Monday, November 19, 2012
HOTUBA YA MHESHIMIWA NOVATUS MAKUNGA,MKUU WA WILAYA YA HAI NA MWENYEKITI WA KAMATI YA USHAURI YA WILAYA,DCC KWENYE UFUNGUZI WA KIKAO CHA KAMATI YA USHAURI YA WILAYA(DCC) YA HAI,TAREHE 19 NOVEMBA 2012
Posted by woinde on Monday, November 19, 2012 in | Comments : 0
-Mheshimiwa Clement Kwayu,mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Hai;
-Ndugu M.O.Humbe;Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Hai,
-Bibi Juliet Mushi,kaimu katibu tawala wa wilaya ya Hai;
-Waheshimiwa wawakilishi wa vyama vya siasa;
-Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini;
-Wakuu wa idara na vitengo katika halmashauri ya wilaya;
-Maofisa tarafa wote
-Maofisa watendaji wa kata;
-Wawakilishi wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali;
-Viongozi wa ngazi mbalimbali katika vijiji,vitongoji,mitaa pamoja na kata;
-Wageni waalikwa,
-Mabibi na Mabwana;
Naomba nianze kwa kumshukuru mwenyezi mungu kwa kutuwezesha kukutana katika kikao hiki cha kamati ya ushauri ya wilaya,DCC kikiwa ni kikao changu cha pili tangu nije hapa wilayani Hai kama mkuu wa wilaya.
Nichukuwe fursa hii kuwakaribisha wote katika mkutano huu.Ni matumaini yangu kuwa kikao hiki kitatusaidia kupata taarifa mbalimbali za utendaji zitakazotuwezesha kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.Hivyo basi nawaomba mshiriki kikamilifu kujadili yale yote yatakayowalishwa na kutoa maoni na mapendekezo kwa uwazi.
Ndugu wajumbe,Napenda kuchukua nafasi hii kutoa pongezi kwa kaimu katibu tawala wa wilaya bi Juliet Mushi kwa maandalizi mazuri ya kikao akishirikiana vyema na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ambaye pia ni katibu wa kikao Mkurugenzi Humbe.
Kuna baadhi ya watoa mada walipata taarifa ya kutakiwa katika mkutano huu ya muda mfupi na kaimu katibu tawala baada ya kushauriana nami kuhusiana na aina ya mada ambazo tunazihitaji kwa hiyo tunawaomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza.
Ndugu wajumbe;Katika vikao vyetu hivi kwa maana kile cha kwanza cha tarehe 19/11/2012 na hiki cha pili kwa kiasi kikubwa tumejaribu kubadilisha mpangilio kwa kuhakikisha taasisi zote ambazo kwa namna moja ama nyingine zinashiriki katika kuwahudumia wananchi zinapata nafasi ya kutoa mada.
Imetubidi kuzama na kuangalia kwa kina hali ya sasa hivi ya maisha na mabadiliko makubwa yanayotokea hapa Hai na duniani kwa ujumla na ndiyo maana tukaona ebu tuboreshe aina ya vikao vyetu hivi.
Lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kwamba malengo ya kikao hiki ya kuwa kamati ya ushauri ya wilaya linatimizwa kwa kugusa kama siyo maeneo yote basi sehemu kubwa ya maeneo ambayo mwisho wa siku yatamhusu mwananchi katika maisha yake ya kila siku.
Ndugu wajumbe;ajenda za kikao chetu cha leo zina mambo makuu nane.Tutakuwa na mada kuhusiana na mazingira kama wengi mnavyofahamu tupo katika operesheni ya kudhibiti uharibifu wa mazingira na kampeni ya upandaji wa miti.
Aidha tutakuwa na mada kuhusina na mkakati wa kufufua zao la kahawa ambalo katika miaka ya nyuma ndilo lilikuwa tegemeo kubwa la uchumi wetu lakini pia tutakuwa pia na mada kuhusiana na uimarishaji na ufufuaji wa elimu ya ufundi.
