BARAZA LA MADIWANI JIJI LA ARUSHA LAANZA RASMI LAWEKA MWELEKEO MPYA ,RUSHWA, BARABARA NA AJIRA KUPIGWA MSASA
Na Woinde Shizza , Arusha
Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha Mjini, Jacob Rombo, amewataka madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kusimamia kikamilifu mapambano dhidi ya rushwa na kutekeleza majukumu yao kwa kufuata utawala bora, baada ya zoezi la uapisho wa madiwani 34 wa jiji hilo, wakiwemo 25 waliochaguliwa na nane wa viti maalumu.
Rombo amesisitiza kuwa madiwani wanapaswa kuepuka kuingilia majukumu ya watumishi wa halmashauri hususan katika masuala ya mipango miji, na kusimamia viapo vyao kwa uaminifu ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Naibu Meya wa Jiji la Arusha, Julius Medeye , ameongeza kuwa madiwani wamefanya maamuzi sahihi na kwamba wanakwenda kufanya kazi moja tu, nayo ni kuwatumikia wananchi kwa uadilifu, ikiwemo kuboresha huduma za maji, barabara na miundombinu ya kijamii.
Amesema hatakubali kuwepo kwa makundi ndani ya baraza, na amehimiza umoja, utii, ushirikiano na mshikamano ili kufanikisha malengo yao.
Amewataka madiwani kutambua kuwa kila mmoja ana deni kwa wananchi na hivyo wanatakiwa kushughulikia changamoto za kata zao kwa bidii na uwajibikaji.
Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Arusha, Maxmillian Irangne, amempongeza Rais kusema kutokana na maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Samia Suluhu Hassan, baraza litaendeleza miradi iliyopo ikiwemo ujenzi wa jengo la jiji, soko la Kilombero na vituo vya afya.
Amebainisha kuwa ubovu wa barabara utakuwa kipaumbele, sambamba na usimikaji wa taa za barabarani na kamera za usalama.
Kadhalika, amesema asilimia kumi ya mapato itaelekezwa kwenye mikakati ya kutengeneza ajira kwa vijana, akisisitiza kuwa zaidi ya wawekezaji elfu moja wamevutwa kuja kuwekeza katika viwanda, hatua itakayosaidia kupunguza ukosefu wa ajira.
Sekta ya utalii nayo imepewa kipaumbele kutokana na nafasi ya Rais Samia kama kinara wa utalii duniani, huku michezo ikitarajiwa kuimarishwa kwa kuunda timu za jiji na kukarabati maeneo ya michezo.
Aidha, Meya ameitaka timu ya mkurugenzi kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuongeza uwezo wa jiji kutekeleza majukumu yake. Mkuu wa Wilaya ya Arusha amesisitiza umuhimu wa kulinda mazingira na kuusimamia mji kuhakikisha unafikia hadhi ya kimataifa, akiwataka watendaji kutoruhusu woga wala upendeleo na kushikilia kanuni, taratibu na misingi ya utawala bora kama walivyoapa.


0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia