Mkurugenzi
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kailima Ramadhan (kushoto),
akimkabidhi Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Benedict Wakulyamba
orodha ya majina 52,078 ya watu waliojiandika katika daftari la kudumu
la wapiga kura kwa mfumo wa BVR zaidi ya mara mbili Dar es Salaam leo,
kwa ajili ya uchunguzi na baadae hatua za kisheria zichukuliwe kwa
wahusika.
Mkurugenzi
wa Idara ya Daftari la mpiga kura, Dk. Sisti Cariah (kushoto),
akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo kuhusu hatua
waliyoifikia kuhusu daftari hilo na shughuli mbalimbali zinazoendelea
kufanywa na NEC kuelekea uchaguzi mkuu.
Mtaalami wa Tehama wa NEC, Fatuma Mkanguzi akiwaelezea wanahabari jinsi mfumo wa Tehama unavyofanyakazi.
Fundi, Francis Skale akiwa kazini.
Mafundi wa NEC wakiendelea na kazi.
Mtaalamu wa mfumo wa ulinzi wa NEC, Adolf Kinyelo akitoa maelekezo ya jinsi ya mfumo huo unavyofanya kazi.
Wanahabari wakichukua taarifa mbalimbali kuhusu NEC inavyofanyakazi zake na hatua waliyofikia kuelekea uchaguzi mkuu.
Picha hii ni baadhi ya watu waliojiandikisha zaidi ya mara mbili katika daftari hilo.
Na Dotto Mwaibale
TUME
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imelikabidhi jeshi la polisi orodha ya
majina ya watu zaidi ya 52,000 ambao wamebainika kujiandikisha zaidi ya
mara moja kwenye daftari la kupigia kura kwa mfumo wa Biometric Voters
Registration (BVR), akiwemo Diwani wa Kata ya Kimara, Pascal Manota
(Chadema).
Idadi
hiyo ilibainishwa Dar es Salaam leo na Mkurugenzi wa NEC, Ramadhan
Kailima wakati wa ziara na waandishi wa habari katika bohari ya
utayarishaji wa vitambulisho vya kupigia kura kwa mfumo wa BVR.
Akizungumza
mara baada ya kukabidhi orodha ya majina hayo kwa Jeshi la Polisi,
Kailima alisema watu hao watachukuliwa hatua kisheria kwani
kujiandikisha zaidi ya mara moja ni kosa kisheria huku akiwatoa hofu
wananchi waliojiandikisha na kutoonekana majina yao.
"Mchakato
wa kutoa majina ni suala ya kisheria kwa sababu ukiangalia kifungu
namba cha sheria ya uchaguzi namba 11 (a) kinasema baada ya kuboresha
daftari tume itaweka wazi majina hayo ili watu waweze kupitia, lakini
kifungu namba 23 cha sheria hiyo hiyo kinasema, iwapo mtu hataliona jina
lake kwenye daftari anapaswa atoe taarifa kwa mkurugenzi wa uchaguzi au
ngazi ya halmashauri ili taarifa zake ziweze kufanyiwa
marekebisho,"alisema
Akizungumzia
namna ya kupiga kura kwa walemavu wasioona, Kailima alisema hadi sasa
wapo kwenye mchakato wa kuleta vifaa vya kupigia kura kwa kundi hilo ili
kuwe na usiri wakati wa upigaji kura na kuepusha watu kupiga kura zaidi
ya mara moja.
"Ijumaa
(leo) mtashuhudia tukifanya maridhiano ya mwisho na kundi hilo,
tumewashirikisha kwenye kikao chetu cha ndani na tukawapa wenyewe kazi
ya kwenda kubuni aina ya karatasi za kupigia kura na tumewapa uhuru
ambapo tutakubaliana nao na tuone mahitaji yao wenyewe kwa wale wanaojua
kusoma maneno yao na wasioweza wapige kura,"alisema.
Kwa
upande wa Msimamizi wa Kitengo cha Kufanya Marekebisho ya 'BVR Kit' na
Kuchakata data, Aguta Obala alisema tuhuma za vitambulisho feki
vilivyokamatwa hivi karibuni si ya tume ya uchaguzi.
"Hizo
taarifa sina uhakika kwa sababu sijaona kama taarifa zinafanana na za
hapa tume, lazima wahakikishe wametoa taarifa za vitambulisho hivyo
kwenye BVR Kit ipi,"alisema.
Kamishna
Msaidizi wa Polisi (ACP), Benedict Wakuryamba baada ya kupokea orodha
hiyo alisema baada watu hao na taarifa zao zitafanyiwa upelelezi na
kufikishwa mahakamani endapo atakutwa na hatia.
Naibu
Katibu Mkuu wa Teknlojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa NEC, Dk.
Sisti Cariah alisema kwa kutumia mfumo wa BVR ni vigumu mtu
kujiandikisha zaidi ya mara moja kwani mfumo huo ni rahisi kumgundua
huku akibainisha kurekebisha kasoro ndogo ndogo.
Manota ajibu tuhuma
Akizungumza
na mwandishi wa gazeti hili kuhusu kutuhumiwa kujiandikisha zaidi ya
mara moja, Manota alisema tuhuma hizo si za kweli na kwamba
alijiandikisha mara moja ambapo jina lake katika kitambulisho hicho
halikuonekana vizuri.
Alisema
kutokana na hali hiyo ilimpasa arudie kujiandikisha upya katika kituo
hicho hicho huku ikiwa muda ni tofauti kutokana na msongamano wa watu
katika mchakato wa uandikishaji.
"Nilipojiandikisha
mara ya kwanza jina langu lilififia kwenye kitambulisho na hapo ndipo
nilipoomba nijiandikishe tena ambapo nilivua koti na kupiga picha,"
alisema na kuongeza kuwa muandikishaji huyo alishindwa kurekebisha data
'edit'.
Manota
alisema baada ya kujiandikisha upya kitambulisho cha awali alikiacha na
kwamba kitambulisho hicho kipo halmashauri ya manispaa hiyo huku
akiamini hiyo ni siasa na kumpigia kampeni.
Rufaa za ubunge
Katika
hatua nyingine, NEC imesema hadi kufikia jana rufaa za wagombea ubunge
na udiwani katika maeneo mbalimbali nchini zilikuwa zimefikia 60.
Pia,
imesema hadi kufikia Agosti 30 ya wiki ijayo rufaa 31 zitakuwa
zimetolewa uamuzi, hivyo tume itakuwa katika nafasi nzuri ya kuzungumzia
hilo.
Akizungumza
na gazeti hili, Mkurugenzi wa NEC, Ramadhan Kailima alisema rufaa za
ubunge zilikuwa 31 na udiwani 29 lakini zinaweza kuongezeka .
Hata
hivyo, alitoa mwito kwa vyama ambavyo vitaona havikuridhika na matokeo
kwa njia moja ama nyingine katika maeneo waliyogombea kuwasilisha rufaa
zao tume hiyo kutokana na kutoridhishwa na wakurugenzi wa uchaguzi
katika maeneo yao.
Alisema
miongoni mwa chama kilichowasilisha rufaa zake tume ni ACT -Wazalendo
ambacho kinalalamikia wagombea wake kutotendewa haki.
(Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com)