Licha ya mada hizo lakini pia tumetoa nafasi kwa taasisi zetu muhimu kuja kutueleza maendeleo ya huduma wanazotoa likiwamo Shirika la Umeme Nchini(TANESCO),Mamlaka ya Mapato(TRA),Jeshi la Polisi,Bodi za maji pamoja na mabenki.
Ndugu wajumbe,Kwa kuwa hutuba yangu hii nayo ni mada inayojitosheleza pia itakuwa siyo vibaya kujadili masuala ambayo nitajitahidi kuyazungumza kwa kirefu ambayo ni haya yafuatayo;
Moja,suala la utawala bora,mbili uwepo wa amani,usalama na utulivu,tatu mikakati ya kutokomeza upikaji na unywaji wa pombe haramu ya gongo pamoja na unywaji wa pombe nyakati za kazi na nne ni utatuzi wa migogoro ya ardhi ikiwemo ya viwanja pamoja na ya wakulima na wafugaji.
Ndugu wajumbe,tano ni uboreshaji wa miundombinu wa usafiri na sita mpango mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji maji wakati saba ujenzi wa maabara katika sekondari za kata katika kipindi cha miaka miwili ijayo.
Suala la nane ambalo nitalizungumzia ni uzinduzi wa awamu ya tatu ya TASAF na tisa maandalizi ya jamii kushiriki katika mkutano wa ushirikiano kwa manufaa ya wote yaani smart partnership.
UTAWALA BORA
Ndugu wajumbe,Changamoto ya masuala yenye mwelekeo wa utawala bora limekuwa tatizo kubwa sana katika wilaya yetu kuanzia sisi tulioko ngazi ya wilaya mpaka viongozi wetu walioko katika ngazi za vijiji.
Aidha Uwajibikaji limekuwa tatizo kubwa sana likitugusa sisi viongozi wa kisiasa mpaka wataalamu wetu wa ngazi mbalimbali huku tatizo kubwa likiwa kusahau majukumu yetu na kudai posho hata katika masuala yanayolenga kuwahudumia wananchi kwa kutumia muda wa kawaida wa saa za kazi ndani ya vituo vyetu vya kazi.
Kwa upande wa changamoto hii nitaieleza katika maeneo mawili tu ambayo sisi kama viongozi tunaulazima mkubwa wa Kujipanga kukabiliana nazo hadi kufikia katika kikao kijacho.
Changamoto ya kwanza inahusu ufanyikaji wa vikao vya kisheria katika ngazi za vijiji na kata.Hilo limekuwa tatizo kubwa sana katika wilaya yetu.Kila unapita katika vijiji malalamiko makubwa ni ufanyikaji wa mikutano ya vijiji na hasa ajenda inayohusu kusomwa kwa taarifa ya mapato na matumizi.
Kwa uchache sana pia tuna tatizo la ufanyikaji wa mikutano ya kamati za maendeleo za kata yaani WDC katika baadhi ya kata.
Changamoto hizo zote siyo siri zinafahamika vizuri kwa maofisa wetu wa ngazi za tarafa na kata hususani kwa ufanyikaji wa mikutano mikuu ya kijiji na kwa ile ya ngazi ya kata zinafahamika katika halmahauri yetu ya wilaya.
Sasa tunalenga kumaliza tatizo la ufanyikaji wa vikao vya kisheria katika ngazi ya vijiji.Agizo langu kwa maofisa tarafa na maofisa watendaji wa kata,hakikisheni kila mwezi mnaleta taarifa ama ratiba za vikao vya kisheria katika vijiji vyenu zenye kuanisha ajenda zote,mahudhurio na maamuzi.
Changamoto hii tayari imesababisha shinikizo kubwa kwa wananchi katika maeneo mengi kutaka kuuondoa uongozi wao.Ni kweli katika maeneo mengi kuna tatizo kubwa la viongozi kutofuata taratibu zikiwemo usimamizi wa fedha za umma.
Michango ya wananchi imekuwa haisimamiwi ipasavyo lakini kibaya zaidi wananchi wanachangishwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo bila kupewa taarifa za mapato kwa maana ya fedha zilizokusanywa pamoja na matumizi yake.
Sisi tumesema basi,hatutaendelea kumvumilia ama kuwavumilia viongozi wa namna hiyo bila ya kujali chama anachotoka.Tutahakikisha taarifa za viongozi wanaoshindwa kusimamia fedha za wananchi tunazifikisha kwa wananchi wenyewe baada ya kufanya ukaguzi na kuwapa wao wenyewe nafasi na fursa ya kuendelea ama kutoendea na aina ya viongozi hao.
Lakini baada ya hatua hizo za wananchi,palipo na ushahidi wa kutosha tutahakikisha wote ambao watabainika ni mchwa wanaotafuna fedha za wananchi na kutumia vibaya madaraka yao tunawafikisha katika mkondo wa kisheria.
Upande wa pili wa changamoto hii ni uwajibikaji.Kwa makusudi kabisa sasa tumehamua kufanya kazi zetu vijijini na siyo ofisini,kuanzia mimi mwenyewe pamoja na mkurugunzi na wakuu wote wa idara tumeshajipangia ratiba ya kufanyakazi zaidi katika maeneo ya vijijini huku tukitenga siku chache sana za kukaa ofisini.
Lakini kwa upande wa masuala ya utawala bora nimalizie kwa kuwataka viongozi wenzetu wa ngazi za vijiji kuhakikisha mnasimamia kwa ukaribu miradi yote inayotekelezwa katika maeneo yenu.
Tunaangalia uwezekano wa kuandaa kwa njia rahisi sana nyaraka za mchanganuo wa gharama za utekelezaji wa mradi yaani BOQ ili iwe rahisi kwenu kufuatilia hatua kwa hatua.
AMANI,USALAMA NA UTULIVU
Katika dunia ya leo,matishio ya uhalifu yamekuwa mengi na ya aina mpya ambayo hatukuizoea.Katika kukabiliana na hali hiyo kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na mawasiliano na mashirikiano ya kiutendaji kati ya taasisi na taasisi katika ngazi zote kuanzia wilaya,tarafa,kata hadi vijiji,mitaa na vitongoji.
Wote tunafahamu kwamba jukumu hili hatutaweza kuwaachia polisi peke yao kutokana na uchache wao mfano,mfano sasa hapa nchini tukigawa idadi ya askari polisi waliopo na wananchi tutaona kwamba inabidi askari mmoja kuwapa huduma ya usalama watu 1,128
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ilani ya chama tawala vinatambua na kubainisha wazi kuwa jukumu la ulinzi na usalama ni la kila Mtanzania.
Ibara ya 28 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa wajibu wa kila mwananchi kuwa mlinzi wa mali zake na za taifa pamoja na wananchi wenzake.
Aidha ibara hiyo hiyo katika kifungu cha pili B,pamoja na sheria za serikali za mitaa sura ya 287 na 288 inaweka bayana jukumu la kusimamia na kutekeleza sheria na ulinzi wa wananchi mikononi mwa serikali za mitaa.
Ndugu wajumbe,matukio ya hivi karibuni ya vurugu zenye mwelekeo wa kidini nchini yanasikitisha na kusononesha.Tunashukuru mungu kwamba katika wilaya yetu hali imeendelea kuwa shwari na tuendelee kushirikiana katika kudumisha amani hasa kwa kudhibiti migogoro yote yenye mwelekeo wa kidini.
Lakini pamoja na wilayani kwetu kuwepo kwa hali ya amani,lakini bado kunatatizo la kuanza kujitokeza kwa vitendo vya ujambazi hasa katika mji wetu wa Hai.Ni vyema tukachukuwa hatua mapema sana kabla ya hali hiyo haijakomaa.
Hali hiyo ingawa inahitaji mikakati ya kudumu lakini katika uhalisia wake inaweza kuwa mbaya zaidi katika kipindi hiki cha kuelekea katika msimu wa sikukuu za mwishoni kwa mwaka yaani krismasi na mwaka mpya.
