WATAKA KAGAME,MUSEVENI NA KABILA WASHITAKIWE,KESI YA BEMBA YAENDELEA KUSIKILIZWA ICC

Baadhi ya vyama vya upinzani dhidi ya serikali ya Rwanda vilivyopo uhamishoni kwa kushirikiana na vyama vya kirai vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Ijumaa wamewasilisha maombi mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kuwashitaki marais watatu,wakiwemo wa Rwanda, Uganda na DRC kwa makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.Katika mahakama hiyo pia Jenerali mstaafu wa jeshi amepanda kizimbani kumtetea kiongozi wa zamani wa kundi la waasi la DRC, Jean Pierre Bemba.
ICC      
Wapinzani wa Rwanda,vyama vya kiraia vya DRC vyataka marais watatu washitakiwe: Baadhi ya vyama vya upinzani dhidi serikali ya Rwanda vilivyopo uhamishoni kwa kushirikiana na vyama vya kirai vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Ijumaa waliwasilisha mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) maombi ya kuwashitaki marais watatu wa Afrika , wakiwemo wa Rwanda, Uganda na DRC.Marais hao, Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda na Joseph Kabila wa DRC wanakiwa kushitakiwa mbele ya mahakama hiyo kwa makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu unaidaiwa kufanywa Mashariki mwa DRC.Maombi hayo yanafuatia taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa Juni mwaka huu ikilituhumu jeshi la Rwanda kuliunga mkono kundi la waasi la M23 kwa kuwapatia silaha, mafunzo na askari.Waliotoa maombi hayo walipokelewa na mwakilishi wa ICC mjini The Hague, Uholanzi. 
Bemba aanza kuleta mashahidi wa utetezi: Jumanne wiki hii, shahidi wa kwanza wa utetezi katika kesi inayomkabli Jean Pierre Bemba alisimama kizimbani kutoa ushahidi wake kama mtaalamu wa Kijeshi.Jenerali mstaafu wa Ufaransa, Jacques Seara aliiambia mahakama hiyo kwamba ingekuwa vigumu kuwa na watoa amri za kijeshi tofauti wakati wa mgogoro wa kivita.
Bemba,Kamanda wa zamani wa kundi la waasi la MLC, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Makamu wa Rais wa zamani wa nchi hiyo, anashitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu(mauaji na ubakaji) na uhalifu wa kivita (mauaji, ubakaji na uporaji)  unaodaiwa kufanywa mwaka 2002-2003, katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).Mawakili wa Bemba wanadai kwamba wapiganaji wa mteja wao walikuwa chini ya CAR wakati uhalifu huo ulipokuwa unatendeka. 
Mahakama ya ICC ina uwezo wa kusikiliza kesi ya Gbagbo: Alhamisi wiki hii ICC iliyatupilia mbali maombi ya utetezi katika kesi inayomkabili Rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo ya kupinga uwezo wa mahakamana hiyo ya kusikiliza kesi ya mteja wao. Katika uamuzi wao, majaji wa mahakama hiyo wameeleza bayana kwamba ICC ina mamlaka ya kusikiliza madai ya uhalifu uliofanyika tangu Novemba 28, 2010 katika nchi hiyo kwa kulingana na tamko la Ivory Coast liliotambua mamlaka ya mahakama hiyo kuanzia Septemba 19, 2002. 
WIKI IJAYO
Kesi ya Bemba kuendelea kuunguruma: Upande wa utetezi katika kesi inayomkabli Jean Pierre Bemba mbele ya ICC unatarajiwa kuendelea kuwasilisha mahakamani hapo mashahidi wake. Bemba,Kamanda wa zamani wa kundi la waasi la MLC, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anashitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita unaodaiwa kufanywa mwaka 2002-2003, katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post