Ticker

6/recent/ticker-posts

BAADA YA HUDUMA YA MABASI YA DART JIJINI DAR ES SALAAM KUANZA DR.MASSABURI AFURAHIA


HATUA ya kuzinduliwa kwa mabasi yaendayo haraka katika Jiji la Dar es Salaam, kumetibua mpango wa vyama vya upinzani, kumchafua mgombea wa ubunge katika Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Didas Masaburi na chama hicho.
Dk Masaburi ndiye Mwenyekiti wa Kikosi Kazi kilichoundwa na serikali kusimamia mradi huo kukamilika haraka iwezekanavyo ili kuboresha usafirishaji wa abiria katika Jiji la Dar es Salaam na kukuza uchumi, Ubungo ikiwa ni mlengwa mkubwa kutokana na kuwekwa katika awamu ya kwanza ya mradi.
Habari za kuaminika zinasema baadhi ya wagombea kutoka vyama vya upinzani walikusudia kutumia hoja za Mradi wa Mabasi Yaendayo kwa Haraka (DART), ubinafsishwaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) na madai ya kutotumia nafasi ya Umeya wa Jiji la Dar es Salaam katika kuinufaisha Ubungo kama silaha za kumhujumu Dk Massaburi na CCM.
Baada ya Mradi wa DART  kuzinduliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia jana, ukiwa chini ya waendeshaji wazawa, Kampuni ya UDA-RT ambayo inaundwa na wawekezaji wazawa Kampuni ya UDA na Muungano wa Wamiliki wa Daladala, hoja hiyo imepoteza nguvu.
Wakizungumza katika vijiwe maarufu vya upinzani vya Kosovo  na Sweet Corner vilivyopo Manzese jijini Dar es Salaam, wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliahidi kuzitumia hoja hizo ili kumdhoofisha Dk Masaburi wakati kampeni zitakapoanza.
Abbas Mwaimu wa CUF na Zebedayo Ngogo walisema wamejipanga kumuuliza Dk Masaburi maswali kuhusiana na hoja hizo, akisema mradi wa DART na UDA ni miradi hewa na isiyo na manufaa kwa wakazi wa Dar es Salaam, hususani Ubungo.
Kuzinduliwa kwa mabasi ya DART katika awamu ya kwanza ya utoaji wa mafunzo kwa madereva jana, kunawafanya wananchi na wajasiriamali wa Ubungo kilipo kituo kikubwa cha mabasi hayo kufikia  ndoto yao ya kupata ajira hasa kwa vijana na  upatikanaji wa ajira kwa vijana, ukuaji wa biashara kwa mamalishe na makundi mengine ya kijamii kutimia.
Kwa wakati tofauti jana, Waziri Ghasia na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Dadiki, walisema Dk Masaburi akiwa Mwenyekiti wa Kikosi Kazi kilichoundwa ili kusimamia Mradi wa DART kukamilika haraka, amefanya kazi kubwa inayoonesha jinsi Serikali ya Rais Jakaya Kikwete na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli inawajali wananchi wake.
Mbali ya Mradi wa DART, Ubungo pia itanufaika na Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP) ambapo Benki ya Dunia tayari imetoa Sh bilioni 8.76 ili kuboresha mazingira ya Jiji la Dar es Salaam kupitia mpango huo, huku maeneo mbalimbali yakitegemewa kuboreshwa ikiwemo upanuzi na urekebishaji wa madaraja ya Mto Mbokomu ambao ni kero kwa wakazi wa Manzese.
Akizungumza kwenye uzinduzi jana, Dk Massaburi alisema; “Hayawi hayawi yamekuwa. Kinachofanyika leo kinadhihirisha namna serikali ya Rais Kikwete na Waziri Magufuli inavyowajali wananchi wake.
“Kuna watu walihaha ili kuhakikisha kuwa mradi huu wasipewe wazalendo wapewe wageni, lakini Rais Kikwete na Waziri Magufuli walisimama kidete. Waliokuwa wanabeza leo wanatakiwa kuzomewa bila kupepesa macho maana hatimaye mabasi yamefika.
“Mradi huu ni muhimu sana kwani utasaidia kuinua ajira, kipato, kuondoa umasikini kwa kuinua uchumi wa wajasiriamali, maana mahala inakopita barabara, viwanja vitapanda bei, vijana watapata ajira, na mama lishe watauza bidhaa mbalimbali. Lakini pia wageni watapenda kutumia usafiri huu kwa hiyo utalii ndani ya Dar es Salaam utakua,” alisema Dk Masaburi.
Aidha Dk Masaburi alitumia nafasi hiyo kuzitaka mamlaka husika kuwapa umuhimu wa pekee watu wanaoishi katika maeneo ya mradi wanapotoa ajira, huku akisema ni lazima wananchi wa Jimbo la Ubungo wapewe umuhimu wa nafasi za ajira.

Post a Comment

0 Comments