BREAKING NEWS

Friday, August 31, 2012

VIJANA WATAKIWA KUPATIWA MAFUNZO YA TAALUMA

JAMII nchini imetakiwa kuwapatia mafunzo ya taaluma vijana wao ili
waweze kujiajiri wenyewe na kuondokana na kasumba ya kutegemea kupata
ajira Serikalini,kwenye taasisi binafsi na sehemu nyingine tofauti.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Saidia Wanajamii Tanzania (SAWATA)
yenye makao makuu yake mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro
Mohamed Issa Mghanja wakati wa uzinduzi wa Chuo cha Ufundi Stadi
Elerai kilichopo mjini Arusha.

Mghanja alisema jamii ikiwa na utamaduni wa kuwapatia mafunzo ya
taaluma vijana wao ili wajiajiri wenyewe itakuwa jambo jema kuliko
kuwekeza kwenye sherehe za harusi na nyinginezo kwani hayo ni mambo ya
muda mfupi yasiyo na tija kwa taifa.

Alipongeza hatua ya kuanzishwa chuo hicho ambacho kitawawezesha vijana
nchini kupata taaluma hivyo kupata elimu bora na makini na kuondokana
na ukosefu wa ajira,vijana kuzurura na kushiriki kutumia dawa za
kulevya.

Ameiomba Serikali imuunge mkono Mkurugenzi wa Chuo hicho Fatuma Iddy
Kibonde ili kumuwezesha vifaa vya chuo kwa ajili ya kutoa elimu bora
zaidi kwa watu watakaojiunga na chuo hicho na kupata elimu ya ufundi.

Kwa upande wake,Mkurugenzi wa chuo hicho kilichopo eneo la Elerai
mjini Arusha Fatuma Iddy Kibonde alisema chuo hicho kinakabiliwa na
changamoto kadhaa ikiwemo mwitikio mdogo wa wasichana kujiunga na chuo
hicho.

Kidonde alisema chuo hicho ambacho kipo chini ya Veta kina lengo la
kuwaanda vijana kupata ujuzi wa kudumu na kuwawezesha wajiajiri
wenyewe katika soko la ajira hasa kipindi hiki cha Sayansi na
Teknolojia.

Aliiomba Serikali kukipatia chuo hicho eneo kubwa kwa ajili ya ujenzi
wa kudumu wa chuo hicho kwani eneo ambalo linatumika na chuo hicho
hivi sasa limekodishwa hivyo kuwa na sehemu ndogo ya kufundishia
wanafunzi wao.

Naye,Mkuu wa chuo hicho Amani Kapinga alisema mafunzo yanayotolewa na
chuo hicho ni ufundi wa umeme wa majumbani,magari,viwandani na umeme
wa mionzi,ufundi magari,ushonaji,elimu ya maisha na biashara.

Mkuu wa chuo hicho alisema kati ya wanafunzi 63 wa chuo hicho
wanafunzi 28 ni yatima wenye kuishi mazingira hatarishi na wanasoma
kwa gharama za Mkurugenzi wa Chuo hicho Fatuma Iddy Kibonde.

Alisema wamefikia mafanikio makubwa baada ya wanafunzi wa chuo hicho
kufaulu vizuri mitihani iliyotolewa na Veta hivyo anaomba jamii
iitikie wito wa kupeleka vijana kwenye chuo hicho kwani elimu ni
hazina ya kudumu.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates