MKUTANO WA UTOFAUTI WA KITAALUMA 2025: MAWAKILI WAJADILI MUSTAKABALI WA MAZINGIRA YA KAZI
Na Woinde Shizza , Arusha
Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimewakutanisha mawakili wa serikali kutoka mikoa mbalimbali nchini katika Mkutano wa Utofauti wa Kitaaluma 2025, ulioangazia namna utofauti, ujumuishaji na teknolojia mpya, hususan akili bandia (AI), vinavyoweza kuboresha mazingira ya kazi katika taasisi za umma.
Mkutano huo, uliandaliwa chini ya kaulimbiu “Kujenga Madaraja: Utofauti kama Chachu ya Umahiri wa Kitaaluma”, ulijikita kwenye mageuzi ya kiteknolojia yanayobadilisha sekta ya sheria na utumishi wa umma.
Makamu wa Rais wa TLS, Laetitia Ntagazwa, alisema bado taasisi nyingi za umma zinakabiliwa na changamoto za kuunda mazingira ya kazi yenye usawa, jambo linaloweza kuathiri mchango wa watumishi, ikiwemo mawakili wa serikali.
“Teknolojia inabadilika kwa kasi na inaleta majukumu mapya katika tasnia ya sheria. Ni muhimu kwa taasisi za umma kuwekeza kwenye mifumo inayothamini rasilimali watu bila kujali tofauti zao,” alisema Ntagazwa.
Washiriki walijadili pia masuala ya mizania kati ya kazi na maisha binafsi, umuhimu wa akili hisia kwa viongozi wa umma, na jinsi mabadiliko ya sekta ya fedha yanavyoathiri huduma za kisheria.
TLS imewahimiza mawakili wa serikali kutumia mkutano huo kama fursa ya kujengea uwezo, kuimarisha mitandao ya kitaaluma, na kubadilishana mbinu za kukabiliana na changamoto zinazotokana na teknolojia na mabadiliko ya kiuchumi.
Alizitaka taasisi za serikali kuongeza uwekezaji katika mafunzo ya teknolojia, mifumo salama ya kidijitali na ujenzi wa mazingira chanya ya kazi ili kuongeza tija, ubunifu na ufanisi wa kiutendaji.
Mkutano huu uliwaleta pamoja mawakili wote wa serikali na binafsi, ukisisitiza umuhimu wa ushirikiano na kujenga madaraja ya kitaaluma katika sekta ya sheria nchini.
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia