Viongozi wa dini hapa nchini wametakiwa kutoruhusu
wanasiasa kuyatumia madhabahu yao na nyumba za ibada kuzungumzia mambo ya
kisiasa katika wakati huu wa uchaguzi ili kuilinda amani hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Jukwaa la
wakristo hapa nchini na Askofu wa kanisa
la Aglikana la mt.Kilimanjaro Stanley Hotay kwenye kongamano la mbegu ya amani
Tanzania lililofanyika jijini hapa na
kuwashirikisha viongozi wa madhehebu ya kikristo kanda ya kaskazini.
Alisema kuwa mimbari zetu zisitumiwe kinyume cha
sheria kwa kuwaelekeza waumini wao kuhusu mgombea ama chama cha siasa cha
kukichagua wao wapewe uhuru wa kufanya maamuzi yao ni yupi wa kumpa kura zao
kwa kuwa wanasiasa hao wote ni waumini wao.
Aliwataka viongozi hao wa dini kukataa rushwa za
pesa,na bakshishi zingine kwa ahadi ya kulindwa na kupewa nyadhifa za kuteuliwa
iwapo wanasiasa hao watapata nafasi hilo ni suala la kuliepuka kabisa.
‘’Mikusanyiko sio kipindupindu tukatae kusimama kwenye
majukwaa ya kisiasa kuwanadi wagombea na pia kwenye nyumba zetu za ibada
kutompigia debe mwanasiasa yeyote hiyo itatuepusha na kuvuruga haki ya waumini
wetu ya kujichagulia wanaomuona anawafaaa’’alisema Hotay.
Aidha alilitaka jeshi la polisi hapa nchini kupitia
kwa mkuu wa jeshi hilo Ernest Mangu kuangalia kutenganisha Maandamano,Mikutano
ya hadhara na mikusanyiko mbali mbali ya kidini na kisiasa kwamba vibali vya
mikusanyiko ya kisiasa wapewe wakuu wa polisi na vibali vya mikusanyiko ya
kidini wapewe wakuu wa wilaya.
Alisema kuwa hilo litaepusha jeshi la polisi au waziri
kutoa adhabu ya jumla na kusababisha viongozi wa dini pamoja na waumini wao
kujenga chuki kubwa kwa serikali yao na kusababisha viongozi wa kidini kufikia
kuzungumzia katika vikao vya mara kwa mara kwamba serikali inaagenda ya siri na
viongozi wa dini.
Alikemea siasa za matusi na kuchafuana katika majukwaa
na badala yake aliwataka kutumia lugha za staha na kuheshimiana,huku akiwataka
kutoa uhuru wao wa siku ya jumapili kuabudu badala ya kuifanya ndio siku ya
uchaguzi.