Baadhi ya wananchi wakiwa kwenye mkutano huo.
BAADHI ya wananchi na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
wamelazimika kuuzuia msafara wa mgombea mwenza wa nafasi ya urais leo
alipokuwa njiani akitokea Wilaya ya Same kuelekea Wilayani Mwanga mkoani
Kilimanjaro huku wakimuomba awasalimu na kuzungumza nao, kabla ya kuendelea
na safari yake.
Bi. Samia Suluhu alilazimika kuusimamisha msafara wake baada ya wananchi
hao kusogea zaidi barabarani wakati akipita huku wakinyoosha mikono ya
kumuomba asimame ili azungumze nao eneo la kilometa chache kabla ya kuingia
njia panda. Wananchi hao wengi wakiwa wakinamama walimsimamisha kwa kuingia
pembezoni mwa barabara alipokuwa akipita na hivyo kulazimika kusimama kwa
dakika chache na kuzungumza nao.
Akizungumza aliwaambia amefarijika na kuwaona na mapenzi makubwa na chama
chao hivyo kuwaeleza kuwa yeye ni mwanamke pia na anajua kwa karibu kero
ambazo wanakabiliana nazo akinamama sehemu mbalimbali na kuahidi endapo
watapata ridhaa pamoja na Dk. John Magufuli atahakikisha anasimamia vizuri
utaratibu wa kuwawezesha akinamama kupitia vikundi vya kijamii ili waweze
kujikwamua kiuchumi pamoja na familia zao.
Alisema yeye ni mwanamke mzazi anatambua shida wanazokumbana nazo akinamama
hasa kwenye wodi za wazazi hivyo akifanikiwa kuingia madarakani
atahakikisha anasimamia ipasavyo ilani ya chama ambayo imeeleza vizuri juu
ya uboreshaji huduma za afya ikiwemo wodi za akinamama na hali ya
upatikanaji madawa.
"...Matatizo ya wanawake nayafahamu vizuri wala sisimuliwi maana na mimi ni
mzazi nimeingia wodi ya wazazi mkitupa ridhaa na mwenzangu (mgombea urais,
Dk. Magufuli) nitahakikisha nayasimamia haya vizuri," alisema Bi. Suluhu
akizungumza muda mfupi na wananchi waliomzuia barabarani wakiomba awasalimu.
Alisema kero ya maji imekuwa inawatesa akinamama kwa kutumia muda mwingi
kutafuta maji na kushindwa kuzalisha uchumi wa familia ipasavyo, hivyo
Serikali ya CCM imeanza mradi wa kutoa maji katika Bwawa la Nyumba ya Mungu
na kuyaingiza katika vijiji vyenye shida ya maji.
Aidha akizungumza katika mkutano mkubwa wa hadhara Mwanga ameisikia kero ya
uhaba wa mabweni kwa wanafunzi wa kike suala ambalo linachangia kwa kiasi
kikubwa mabinti hao kutiwa mimba na kukatisha masomo eneo hilo na kudai
suala hilo lipo katika ilani ya CCM mwaka huu na litashughulikiwa vizuri
endapo watapewa ridhaa na wananchi, ikiwa ni pamoja na suala zima la
kupambana na kuongeza fursa za vijana ili kukabiliana na uhaba wa ajira.
Alisema Serikali iliyopita imejitahidi kuongeza huduma za umeme katika
vijiji ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi lakini katika awamu hii CCM
ikipewa ridhaa itahakikisha vijiji vilivyobaki kwa baadhi ya maeneo
vinawekewa umeme. Alisema anawapa akinamama kazi kuhakikisha Dk. Magufuli
na wagombea wa CCM eneo hilo wanashinda kwa asilimia 80 kwani wao ndio
wenye ushawishi mkubwa katika familia. Vivyo hivyo kuwataka madiwani
wanaogombea kuhakikisha mgombea uraisi na wengine wanapata kura za kutosha
ili kushinda uchaguzi.
Kwa upande wake Asumta Mshana aliyekuwa mbunge wa CCM na uchaguzi huu
aligombea na kura hazikutosha alisema anawashangaa wanachama ambao
waligombea ndani ya Chama Cha Mapinduzi na waliposhindwa wakaamua kuondoka
ndani ya chama hicho. Alihoji kwani walipokuwa wakiomba nafasi hizo
hawakutambua kuna kushindwa na kushinda? Aliwafananisha wanaofanya hivyo ni
sawa na akinababa wanaoamua kukimbia familia zao jambo ambalo ni aibu.
"Nawashauri wababi ndani ya chama na kukijenga chama ili kiweze kufanya
vizuri, kama kura hazikutosha safari hii usikimbie chama kwani mlikuwa
hamjui kuna kushinda na kushindwa unapoomba uongozi," alisema.
Naye Mwenyekiti wa CCM, Mkoa Idd Juma Mohamed alimshukuru Bi. Samia kwa
kuamua kuanza kampeni katika mkoa wake na kumuhakikishia watahimiza wapiga
kura kwani Kilimanjaro bado ni ngome ya CCm na watahakikisha wanatwaa
majimbo yote, viti vya udiwani.