwa masikitiko baada ya kugongwa na kufa
KUNDI la wafugaji jamii ya kimasai wenye hasira kali wakazi wa  kijiji cha Losimingori kata ya Lepunko wilaya ya Monduli mkoani Arusha,wamejikusanya na kufunga barabara ya kutoka Arusha kwenda Singida na Dodoma kufuatia basi la AM Coach kuparamia mifugo yao na kuua ng’ombe 19 papo hapo.
Kwa mujibu  Afisa mtendaji wa kijiji  hicho,Shongon Leswaki Mayon tukio hilo limetokea leo katika eneo la Nanja kijiji cha Losimingori majira ya saa2.30 asubuhi na kwamba ng’ombe waliogongwa  wametambulika kuwa ni mali ya mfugaji, Saikon Sanai (78)mkaazi wa kijiji cha Losimingori .
Mtendaji huyo alieleza kuwa basi hilo lenye namba za usajiri T 316 AZR lilikuwa likiendeshwa na dereva aliyetambulika kwa jina moja la Abdalah likitokea jijini Arusha na kuelekea mkoani  Mwanza.
Alisema kuwa dereva wa basi hilo aliparamia mifugo hiyo na kuua ng’ombe 17 wakiwemo punda wawili   bila kujali tahadhari ya alama za vibao  barabarani vinavyoonyesha kuwa  eneo hilo  mifugo inaruhusiwa  kuvuka .
Baada ya tukio hilo dereva wa basi  hilo hakusimama hadi alipojisalimisha katika kituo cha polisi makuyuni ambapo  gari hilo limezuiwa na polisi  kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Wafugaji hao wakiwa na silaha mbalimbali za jadi walijikusanya na kupanga mawe na magogo barabarani na kuzuia magari yatokayo jijini Arusha na Singida kwa muda wa zaidi ya masaa matatu hadi alipofika mkuu wa wilaya ya Monduli Jowika Kasunga na kuwasihi kutojichukulia sheria mkononi.
Kasunga aliwasihi wafugaji hao kufuata sheria ikiwemo kwenda polisi kufungua jalada la madai katika kituo kidogo cha polisi makuyuni ,ambapo wananchi hao walijiteua akiwemo mmiliki wa ng’ombe waliouawa na kwenda kituopni hapo.
Kwa mujibu wa mmiliki huyo ng’ombe hao wanathamani ya zaidi ya shilingi 45,000 na wanachodai mmiliki wa basi hilo ajitokeze awalipe mifugo yao kwani dereva wake aligonga kwa maksudi ng’ombe hao akiwa kwenye mwendo kasi.
Katika hatua nyingine wafugaji hao wameapa kuyazuia magari yote ya AM coach kutopita katika eneo hilo  hadi wapate mwafaka wa malipo ya mifugo yao.
Kamanda wa polisi mkoani Arusha ,Liberatus Sabasi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa polisi wanafanya uchunguzi juu ya tukio hilo na kuwasihi wafugahi hao kuendelea kuwa watulivu wakati jeshi la polisi likifanya uchunguzi.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates