Edward Ngoyayi Lowassa (Chadema) - Rais
Freeman Aikaeli Mbowe (Chadema) - Mambo ya Nje
John John Mnyika (Chadema) - Fedha na Uchumi
David Kafulila (NCCR-Mageuzi) - Kazi na Ajira
David Ernest Silinde (Chadema) - Tamisemi
Dk. Emmanuel John Makaidi (NLD) - Viwanda, Biashara na Masoko
James Mbatia (NCCR-Mageuzi) - Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Joseph Selasini (Chadema) - Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu)
Magdalena Hamisi Sakaya (CUF) - Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
Masoud Abdallah Salim (CUF) - Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano)
Mchungaji Peter Simon Msigwa (Chadema) - Maliasili na Utalii
Mhandisi Mohammed Habib Juma Mnyaa (CUF) - Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu
Pauline Phillipo Gekul (Chadema) - Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji)
Prof. Kulikoyela Kanalwanda Kahigi (Chadema) - Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma)
Rajab Mohammed Mbarouk (CUF) - Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge)
Tundu Antipas Lissu (Chadema) - Sheria na Katiba
Wilfred Muganyizi Lwakatare (Chadema) - Ofisi ya Rais (Utawala Bora)
Na Daniel Mbega
UKAWA wameokota almasi kwenye mchanga wa pwani, na kwa kumpata Edward
Lowassa Umoja huo wa Katiba ya Wananchi unaamini utachukua dola ifikapo Oktoba
25 mwaka huu.
Lowassa, waziri mkuu aliyelazimika kujiuzulu kufuatia kashfa ya
kinyonyaji ya kampuni za ufuaji umeme wa dharura za Richmond na Dowans,
ameshawishika kujiunga na umoja huo kupitia Chadema, hali ambayo wachambuzi
wengi wa masuala ya siasa wanasena kuna kila dalili za kuung’oa utawala msonge
wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho huenda baada ya Oktoba itabidi kiunde
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB).Duru za siasa kutoka ndani ya Ukawa zinaeleza kwamba, ilikuwa kazi ngumu
kumshawishi Lowassa kuhamia Ukawa baada ya kuenguliwa na CCM katika
kinyang’anyiro cha urais, lakini kwa sasa kazi itakuwa rahisi zaidi kushinda
uchaguzi wa mwaka huu kutokana na mwanasiasa huyo kuwa na wafuasi wengi nyuma
yake.
Mchakato unaoendelea hivi sasa, kwa mujibu wa vyanzo vya ndani, ni
kuangalia nani kati ya viongozi wa vyama vinavyounda umoja huo atashika nafasi
gani, ingawa tayari maafikiano yanakaribia kufikia tamati.
Taarifa zinasema kwamba, ikiwa Lowassa atagombea urais kupitia Ukawa
akitokea Chadema, basi mgombea mwenza – ambaye ndiye atakayekuwa Makamu wa Rais
– atakuwa Haji Duni kutokea Chama cha Wananchi (CUF) upande wa Zanzibar, ambaye wamemtangaza Agosti 4, 2015 kama mgombea mwenza.
Habari za ndani zinaeleza kwamba chini ya makubaliano ya
Ukawa ikiwa mgombea urais atatoka Chadema, mgombea mwenza akitoka chama kingine
itabidi ahame chama chake ili aingie chama alicho mgombea urais ili kukidhi
matakwa ya kikatiba.
“Tutakaposhinda uchaguzi, kama makamu wa rais atatoka CUF
itabidi kila akitoka katika ofisi ya makamu wa rais, kituo cha kwanza atasimama
Makao Makuu ya CUF kwa ajili ya kupeleka taarifa na kupata baraka za chama
katika masuala muhimu,” chanzo kimoja kilinukuliwa kikisema.
Hata hivyo, katika upangaji wa uongozi, inabainishwa kwamba Dk. Wilbrod
Peter Slaa ndiye aliyepangwa kuwa Waziri Mkuu na kujenga safu imara ya uongozi wa juu
wa taifa, lakini kitendo chake cha kukaa pembeni hivi sasa kimeweka doa kambi hiyo ya Ukawa.
Vyanzo hivyo vinawataja wabunge kadhaa wa vyama hivyo waliomaliza muda
wao kwamba ndio wanaopigiwa chapuo kuongoza wizara mbalimbali, japokuwa wapo
baadhi yao ambao wameanguka katika kura za maoni.
“Mhandisi Mohammed Habib Juma Mnyaa ameshindwa kwenye jimbo lake la
Mkoani huko Pemba, lakini huyu jamaa ndiye anayefaa kuongoza Wizara ya
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ambayo aliiongoza akiwa waziri kivuli.
“Yupo pia Mhandisi aliyebobea, Dk. Emmanuel John Makaidi, ambaye
anastahili kuongoza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa ufanisi mkubwa,” mjumbe
mmoja kutoka CUF.
Taarifa hizo zinasema, Dk. Makaidi, Mwenyekiti wa chama cha NLD
kinachounda Ukawa ambaye alipata kuwa mwenyekiti wa klabu ya soka ya Simba
kabla ya kurithiwa na Juma Salum, anaweza kuteuliwa na rais kutoka kwenye
‘kapu’ badala ya kuingia majimboni kupigana vikumbo, fursa ambayo pia anaweza
kuipata Mhandisi Mnyaa.
Mwaka 2005 alishika nafasi ya saba kati ya wagombea urais
10 waliojitokeza na kupata kura 21,574 sawa na asilimia 0.19, akiwa
nyuma ya Mchungaji Christopher Mtikila wa DP.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, anatajwa kwamba ataongoza Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, wakati Mchungaji Peter Simon
Msigwa ataongoza Wizara ya Maliasili na Utalii.
Waziri wa zamani wa Maliasili, Utalii na Mazingira, Juma Hamad Omar,
ambaye amepitishwa na CUF kugombea katika Jimbo la Wawi kuziba nafasi ya Hamad
Rashid Mohammed bado hajafikiriwa nafasi gani atapatiwa kutokana na uzoefu
wake, ingawa anatajwa kwamba anafaa kuongoza Wizara ya Mazingira, lakini kashfa
ya mkataba ‘haramu’ wa Loliondo inaweza kumtia doa.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, Juma Hamad Omar, ambaye aliongoza wizara
hiyo wakati wa serikali ya awamu ya pili, hatasahaulika kirahisi katika
historia ya uongozi wa wizara hiyo, kwani wakati wa uongozi wake ndipo
ilipotokea kashfa ya uuzwaji wa Pori la Loliondo kwa Mwana wa Mfalme wa Falme
za Kiarabu.
Kashfa hiyo ni kati ya matukio
makubwa yaliyotikisa nchi kwani ilisababisha kuundwa kwa Kamati ya Bunge
iliyoongozwa na Mateo Qaresi na chanzo cha kuondolewa kwa Mkurugenzi wa Idara ya
Wanyamapori wakati huo, Muhidin Ahmad Ndolanga, ambaye alimchapa kibao Qaresi
bungeni pale Karimjee. Omar aliondoka katika wizara hiyo mwaka 1995 baada ya
Rais Mkapa kuingia madarakani.
Ifuatayo ni orodha pendekezwa ya baadhi ya wizara za sasa (japokuwa kuna
uwezekano wa kuzipunguza ikiwa Ukawa wataingia madarakani ili kupunguza
matumizi ya serikali):
Waziri katika Ofisi ya Rais (Utawala Bora): Wilfred Muganyizi Lwakatare,
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, ambaye kwa sasa ameshinda kura za
maoni kugombea tena katika Jimbo la Bukoba Mjini.
Waziri Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma): Profesa
Kulikoyela Kanalwanda Kahigi (Chadema), ambaye anagombea tena katika Jimbo la
Bukombe.
Waziri katika Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu): Joseph Roman
Selesini (Chadema) anatetea nafasi yake katika Jimbo la Rombo.
Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge): Rajab Mohammed
Mbarouk (CUF) ambaye alikuwa waziri kivuli katika Bunge lililopita na anatetea
nafasi yake katika Jimbo la Ole.
Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi): David Ernest Silinde
(Chadema), ambaye licha ya kuwa waziri kivuli katika Bunge lililopita,
alionyesha umakini mkubwa hata wakati wa uwasilishaji wa bajeti kivuli.
Anagombea katika Jimbo la Momba mkoani Songwe.
Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira): Juma Hamad Omar (CUF)
anagombea katika Jimbo la Wawi.
Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano): Masoud Abdallah Salim
(CUF) ambaye anatetea tena nafasi yake katika Jimbo la Mtambile.
Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji): Pauline Philipo
Gekul (Chadema) ndiye aliyekuwa waziri kivuli. Uwezo wake wa kujenga hoja na
kuzitetea ndio umemfanya hata akashinda kura za maoni katika Jimbo la Babati
Mjini mkoani Manyara.
Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango: John Mnyika (Chadema), ambaye safari
hii anagombea katika Jimbo jipya la Kibamba badala ya Ubungo.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi: James Mbatia (NCCR-Mageuzi),
ambaye anagombea tena katika Jimbo la Vunjo, lakini atakumbukwa na wengi jinsi
alivyoipeleka mchaka mchaka serikali Bungeni kuhusu suala la mitaala ya elimu.
Waziri wa Maliasili na Utalii: Mchungaji Peter Msigwa (Chadema).
Anafahamika vyema jinsi alivyokuwa akipambana kufichua uovu katika wizara hiyo
na hoja zake ndizo zilichangia wakurugenzi takriban saba wa wizara hiyo
kutimuliwa.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi: Halima James Mdee
(Chadema). Ni mmoja kati ya wabunge imara ambaye tangu ameingia mwaka 2005,
kwanza kupitia Viti Maalum na baadaye jimboni Kawe, aliweza kufichua uozo wa
serikali katika uuzaji wa ardhi na kusababisha migogoro mingi.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto: Magdalena Sakaya (CUF).
Wizara ya Katiba na Sheria: Tundu Antipas Lisu (Chadema), ndiye
Mwanasheria Mkuu wa Chadema na alikuwa Mnadhimu Mkuu (Chief Whip) wa upinzani.
Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko: Dk. Emmanuel John Makaidi (NLD).
Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu: Mhandisi Mohammed Habib
Juma Mnyaa (CUF).
Wizara ya Kazi na Ajira: David Kafulila (NCCR-Mageuzi).
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia