WANANCHI WAPOKEA FIDIA YA UWANJA WA AFCON 2027
Na Woinde Shizza,Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, amekabidhi hundi ya shilingi bilioni 2.3 kwa wananchi waliopisha eneo la ujenzi wa uwanja wa michezo utakaotumika kwa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) katika kata ya Olmoti, jijini Arusha.
Akizungumza katika hafla fupi ya makabidhiano hayo, Makalla alisema fedha hizo ni sehemu ya jumla ya shilingi bilioni 4.6 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya fidia kwa wananchi 12 waliotoa maeneo yao kwa mradi huo mkubwa wa kitaifa.
“Kati ya wananchi 12 waliopisha ujenzi huu, saba walishalipwa awali, na leo tunakamilisha malipo kwa watano waliobaki kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo,” alisema Makalla.
Amesema kuwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imetenga zaidi ya shilingi bilioni 340 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo wenye jumla ya hekari 83, ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Julai 2026 ili kuendana na ratiba ya mashindano ya AFCON 2027.
“Serikali imeweka mikakati madhubuti kuhakikisha miundombinu yote muhimu kama barabara, maji, na umeme inakamilika mapema kabla ya kuanza kwa mashindano ,Tunataka uwanja huu uwe wa viwango vya kimataifa,” aliongeza Makalla.
Mkuu huyo wa mkoa alimtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati.
Kwa upande wake, Mhandisi Denice Benito Mtemi, mwakilishi wa kampuni ya China Railway Construction, alisema ujenzi wa uwanja huo umefikia asilimia 71 hadi sasa.
“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kutoa fedha kwa wakati ,Uwanja huu utakuwa na nyasi asilia, vyumba vinne vya kubadilishia nguo, uwanja wa mazoezi ambapo hadi sasa kiwanja kimoja cha mazoezi teari tumekijenga na kipo katika hatua za mwisho na miundombinu yote ya kisasa kulingana na viwango vya kimataifa,” alisema Mtemi.
Hata hivyo, Mtemi alibainisha kuwepo kwa changamoto ya ucheleweshaji wa utoaji wa vifaa bandarini, jambo linalochelewesha kasi ya utekelezaji wa mradi.
“Tunaiomba Serikali kusaidia kutatua changamoto ya ucheleweshaji wa mizigo bandarini, Katika kipindi kilichopita, baadhi ya vifaa vilikaa bandarini kwa zaidi ya siku 27, hali iliyosababisha kazi kusimama kwa muda,” alifafanua Mtemi.
Aliongeza kuwa kukamilika kwa uwanja huo kutafungua fursa nyingi za ajira na uwekezaji kwa wananchi wa Arusha, hususan wanaoishi jirani na eneo la mradi.
About Woinde Shizza
This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.





0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia