MJUMBE wa kamati ya
utekelezaji wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) mkoani Arusha,Diwani Kimai ameushauri
uongozi wa chama hicho ngazi ya taifa kujitathmini na kutafakari namna ya
kumaliza makundi mbalimbali yaliyopo ndani ya chama hicho kwa kuwa yanakidhorotesha chama chao.
Hatahivyo,mjumbe huyo
amezungumzia hatua ya baadhi ya makada wa chama hicho wanaohamia upinzani na
kusisitiza kwamba hilo
ni wimbi ambalo linapita na baada ya muda litatulia.
Kimai,alitoa tamko hilo juzi wakati
akizungumza na waandishi wa habari katika mgahawa wa Africafe uliopo jijini
Arusha ambapo alisema kuwa makundi ndani ya CCM yanahatarisha afya na ustawi wa
chama hicho.
Alisema kwamba ni vyema
uongozi wa taifa ukatafuta njia ya kutatua makundi yaliyopo ndani ya chama
hicho kwa lengo la kumaliza tofauti mbalimbali za kiitikadi zilizopo miongoni
mwa baadhi ya wanachama wake.
“Cha msingi tutulie uongozi
wa juu utafute njia ya kumaliza haya makundi kuanzia juu na kisha uje hadi
chini ili kuimarisha afya na ustawi wa chama chetu”alisema Kimai
Kimai,ambaye pia ni mjumbe wa
baraza la UVCCM wilayani Monduli alizungumzia kitendo chama baadhi ya makada wa
chama hicho wanaohamia upinnzani kwamba hilo ni wimbi linapita na baada ya muda
litatulia.
Alitolea mfano wa chama cha
NCCR Mageuzi kilichowika na kuvuma mnamo mwaka 1995 na kudai kwamba baada ya
muda kilipotea katika ramani za siasa nchini na kuiacha CCM ikiendelea kutamba
na kushika dola nchini.
Hatahivyo,alisema kwamba
ndani ya CCM hakuna kundi au mwanachama mwenye haki zaidi ya mwingine hivyo wanachama
wote wana haki hivyo wanastahili kutendewa haki hizo bila ubaguzi.