RC MAKALA AWATAKA MADIWANI ARUSHA KUBUNI VYANZO VIPYA VYA MAPATO

 



Na Woinde Shizza Arusha 

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makala, amewataka madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kuhakikisha wanawajibika ipasavyo katika kata zao kwa kubuni na kuendeleza vyanzo vipya vya mapato kuanzia ngazi ya kata hadi jiji.

CPA Makala ametoa maelekezo hayo leo jijini Arusha wakati akizungumza na madiwani wa Jiji la Arusha katika kikao cha Baraza la Madiwani, akisisitiza umuhimu wa uongozi wenye uwajibikaji katika kukuza mapato ya ndani.



Amesema madiwani wanapaswa kuboresha miundombinu katika vyanzo vya mapato, ikiwemo sekta ya maji na huduma za afya, ili wananchi wengi zaidi waweze kushiriki kikamilifu katika kulipa mapato na kuchangia maendeleo ya jiji.

Aidha, amewataka madiwani kuwa na umoja na mshikamano katika utekelezaji wa majukumu yao na kuachana na siasa zisizo na tija ambazo zinaweza kusababisha kudorora kwa ukusanyaji wa mapato.

CPA Makala ameongeza kuwa Halmashauri ya Jiji la Arusha inapaswa kuendeleza jitihada mbalimbali za ukusanyaji wa mapato sambamba na kuhakikisha jiji linakuwa safi, hatua itakayovutia wananchi na wawekezaji wa ndani na nje.

Pia amewahimiza madiwani kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao ili ihitimishwe kwa wakati na kwa viwango vinavyokusudiwa.










Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Lemara, Matuyani Laizer amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa maelekezo na ushauri alioutoa kwa Baraza la Madiwani, akiahidi kuyatekeleza kwa vitendo.

“Kwa niaba ya madiwani wenzangu, tumeyapokea maelekezo yote tuliyotolewa na Mkuu wa Mkoa na tunaahidi kuyasimamia kikamilifu, ikiwemo suala la ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha Jiji la Arusha linakuwa safi,” amesema laizer

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia