Makamu wa Pili
wa Rais Zanzibar,Balozi Seif Ali Idd amesema juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kutafuta Meli kubwa kwa ajili ya wananchi wake zinaleta matumaini
kutokana na Watendaji husika waliopewa agizo hilo kulisimamia kwa nguvu zote
katika kulifanikisha.
Amesema Wizara
ya Fedha Uchumi na Maendeleo kwa kushirikiana na Wizara ya Miundombinu na
Mawasiliano ZanzÃbar tayari imeanza mikakati ya kupatikana kwa Meli hiyo ikiwa
ni pamoja na kukusanya pesa kutoka vyanzo mbali mbali vikiwemo vile vya
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Balozi Seif
ameyasema hayo leo alipokuwa akitoa hotuba yake ya kuahirisha kikao cha nane
cha Baraza la Wawakilishi ambacho kilianza June mwaka huu huko Mbweni nje
kidogo ya mji wa Zanzibar.
Amesema
Serikali ya Mapinduzi imejipanga vyema kukabiliana na matatizo yanayowakabili
wananchi likiwemo suala la usafiri wa baharini ambapo kupatikana kwa meli hiyo
kutaweza kutatua tatizo hilo ambalo limeonekana linaathiri sana uchumi wa
wananchi wa Zanzibar.
Aidha
amewahakikishia Wajumbe wa Baraza hilo kuwa ripoti iliyotolewa na Kamati ya
kusimamia matumizi ya Serikali PAC, Serikali inaifanyia kazi kwa umakini ili
kuweza kutoa maamuzi ya uhakika na sahihi.
Amewataka Wajumbe
hao kuendelea kuwa na subra ili suala hilo liweze kukamilika na Serikali
haitasita kueleza bayana juu ya maamuzi yake ambayo watayatoa.
Balozi
amefahamisha kuwa katika kuwajengea uwezo Akinamama tayari Serikali imetafuta
wataalamu wa kufanya uchambuzi yakinifu ili kuanzisha Benki ya Wanawake
Zanzibar.
Kuhusu suala la
utumiaji wa Madawa ya kulevya Balozi ameeleza kuwa suala hilo linawahusu
wananchi wote na kwamba Serikali inawahakikishia usalama wale wote ambao
wataweza kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na madawa hayo.
Akielezea juu
ya umuhimu wa amani ya nchi Balozi amesema kuwa Amani ya nchi ndio rasilimali
muhimu ambayo haifai kuchezewa na kwamba kila mwananchi anajukumu la kuienzi .
Amesema
Serikali iko makini katika kukabiliana na viashiria vyovyote vya kuhatarisha
amani ya nchi na haitochelea kumchukulia hatua mtu yeyote atakayeweza kuchezea
na kuhatarisha amani hiyo.
Balozi
amewataka wananchi ambao hawajapata nafasi ya kutoa maoni yao juu ya Katiba
mpya kujitayarisha kutoa maoni yao pale zoezi hilo litakapoendelea katika
maeneo ambayo bado halijafanyika.
Amesema ni
vyema wananchi kujitayarisha vyema kwa kuiga wenzao ambao waliweza kuitumia
nafasi hiyo vyema katika Mkoa wa Kusini Unguja na Kusini Pemba.
Kikao cha
Baraza la Wawakilishi kilichoanza mwezi wa Juni kimeahirishwa leo hadi Octoba
10 mwaka huu baada ya kupitisha makadirio ya matumizi ya fedha kwa Wizara zote
za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.