RC MAKALLA AANZA KUSIKILIZA KERO ZA WANANCHI ARUSHA


 

Na Woinde Shizza , Arusha 

 Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, ameanza mchakato wa kusikiliza kero za wananchi kwa kukutana na wadau wa bodaboda, bajaji pamoja na wananchi, akisema serikali imelenga kupata suluhisho la kudumu kwa changamoto zinazowakabili.

Makalla alisema kazi ya bodaboda na bajaji ni halali kama zilivyo kazi nyingine, hivyo waendesha vyombo hivyo wanapaswa kuheshimiwa na kuwekewa mazingira rafiki ya kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria.

Alisema kero zote zilizowasilishwa zitashughulikiwa kwa mpangilio kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, huku akiwataka waendesha bodaboda na bajaji kushirikiana na vyombo vya usalama barabarani ili kuimarisha usalama na nidhamu.

Katika hatua nyingine, Makalla alizindua kampeni ya kusikiliza kero za wananchi na kuwaagiza wakuu wa wilaya kuanza mikutano ya hadhara katika maeneo yao ili wananchi wapate fursa ya kueleza changamoto zao moja kwa moja.

Akizungumza kwa niaba ya waendesha bodaboda, Katibu wa Umoja wa Bodaboda Jiji la Arusha, Khatibu Msemo, alisema sekta hiyo ina mchango mkubwa katika uchumi na utalii, sambamba na kusaidia familia nyingi kupata kipato cha kila siku.

Msemo alisema kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa mkoa, wamefanikiwa kupunguza vitendo vya uhalifu na kuwaingiza wanachama kwenye mfumo rasmi wa taarifa. Hata hivyo, alitaja changamoto za miundombinu mibovu ya barabara, ukosefu wa sare rasmi na mipango madhubuti ya maendeleo ya sekta hiyo.

Naye mmoja wa waendesha bodaboda, Msukuma, alilalamikia pikipiki zenye kelele kubwa na taa kali aina ya “disko”, akisema ni hatari kwa usalama wa barabarani.

Kwa upande wa bajaji, mmoja wa wawakilishi alisema licha ya migogoro ya awali ikiwemo migomo ya madereva, hali hiyo ilishughulikiwa, lakini akaomba serikali kurejesha baadhi ya vituo vya kazi vilivyohamishwa ili waendelee kutoa huduma kwa utaratibu rasmi.






About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia