Uboreshaji
wa Daftari la kudumu la Wapiga Kura kwa kutumia mfumo wa Biometric
Voters Registration (BVR) ulikamilika tarehe 04/08/2015 katika Mikoa
yote ya Tanzania Bara na Visiwani.
Baada
ya kukamilika kwa zoezi la Uboreshaji Tume imekuwa ikichakata
(processing) taarifa za Wapiga Kura ili kuweza kuandaa Daftari la Awali
la Wapiga Kura, katika maandalizi hayo mifumo imeweza kugundua kasoro
mbali mbali ambazo baadhi zimefanyiwa kazi na zingine zinaendelea
kufanyiwa kazi, kasoro hizo ni pamoja na Wapiga Kura Kujiandikisha zaidi
ya mara moja.
Mfumo
wa BVR unao mfumo mdogo wa “Mini AFIS” unaoweza kubaini Mpiga Kura
anayataka kujiandikisha zaidi ya mara moja katika kituo husika, mfumo
huo ulikuwa umeandaliwa ili kuweza kubaini Wapiga Kura wanaotaka
kujiandikisha zaidi ya mara moja na kuzuia Uandikishaji huo katika BVR
Kit yoyote. Hii ingewekana iwapo Mfumo wa mawasiliano ungekuwa na nguvu
katika vituo vyote na kuweza kuwasiliana na mifumo iliyoko katika kituo
kikuu cha maandalizi ya Daftari(Data Processing Center) kwani katika
kituo hicho imewekwa mifumo ya hali ya juu inayoongoza kimataifa katika
kulinganisha alama za vidole na kubaini waliojiandikisha zaidi ya mara
moja.