BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara limemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo kuhakikisha wazazi ambao watoto wao hawakufanya mtihani wa darasa la saba mwaka jana wanachukuliwa hatua.
Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu,Afya na Maji Sumleck Ole Sendeka akisoma maazimio ya kamati hiyo alisema bila kuchukuliwa hatua tabia hiyo inaweza ikajirudia mwaka huu wakati wa kufanyika kwa mtihani huo.
Kutokana na hali hiyo Baraza hilo la madiwani limemtaka Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo,Alhaji Muhammad Nkya kuhakikisha hatua zinachukuliwa kwa wazazi wote ambao watoto wao hawakufanya mtihani.
Sumleck alisema Ofisa Elimu Msingi wa wilaya hiyo,Jackson Mbise ahakikishe kuwa wanafunzi wote wa darasa la saba wa mwaka huu wanahudhuria kufanya mtihani siku ya zoezi hilo itakapowadia.
Pia wamemtaka Ofisa huyo Mbise kuhakikisha anatafuta fedha sehemu yoyote kwa ajili ya ukarabati wa jengo la shule ya msingi Tanzanite iliyopo kitongoji cha Songambele kata ya Mirerani.
Hata hivyo,Baraza hilo limemuagiza Mbise afuatilie na kuhakikisha kuwa mwalimu mkuu wa shule ya msingi Losinyai kata ya Oljoro namba tano anarudisha fedha kiasi cha sh5 milioni kwenye akaunti ya shule hiyo.
Sumleck alisema kamati hiyo imeagiza mwalimu mkuu huyo wa shule ya Losinyai achukuliwe hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kusimamishwa kazi wakati wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha hizo ukiendelea.
Pia Baraza hilo la madiwani limemtaka Ofisa elimu huyo Mbise kuhakikisha kuwa anatafuta fedha sehemu yoyote kwa ajili ya ukarabati wa jengo la shule ya msingi Tanzanite iliyopo kitongoji cha Songambele kata ya Mirerani.
Sumleck alisema kamati yake imeazimia kuwa endapo fedha zilizopangwa kwenye bajeti kwa ajili ya kuweka umeme katika shule ya sekondari Naisinyai kiasi cha sh40 milioni hazitatosha ifanyike harambee ya kuongeza fedha hizo.