UAMUZI wa kupinga uteuzi wa kadhi
mkuu na makadhi wa mikoa 14 uliofanywa na Sheikh Mkuu wa Tanzania,Mufti Shaaban
Simba umezidi kupingwa vikali baada ya baadhi ya viongozi na waumini wa
dini hiyo mkoani hapa kuupinga kwa nguvu zote huku wakisema ya kwamba
uteuzi huo unalenga kuwavuruga waislamu nchini.
Hivi karibuni Mufti Simba
alimtangaza Sheikh Abdallah Mnyasi kuwa kadhi mkuu na pia aliwateua
manaibu wake wawili,Sheikh Abubakar Zubeir na Sheikh Muhidini Mkoyogole.
Akipinga uteuzi huo,Imamu wa msikiti
mkuu mkoani Arusha,Mohammed Hambal alisema kwamba uteuzi huo una makosa makubwa
kwa kuwa kadhi mkuu huteuliwa na jopo la wasomi na sio mtu mmoja.
Alihoji kwamba taifa liko
kwenye hatua ya uundwaji wa mchakato wa katiba mpya kwa sasa na kilio cha
waislamu nchini ni uundwaji wa mahakama ya kadhi iingizwe kwenye katiba hiyo na
kushangaa uteuzi huo kufanyika wakati huu.
“Wakati tume ya kukusanya maoni
ikipita tunashangaa Mufti anamteua Kadhi mkuu kitu ambacho ni kinyume na
taratibu na mwogozo wa nchi”alisema Hambal
Hatahivyo,Hambal alihoji uteuzi huo
umezingatia katiba ipi kwa kuwa katiba ya nchi pamoja na katiba ya Bakwata
haina kpengere wala maelekezo ya mfumo wa uundwaji wa Mahakama ya kadhi.
Naye,mwenyekti wa msikiti
huo.Abdulazizi Mkindi alisema kwamba amepokea uteuzi wa Mufti kwa masikitiko
makubwa kwa kuwa uteuzi huo umefanywa na kikundi cha watu wachache kwa lengo la
kuwaongoza wailsamu nchini na taasisi zao.
Alisema kwamba masuala ya uteuzi wa
Kadhi mkuu yanapaswa kusimamiwa na watalaamu na wasomi waliobobea katika
sheria na sharia za kiislamu na si vinginevyo.
“Kilio cha mahakama ya kadhi ni
kilio cha wailsamu wote na si kilio cha Bakwata pekee,masuala ya kadhi
yanatakiwa yasimamiwe na wataalamu waliosomea sheria na sharia za kiislamu na
si watu wa hovyo”alisema Mkindi
Mustapha Kihago sanjari na Salim
Mvungi maarufu kama Shefu kwa upande wao walipinga uteuzi huo na kusema
kwamba wameshutushwa na wanahisi kwamba hizo ni njama za serikali
kuitumia taasisi ya Bakwata kuwavuruga wasilamu nchini.
Walimnyooshea vidole Mufti
Simba kuwa amelifanya suala la uteuzi wa Kadhi mkuu kama ajenda yake binafsi
wakati jambo hilo ni la wailsamu wote nchini.