Wote tunafahamu kwamba katika kipindi hicho ndugu zetu kutoka kila kona ndani na nje ya nchi watakuwa wanarejea na hivyo ongezeko hilo kuwa na nafasi kubwa ya kuleta na kuvuta pia na idadi kubwa ya wananchi ambao siyo raia wema.
Katika kutafuta mbinu ya kukabiliana na hali hiyo,nimekaa na wenzangu viongozi wa ngazi ya wilaya na siku chache zijazo nitakutana na viongozi wa ngazi za vitongoji,mitaa na vijiji wa kata za Hai mjini na Kwasadala kuweka mkakati wa kukabiliana na hali hiyo.
Tunaanza na maeneo hayo kwa majaribio ingawa maeneo mengine hatutayaacha hivi hivi.Lengo ni kuwa na doria ya saa ishirini na nne kwa kuwashirikisha askari mgambo kwa uratibu wa jeshi la polisi.
Katika kufanikisha mkakati huo tutahitaji sana ushirikiano wa wananchi wakiwemo wafanyabiashara pamoja na viongozi wa kisiasa hasa madiwani.
POMBE HARAMU YA GONGO
Ndugu wajumbe,sote tnafahamu kundi kubwa la vijana katika wilaya yetu linavyoendelea kuangamia kutokana na kukithiri kwa unywaji wa pombe haramu ya gongo.
Kwa mwananchi yeyote mwenye uchungu na wilaya yetu ya Hai lazima suala hili litamgusa kwani hivi sasa ni janga la wilaya na hali hii ikiendelea baada ya miaka mitano mpaka kumi ijayo hatutakuwa tena na wilaya ya Hai yenye uhai.
Lakini baya zaidi baadhi ya viongozi wenzetu katika vijiji na vitongoji wamekuwa vinara katika kuhakikisha biashara hii ya pombe haramu ya gongo inaendelea kudumu.
Rai yangu kwa kikao chetu muhimu kutoa ushauri na mapendekezo ambayo yatatuhakikishia kwamba tunaweka mkakati wa kupambana na watengenezaji,wauzaji na watumiaji wa pombe haramu ya gongo na kuhakikisha imekwisha kabisa.
Nilikutana na tatizo hilo mara tu baada ya kuhamia wilayani hapa na kujitahidi kuanza kuchukuwa hatua lakini nikabaini kunahitajika maandalizi makubwa hasa katika uwezeshaji wa kufanyika kwa operesheni kubwa hasa kwa keshi la polisi.
Lakini sisi kama kamati ya ushauri ya wilaya hatuna jinsi lazima tuchukuwe hatua za makusudi kukomesha pombe hiyo haramu.
Lakini kwa upande huo huo,sasa tunahitaji kuingia katika maamuzi magumu kwa unywaji wa pombe halali lakini nyakati za kazi yaani kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa kumi na moja.
Hivi sasa wilayani kwetu imekuwa kama vile ni utaratbu wa kudumu wa makundi ya vijana mpaka wazee kuanza kunywa pombe majira ya asubuhi.Tabia hii kwa kiasi kikubwa imeanza kushusha hali ya uchumi,lazima tubadilike na kusimamia sheria kwa kuhakikisha pombe inaanza kuuzwa jioni na siyo asubuhi na mapema.
MAZINGIRA
Ndugu wajumbe,mazingira ndiyo uhai wetu.Kwa kutambua hilo na kasi kubwa iliyojitokeza ya ukataji wa miti,serikali katika mkoa wa kilimanjaro kwa nia nzuri kabisa ilisitisha vibali vya ukataji wa miti kwa ajili ya mbao na magogo.
Maamuzi haya hayakuchukuliwa kwa ajili ya manufaa ya mtu binafsi au kwa lengo la kuwakomoa wananchi,bali kuthamini ustawi wa maisha ya jamii yote ya mkoa wa Kilimanjao wakiwemo wakazi wa wilaya ya Hai.
