mama mzazi wa Kadogo kalanga ambaye anasadikiwa amepigwa na maaskari akiwa anaonyesha waandishi wa habari sehemu ambazo mtoto wake ameumia
manesi wa hopitali ya seliani wakiwa wanamtoa kijana huyo nje mara baada ya kijana huyo kuonekana ameumia sana na awezi kutibiwa pale
kijana kadogo kalanga akiingizwa kwenye gari
Manesi wa hospitali ya selian wakimtoa kijana huyo na kumpeleka hospitali ya Agakhan kwa ajili ya vipimo |
KASHFA nzito imelikumba jeshi la polisi mkoani Manyara baada ya askari wake watatu kutuhumiwa kumpiga kijana ,Kadogoo Kalanga(16) mkazi wa Orkesmet wilayani Simanjiro hadi kujikojolea na kisha kupoteza fahamu kitendo kilichopeleka kijana huyo kulazwa wodi ya wagonjwa mahututi(ICU) katika hospitali ya Selian iliyopo mkoani Arusha.
Tukio hilo lilijitokeza juzi majira ya saa 5;30 katika eneo la Orkesmet ambapo askari hao mmoja wao akitambulika kwa jina moja la John walimkamata mara baada ya kumtuhumu kuiba mbuzi wa jirani yake ambaye ametambuliwa kwa jina la Mama Shedi mkazi wa eneo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya chumba cha wagonjwa mahututi(ICU) ndani ya hospitali ya Selian mama mzazi wa kijana huyo,Paulina Kalanga alisema kwamba askari hao watatu walimfuata kijana wake eneo la mnadani na kumtuhumu kuiba mbuzi hao kabla ya kuanza kumshushia kipigo kikali.
Alisema kwamba mara baada ya kumkamata walianza kumpiga kwa kutumia rungu na mateke katika maeneo yake mbalimbali ya mwili kitendo kilichopelekea kuanza kutokwa na mkojo mfululizo na kisha kupoteza fahamu.
Huku akitokwa na machozi mama huyo alisema kwamba askari hao wakati wakiendelea kumpiga kijana wake walimshika katika sehemu zake za siri na kisha kuzivuta huku wakizigongagonga kwa kitako cha silaha ya moto.
“Walimkamata na kisha kuanza kumpiga kwa marungu na mateke na kama hawakuridhika wakazishika sehemu zake za siri na kuanza kuzigongagonga na kitako cha silaha ndipo akaanza kukojoa na kisha kupoteza fahamu”alisema huku akitokwa na machozi
Mama huyo alienda mbali zaidi na kusisitiza ya kwamba polisi hao baada ya kuona hali ya kijana wake imekuwa mbaya walimbeba na kisha kumkimkimbiza haraka katika kituo cha afya cha Orkesmet kwa ajili ya matibabu.
Hatahivyo,alisema kwamba alipokea taarifa kutoka kwa rafiki yake kuhusu tukio hilo na ndipo alipochukua jukumu la kukimbia kituoni hapo na kukuta hali ya kijana wake ikizidi kuwa mbaya ambapo alikuwa haongei huku akirusharusha miguu na kichwa chake.
Alisema kwamba baada ya kuona hali hiyo ndipo yeye pamoja na ndugu zake walichukua jukumu la kuomba gari la wagonjwa mahututi (ambulance) walilopewa na kisha kumkimbiza katika hospitali ya Selian iliyopo mkoani Arusha.
Hatahivyo,alisisitiza kwamba pamoja na askari hao kumtuhumu kuiba mbuzi hao lakini cha ajabu hawajamfungulia mashtaka yoyote na hata wao walipotaka kufungua mashtaka dhidi ya askari waliompiga walinyimwa .
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Manyara,Akili Mpwapwa alipohojiwa juu ya tukio hilo alikiri kupata taarifa zake huku akisema kwa kifupi kwamba tayari ameshatoa maelekezo kwa mkuu wa polisi wilayani humo kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo na kisha aletewe ripoti kamili mezani kwake.
“Nimeshatoa maelekezo kwa OCD kwamba uchunguzi wa kina ufanyike na nipewe ripoti kamili kwa kuwa jana ndiyo nilipigiwa simu na kuelezwa juu ya tukio hilo”alisema na kukata simu ghafla
Hatahivyo,aliongeza kwa kusema kwamba endapo kuna askari atabainika kuhusika na tukio hilo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia