Mshitakiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda, Jean Uwinkindi, amekataa
kwa mara ya nne mfululizo kujibu maswali ya mwendesha mashitaka wa
Mahakama Kuu ya Kigali, nchini Rwanda alikopelekwa kusikilizwa maelezo
ya awali ya kesi inayomkabili.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Mwendesha Mashitaka, Alain Mukurarinda, Uwinkindi anadai kwamba ‘’ana haki ya kukaa kimya.’’
Mchungaji Uwinkindi alitiwa mbaroni Juni 30, 2010 nchini Uganda na
kuhamishiwa makao makuu ya ICTR, mjini Arusha, Tanzania, siku mbili
baadaye.Aprili 19, 2012 akawa mshitakiwa wa kwanza wa ICTR, kesi yake
kuhamishiwa nchini Rwanda kwenda kusikilizwa katika Mahakama Kuu ya nchi
hiyo. Alikana tuhuma zote dhidi yake.
Kukataa kwake kuzungumza hakuzuii kesi kuendelea kusikilizwa,
Mukurarinda aliliambia Shirika la Habari la Hirondelle. ‘’Usikilizaji wa
awali wa kesi hiyo unatarajiwa kuanza kama ilivyopangwa Agosti 27,
2012.’’
Gatete Gashabana, Wakili wa utetezi wa Uwinkindi hakutaka kusema
lolote kuhusiana na kukataa kwa mteja wake kujibu maswali ya mwendesha
mashitaka, lakini aliliambai Shirika la Habari la Hirondelle kwa njia ya
simu kwamba wako tayari kwa kusikiliza maelezo ya awali. ‘’Tutaomba
mteja wetu aachiwe kwa dhamana,’’ aliongeza.
Mchungaji Uwinkindi anashitakiwa kwa mauaji ya kimbari na kuteketeza kizazi.