Babu zetu walifanyakazi kubwa ya kupanda miti kwa kasi na ndiyo maana wengi wetu wakati tunazaliwa tulikuta wilaya ya Hai ikiwa na mazingira ya kuvutia yenye mvua za kutosha zilizotusaidia kuendesha shughuli zetu za kilimo na ufugaji kwa ufanisi mkubwa.
Kibaya kilichojitokeza hivi sasa bila ya kuthamini jitihada za wazazi wetu za kupanda miti na kuitunza hivi sasa tumekuwa tukikata miti hii kwa kasi kubwa sana na kuharibu mazingira hali ambayo imesababisha hata msimu wa mvua usiwe wa uhakika huku joto likiongezeka maradufu.
Kutokana na hali hiyo ndipo serikali mkoani Kilimanjaro ikachukuwa maamuzi magumu ya kusitisha vibali vya ukataji wa miti kwa ajili ya mbao na magogo.
Ndugu wajumbe,cha kushangaza katika maeneo mengi ya wilaya ya Hai viongozi wenzetu wamekuwa wakishiriki kikamilifu kuhujumu operesheni hii kwa kusimamia ukataji huo wa miti na pia kutoa vibali.
Mifano mingi tunayo na naendelea kuwashukuru na kuwapongeza wananchi ambao wamekuwa wakitupigia simu na wengine kuja moja kwa moja ofisini na kuwafichua waharifu hao wa mazingira.
Kadhalika niwapongeze viongozi majadiri ambaokwa v wamekataa kushiriki katika udhalimu wa kuharibu mazingira.
Baadhi ya mifano ambayo inasikitisha ni pamoja na ukataji wa miti unaofanyika katika mto Kikafu katika eneo la Makoa.Tathimini inaonyesha wastani wa mti mmoja ama miwili mikubwa aina ya mkufi ukatwa kila wiki na mbao zake kuuzwa katika kijiji cha Kwasadala
Tatizo kama hilo pia lipo katika vijiji vyote vilivyoko pembezoni mwa mto Kikafu na pia vijiji mbalimbali vya ukanda wa tambarare hasa Chemka kwa ajili ya uchomaji wa mkaa
Tumeanza kuchukuwa hatua kwa kushughulika kikamilifu na eneo la Makoa katika mto Kikafu pamoja na kijiji cha Chemka.
Katika la mazingira hatuna mbadala wala mzaa tena,viongozi wetu katika ngazi za vijiji na kata tunawaheshimu na kuwathamini lakini kwa la mazingira muda wa mzaa umekwisha na hatutasita kumkamata kiongozi yeyote yule na kumfikisha katika mikondo wa sheria.
Lakini sanjari na hilo hivi sasa tupo katika kampeni ya upandaji wa miti katika maeneo mbalimbali.Pamoja na mkakati huo lakini imebainika bado vijiji vingi vimelala usingizi na hata shule za msingi na sekondari.
Tumeagiza na kuwaandikia barua kwamba kila kijiji na shule vinatakiwa kuanzisha kitalu ama bustani ya miche ili msimu wa mvua utakapoamza basi tusipate tatizo la miche.
Kwa bahati nzuri baadhi ya taasisi zimejitolea kufadhili mikakati ya kuanzisha kitalu cha miche mashuleni ikiwemo inayosimamia uwanja wa ndege wa kimataifa wa kilimanjaro yaani KADCO.
Viongozi wote mliopo ndani ya ukumbi hakikisheni mnalwenda kusimamia zoezi la maandalizi ya upandaji wa miti kwa kukagua vitalu vya miche vya vijiji na shule na taarifa kuzileta wilayani
KILIMO CHA UMWAGILIAJI
Wilaya yetu ya Hai ina eneo linalofaa kwa kilimo la hekta 46,506 kati ya hizo hekta 27,406 zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji maji lakini zinazotumika ni hekta 17,030.
Lazima kuongeza eneo la umwagiliaji maji hasa katika maeneo ya kata za Machame kusini,Machame weruweru,Masama Rundugai na Masama Magharibi.
Tayari vikao vya kitaalamu vya halmashauri yetu ya wilaya vimeanza kuweka mkakati wa kuhakikisha kwamba sasa tunaingiza wilaya yetu katika kilimo cha umwagiliaji ili kuondokana kabisa na utegemezi wa kuwa omba omba wa chakula
UFUFUAJI WA ZAO LA KAHAWA
Uzalishaji wa zao la kahawa katika miaka minne umeonyesha kupungua mwaka hadi mwaka mfano mwaka 2007/2008 ulikwa tani 2,568 na mwaka uliofuata wa 2008/2009 ulikuwa tani 2,061.3 ilihali mwaka 2009/2010 ulikuwa tani 1,150.4 wakati kwa msimu wa 2010/2011 ulikuwa tani 1,069.6.
Lazima kuanzia sasa tuje na mkakati wa kufufua zao hilo ambalo ndiyo nembo ya wilaya yetu ya Hai.
UIMARISHAJI WA MIUNDOMBINU YA USAFIRISHAJI
Wilaya ya Hai ina barabara zenye urefu wa kilometa 466.2 kati hizo kilometa 32 ni za barabara kuu,kilometa 42 ni za mkoa,kilometa 175.93 ni za wilaya na kilometa 150.27 ni za vijiji na kilometa 66 ni za eneo la Hai mjini.
Lakini barabara zinazoweza kupitika kwa nyakati zote ni zenye jumla ya kilometa 235.53 sawa na asilimia 50.82
Barabara hizo ni muhimu hasa katika zama hizi ambazo zao la kahawa limeanguka.Wilaya yetu kwa kiasi kikubwa sasa inategemea zao la ndizi kama la biashara.
Hivyo bila ya kuwa na barabara nzuri zitakazowezesha kurahisisha usafirishaji wa ndizi kutoka migombani hatutakuwa tumewsaidia wananchi wetu kuendesha maisha yao.
MASUALA YA ARDHI
Ndugu wajumbe,migogoro ya ardhi imekuwa sehemu ya maisha katika wilaya yetu ya Hai na kutuchukulia muda mrefu sisi viongozi wa kuishughulikia badala ya kusimamia masuala mengine ya maendeleo.
Migogoro hii imegwanyika katika maeneo tofauti tofauti ipo ambayo inatuhusu sisi kama wasimamizi wa ardhi lakini ipo pia inayozihusisha familia.Kuna tatizo kubwa la ugawaji viwanja kwa mtu zaidi ya mmoja katika maeneo ambayo halmashauri yetu ya wilaya imeweza kupima viwanja na tatizo hilo linajitokeza tangu mji huu wa Hai unaanzishwa .Lazima tuje na mwarobaini kwa kukomesha tatizo hilo kama ilivyo kwa maeneo mengine nchini.
Katika suala la ardhi pia kuna tatizo ambalo lina kuja mbele yetu ya kuibuka kwa makazi yasiyokuwa na mpangilio na mfano halisi ni eneo la Kwasadala.
Kwa takwimu zilizopo katika wilaya yetu kuna jumla ya maeneo ama viwanja vilivyopimwa vipatavyo 7,045 ambapo kati hivyo viwanja ambavyo visivyoendelezwa ni 1,244.
Hivi sasa tumebuni mpango wa kuwa na mji uliopangika pale eneo la Kwasadala.Tumeanza majadiliano na viongozi ili kuanza mchakato wa kupima eneo hilo kwa kufuata sera ya ardhi.Lile ni eneo la mji unaokuwa kwa kasi tunalenga kupima viwanja kwa mwananchi mwenye eneo kubwa tutaangalia jinsi bora ya kufidiana lengo likiwa kupata mji wa kisasa zaidi.
Lakini kwa wenzetu ambao walibahatika kupata viwanja vilivyopimwa hasa eneo la uzunguni ni vyema sasa wakaanza kuviendeleza.Baadhi ya maeneo hayo yamekuwa vituo vya vibaka.
Lakini eneo la pili ambalo nalo tupo mbioni kuliboresha ni lile lililoko pembezoni mwa uwanja wa ndege wa Kilimanjaro ambalo linabainishwa kama la EPZE.
Aidha katika eneo la ardhi pia Kuna migogoro ya mipaka kati ya vijiji vya Uduru na Nshara hali ambayo imesababisha kushindwa kukamilisha mchakato wa upimaji wa mipaka.
Kadhalika kuna mgogoro wa mipaka kati ya kijiji cha Kwasadala na Mbatakero ambao nao unaathiri kwa kiasi kikubwa sana mipango mbalimbali ya maendeleo.
Migogoro yote hiyo, jitihada za usuluhishi zipo katika hatua nzuri na kwamba tunatarajia katika kipindi kifupi kijacho itakuwa imemalizika kabisa
Lakini katika changamoto za ardhi iliyo kubwa ni migogoro ya wakulima na wafugaji.Ingawa wilayani kwetu haijajitokeza kwa kiwango cha juu lakini migogoro hiyo ipo kutokana na matukio mbalimbali likiwemo la mama mmoja aliyekatwa panga katika kijiji cha Kawaya na matukio yaliyowahi kutokea miaka michache iliyopita ya kundi la wafugaji kuvamia kituo cha umeme cha Kikuletwa na kufanya vurugu kubwa na baadaye kuwapora walinzi silaha.
Wilaya ya Hai ni miongoni mwa wilaya ambazo zina tishio kubwa la kuvamiwa na makundi makubwa ya mifugo yakitokea katika wilaya za jirani za Simanjiro,Longido,Monduli pamoja na Siha.
Wilaya yetu ya Hai ina eneo la hekta 27,297 zinazofaa kwa malisho ya mifugo.Lazima tujipange vyema kudhibiti eneo hilo kwa kuhakikisha kwamba linatumiwa ipasavyo kwa idadi ya mifugo iliyopo lakini bila kusababisha migogoro ya wakulima na wafugaji.
Tunapanga kuwa na mkutano mkubwa wa wadau katika kuhakikisha tunaweka mkakati wa kudhibiti kabisa migogoro ya wakulima na wafugaji wilayani mwetu.
MFUKO WA MAENDELEO YA JAMII(TASAF)
Serikali imezindua awamu ya tatu ya TASAF ,uzinduzi huo ulifanywa na mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Agosti 2012.
Madhumuni ya awamu hii ya TASAF ni kuwezesha kaya maskini kuongeza kipato,fursa na uwezo wa kugharamia mahitaji yao muhimu.
Walengwa ni kaya maskini zilizo katika mazingira hatarishi na itakuwa na sehemu kuu nne ambazo ni ;
-Mpango wa kitaifa wa kunusuru kaya maskini na zilizo katika mazingira hatarishi.
-Programu ya kuinua hali ya maisha kupitia uwekaji akina na shughuli za kiuchumi
-Miundombinu inayolenga maeneo mahsusi
-Kujenga uwezo
Awamu hii inatarajia kugharimu shilingi bilioni 408 ambazo sawa na dola za Marekani 272 na utekelezaji wake kufanyika kwa miaka kumi kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano
Utekelezaji utaanza kwa kujenga uwezo wa watendaji na wahusika katika ngazi ya taifa,mkoa,halmashauri,wilaya,kata na vijiji,mtaa na shehia.
Kadhalika kujenga mifumo na kutambua kaya maskini ni miongoni mwa shughuli zitakazotekelezwa mwanzo.
Ndugu wajumbe,Ni vyema kujipanga kuanzia sasa kuhakikisha fursa hiyo katika wilaya yetu tunaitumia ipasavyo kuyakwamua kiuchumi makundi ambayo hayana uhakika wa kupata mahitaji yao ya kila siku.
USHIRIKIANO KWA MANUFAA YA WOTE
Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa ujulikanao kama Global 2013 Smart Partnership Dialogue ambao kwa kiswahili ni ushirikiano kwa manufaa ya wote.
Mkutano huu utafanyika jiji Dar-es-Salaam kuanzia tarehe 24-28 Mei 2013 na unafanyika hapa nchini kutokana na ahadi aliyoitoa Mhe.Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete wakati akihidhuria mkutano kama huo huko Petrojaya,Malaysia mwezi Juni 2011.
Mikutano ya smart partnership dialogue ni tofauti na mikutano mingine kwani hii ni jukwaa la majadiliano kati ya serikali na jumuia mbalimbali za wananchi kuhusu jambo lolote lenye manufaa kwao na ambalo kwa njia moja ama nyingine litachangia katika kuleta maendeleo yao kijamii na kiuchumi.
Viongozi wa ngazi mbalimbali wa serikali wakiwemo wa ngazi ya juu ukaa pamoja kama watu wa ngazi sawa na jumuia za wananchi zikiwemo za vijana,wasomi,wafanyakazi,wafanyabiashara,waandishi wa habari,wanasanaa na utamaduni,wanasiasa na madhehebu ya dini.Kwa ujumla jumuia hizo hujulikana kama smart partnership links.
Lengo kubwa la majadiliano hayo ni kupata maoni na mawazo kutoka kwa watu wa kawaida kuanzia ngazi ya chini mpaka juu.Kwa msingi huo,dhana hii inatambua kwamba kila mtu anao mchango wake kwenye jumuia anayoishi na kwamba utendaji wa kazi wa mtu mmoja unaathiri utendaji wa kazi wa mtu mwingine.
Hivyo basi kwa kawaida nchi inayoandaa mkutano huo ina wajibu wa kuanza kuandaa majadiliano ya kitaifa kwa mahudhui yale yale na kwa mkutano huo mahudhui yake ni Leveraging Technology for Africa's Social Economic Transformation:The Smart Partnership Way.
Kwa nchi kama Tanzania,changamoto kubwa ni kupata teknolojia na ubunifu ambao utaongeza tija,kupunguza muda na gharama za uzalishaji,upanuzi na ushindani wa biashara kuanzia ngazi ya kifamilia hadi taifa na kitaifa katika nyanja zote za uzalishaji na utoaji wa huduma.
Kinachotakiwa kabla ya mkutano huo lazima tuwe na makundi tayari ya kuchangia.Katika wilaya yetu naamini kuna wagunduzi hivyo ni lazima tuwe na mkakati wa kuwabaini na kuwaendeleza ili kazi zao zisaodie kuendeleza sayansi na teknolojia.
UFUGAJI WA NYUKI
Miongoni mwa sekta za uzalishaji katika maeneo mbalimbali nchini ambazo inayokuwa kwa kasi ni ufugaji wa nyuki.
Ufugaji wa nyuki umekuwa chanzo kikubwa sana cha mapato katika jamii lakini kwa wilaya ya Hai bado kabisa haijachangamka.
Ufugaji wa nyuki unafanyika zaidi katika eneo la ukanda wa juu hasa vijiji vinavyopakana na msitu wa hifadhi ya mlima Kilimanjaro.
Kwasasa kuna jumla ya vikundi kumi na tatu vinavyojishughulisha na shughuli za ufugaji wa nyuki.
Kuna jumla ya mizinga 13,200 ambapo wastani wa uzalishaji wa asali ni kilo 4,900 na nts kilo 192
Ndugu wajumbe ebu tutokea na mkakati wa kuingia katika ufugaji wa nyuki,hivi sasa kutokana na mfumo wa maisha ambao unahitaji umakini mkubwa katika mipango ya chakula,asali imekuwa na soko kubwa sana ndani na nje ya nchi.
Kwa kumalizia nawashukuru sana kwa kunisikiliza na kikao chetu kimefunguliwa rasmi.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia