HOTUBA
YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHE. SYLVESTER MHOJA
KASULUMBAYI (MB) KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2012/13 NA
MAKADIRIO YA MATUMIZI YA WIZARA YA MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI KWA MWAKA WA
FEDHA 2013/14
(Inatolewa chini ya Kanuni ya 99 (9), ya Kanuni za
Kudumu za Bunge Toleo la Mwaka 2013)
A: UTANGULIZI
Mheshimiwa
Spika, dira ya Wizara ya
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ni kuhakikisha kuwa raslimali za mifugo na uvuvi
zinaendelezwa na kutunzwa katika mazingira endelevu kwa ajili ya ukuaji wa
uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha dira inalenga kuhamasisha ufugaji wa kisasa na uvuvi endelevu ili
kujenga uchumi endelevu kwa jamii nzima ya wafugaji na wavuvi na taifa kwa
jumla.
Mheshimiwa
Spika, Licha ya ukweli kwamba
wafugaji na wavuvi wana mchango mkubwa katika uchumi wetu, Serikali hii ya CCM
imeshindwa kuwapatia maeneo maalum kwa ajili ya malisho kwa maendeleo ya mifugo
yao. Wafugaji wamekuwa wakihamishwa na au wakifukuzwa kutoka eneo moja la nchi
hadi eneo lingine kama vile hawana haki ya kufanya shughuli za kiuchumi kama
ufugaji katika nchi yao. Ni aibu kwa Serikali kushindwa kuwapatia wafugaji mahitaji
muhimu ambayo yangepelekea ufugaji wao kuwa wa kisasa, kibiashara na endelevu
kama ilivyobainisha katika dira ya Wizara hii.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, haioni sababu ya Serikali kuwapatia
wafugaji maeneo ya kufugia kwa kuwa
wafugaji wangeweza kuingia ubia na mashamba
makubwa ya mifugo ambayo yalikuwa yanamilikiwa na Ranchi za Taifa, lakini kutokana
na ubinafsi na ufisadi uliofichwa kwenye kivuli cha cha sera ya ubinafsishaji, Serikali ya CCM imesimamia zoezi la viongozi wa serikali na Chama cha Mapinduzi
wakigawiana ranchi hizo na kuwaacha wafugaji wakifukuzwa ovyo na kupewa jina la
wachungaji.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa
wavuvi hali ni hiyo hiyo, kwani mapato
mengi ya Serikali yanayokusanywa kutoka
katika sekta ya uvuvi yanatokana na wavuvi wadogo ambao mara zote wao ndio
waathirika wa mfumo kandamizi wa Serikali.
Zana za uvuvi zinapokamatwa, wao ndio wanapata hasara, lakini wauzaji wa
zana hizo za uvuvi wala hawaulizwi na
wala hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi yao.
Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa inayozikabili sekta hizi za
ufugaji na uvuvi ni kwamba sekta zote
mbili hazina bima dhidi ya majanga
ambayo yanaweza kutokea. Katika
mazingira kama haya, dhana ya kuwa sekta za kisasa, kibiashara na endelevu
inakuwa ngumu sana.
Mheshimiwa Spika, katika
hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa mwaka wa fedha
2012/2013 liainisha mapungufu makubwa katika ya kiutendaji na kiuwajibikaji kwa
wizara hii na kuitaka Serikali kufanya mambo yafuatayo:
1.
Kuwajibika
kwa uzembe wa kuitelekeza meli ya uvuvi ya Tawariq iliyokamatwa ikifanya uvuvi
haramu katika ukanda wa bahari ya hindi hadi meli hiyo kuharibika kabisa na
kuanza kuzama bila faida yoyote?
2.
Kuchukua
hatua dhidi ya mwekazaji wa Kagera Sugar kwa kushindwa kuendeleza shamba la
ukubwa wa hekta 45,000 (sawa na ekari 112,500) kinyume na mkataba.
3.
Kueleza
sababu za kuwapa mashamba makubwa wawekezaji wa kigeni na kuwanyanyapaa
wafugaji wa asili kinyume cha sheria.
4.
Kutatua
migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji ambayo mara kadhaa imesababisha
uvunjifu wa amani na umwagaji damu miongoni mwa wananchi.
5.
Kujenga
viwanda vya kusindika nyama katika mikoa ya wafugaji ili kuongeza thamani ya
bidhaa ya nyama na hivyo kukuza uchumi.
6.
Kuweka
wazi kiasi cha fedha kinachopatika kama mrahaba kutokana na uvuvi katika bahari
kuu, pamoja na fedha za leseni kwa meli zinazofanya uvuvi katika ukanda wa
bahari kuu.
B. SEKTA
YA MIFUGO
Mheshimiwa
Spika, Sekta ya Mifugo ina
nafasi kubwa katika kujenga uchumi imara wa Taifa, kuongeza kipato kwa
Watanzania wanaotegemea mifugo, na kutoa fursa za ajira sanjari na kuhifadhi
rasilimali za Taifa. Sera ya mifugo inaeleza nia ya Serikali na wadau wengine
katika kukabiliana na changamoto zinazokabili Sekta ya Mifugo. Lengo kubwa ni
kujenga mazingira mazuri yatakayotoa fursa za kuongeza kipato na ajira kwa
wafugaji wadogo, kufuga kibiashara na kuongeza ajira. Ili kufikia haya Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutekeleza, malengo makuu matatu ya kisera
kama ifuatavyo:-
1.
Kuendeleza
Sekta ya Mifugo itakayokuwa na mwelekeo wa kibiashara, yenye ufanisi na
itakayohimili ushindani wa kimataifa;
2.
Kuibua
mifumo bora ya uzalishaji itakayoongeza tija miongoni mwa wafugaji wadogo na wa
asili.
3.
Kuhifadhi
rasilimali za mifugo na kuunda sera na taasisi zitakazosimamia maendeleo na
matumizi endelevu ya rasilimali hizo n.k.
Mheshimiwa
Spika, Sera hiyo ya mifugo
imeweka wazi azma ya Serikali ya kuboresha sekta hii ya mifugo, lakini
kutokuwepo na mkakati madhubuti wa kufanikisha yale yote yanayohitajika
kufanyika na sera hii ya Mifugo ya mwaka 2006, kunaendeleza matatizo katika
sekta hii mpaka sasa.
Mheshimiwa
Spika, Sekta ya Mifugo hapa
nchini ina nafasi kubwa katika ujenzi wa uchumi wa Taifa. Kwanza kwa
kuthamanisha kiwango cha nyama kinachotumika kila siku hapa nchini ikiwa kiwango hicho kingekuwa kinaagizwa toka nje ya
nchi. Pili ni kuongeza kipato kwa Watanzania wanaotegemea mifugo, na kutoa
fursa za ajira sanjari na kuhifadhi rasilimali za Taifa.
Mheshimiwa
Spika, Mashamba makubwa ya
mifugo yana uwezo wa kuongeza viwango vya uzalishaji na uuzaji wa mifugo na
mazao yake nje ya nchi, ajira na kuboresha maisha ya wafanyakazi wake. Mkakati
umetumika wa kugawa mashamba makubwa ya Kampuni ya Ranchi za Taifa KARATA
(NARCO) na yale yaliyokuwa chini ya Kampuni ya Ng’ombe wa Maziwa (DAFCO) kuwa
mashamba yenye ukubwa wa kati kwa ajili ya ufugaji wa kibiashara unaolenga
kutekeleza dhana hii. Mkakati huu umeongeza upeo wa umilikaji mashamba na pia
kuwawezesha Watanzania kuingia katika ufugaji wa kibiashara. Maeneo ya ranchi
za KARATA (NARCO) yaliyobaki yataendelea kutumika kama ranchi za mfano na
maeneo yasiyo na magonjwa ya mifugo kwa ajili ya soko la nje ya nchi[1].
Mheshimiwa Spika, ilani ya CCM ya mwaka 2005-2010 aya ya 32 inasema
kwamba, “Pamoja na kwamba
Tanzania ina mifugo mingi sana; mchango wa mifugo kwenye uchumi wa Taifa ni
mdogo. Kwa lengo la kuendeleza Sekta ya Mifugo ili ichangie zaidi ukuaji wa
uchumi wa Taifa na kuwaongezea kipato wafugaji, Serikali za CCM zitaendeleza
kwa msisitizo zaidi lengo la kuzingatia zaidi ubora kuliko wingi pekee katika
ufugaji. Ili kufikia lengo hilo, hatua zifuatazo zitachukuliwa katika kipindi
cha 2005-2010:-
(a)
Kujenga mazingira ya kuvutia uwekezaji
katika viwanda vya kuongezea thamani mazao ya mifugo kama vile ukataji nyama,
usindikaji wa maziwa, utengenezaji wa bidhaa za ngozi n.k.”
Mheshimiwa
Spika, na katika Ilani ya
CCM ya mwaka 2010-2015 aya ya 38 inasema
kwamba; “Katika kipindi cha Ilani hii ya miaka 2010-2015, Chama Cha Mapinduzi
kitazielekeza Serikali kuiendeleza sekta ya mifugo kwa ari zaidi, nguvu zaidi
na kasi zaidi ili kuiwezesha kutoa mchango mkubwa kwenye pato la Taifa kwa
kuchukua hatua zifuatazo:-
(a)
Serikali iandae programu kabambe ya kuendeleza sekta ya mifugo na ufugaji.
Programu hiyo ijumuishe pamoja na mambo mengine masuala ya uendelezaji wa
maeneo ya malisho, kuchimba na kujenga malambo, mabwawa, majosho na huduma za
ugani ili hatimaye wafugaji waondokane na ufugaji wa kuhamahama.
(b)
Benki ya Kilimo itakayoanzishwa iwe pia Benki ya Mifugo ili iweze pia kutoa
mikopo kwa wasomi wenye nia ya kufuga na kuwawezesha kuingia kwa wingi katika
ufugaji wa kisasa.
(c)
Kuelimisha wafugaji uwiano kati ya idadi ya mifugo na eneo.”
Mheshimiwa
Spika, katika kuonyesha
kuwa CCM yale wanayoandika sio wanayosimamia katika kuinua sekta ya ufugaji hasa wa asilia ambao unachangia zaidi ya asilimia
85 ya ufugaji wote, Kambi Rasmi ya Upinzani, inauliza kwa mkakati huo wa CCM
dhidi ya wafugaji na Ufugaji ni kwa vipi ufugaji unaweza kuwa endelevu na wa
kisasa wakati wafugaji wanaporwa maeneo ya kulishia mifugo yao, hawapewi maeneo
ya malisho, hawapati huduma za ugani, hawapati mikopo na hawana soko la uhakika
wa bidhaa zinazotokana na mifugo. Kambi Rasmi ya Upinzani, inauliza kwa makati
huo wa CCM dhidi ya wafugaji na ufugaji ni kwa vipi ufugaji unaweza kuwa
endelevu na wa kisasa wakati wafugaji wanaporwa maeneo ya kulishia mifugo yao?.
Hawapewi maeneo ya malisho, hawapati huduma za ugani, hawapati mikopo, hawana
soko la uhakika. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa kauli juu ya
ni wapi wafugaji wa asili watafugia mifugo yao ili kuwa endelevu nay a kisasa?
jumla ya
wafugaji wakulima wa vijiji vinne vya
Makuyuni, Loikisale, Naiti na Mswakini
katika Wilaya ya Monduli wanatishiwa kuhamishwa kutokana na mkakati
mahususi ulioasisiwa na Mheshimiwa Waziri Kagasheki wa kutangaza maeneo hayo
kuwa ni Wildlife Management Area (WMA). Uhakika ni kwamba WMA hiyo ni hewa
haipo na ukweli ni kwamba eneo hilo kinapewa kikundi kinachoitwa ELEWANA AFRIKA.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali kuwaeleza Wafugaji hao, ni wapi wanakwenda na mifugo
yao? Aidha, kwa kuwa utaratibu wa kuanzisha WMA huwa inaanzishwa kwa kupata
ridhaa za wanavijiji ambao kwa hiari yao wanatoa maeneo ya vijiji vyao kuwa WMA
na ndipo kazi ya Waziri husika inafuata ya kutoa idhini ya uanzishwaji wa hiyo
WMA. Kwa kuwa huo ndio utaratibu wa
kuanzisha WMA, Je, ni kwanini vijiji hivyo havikupewa fursa hiyo?
Mheshimiwa Spika,
Mgogoro wa ardhi katika eneo la Loliondo ni taswira nyingine ya jinsi ambavyo
Serikali ya CCM imekiuka haki za wafugaji wa Kimaasai kwa manufaa ya wawekezaji
wa kigeni katika sekta ya uwindaji wa kitalii.
Mheshimiwa
Spika, mgogoro wa Loliondo
bado haujapatiwa ufumbuzi na sasa umeanzishwa mgogoro mwingine Wilaya ya
Monduli. Hii ni kwa makusudi kuhakikisha wafugaji wa asili wanakwisha kabisa?
Mheshimiwa
Spika, hapo kabla ya
uhuru Serikali ilitenga eneo la zaidi ya
hekta 18,000 sawa na ekari 45,000 wilayani Maswa lililojulikana kama SHISHIYU Holding ground kwa ajili ya
kunenepesha mifugo kabla ya kusafirishwa kwenye kiwanda cha Nyama cha
Tanganyika Packers, ambacho kimekufa, cha ajabu ni kwamba katika eneo hilo bado
hadi sasa wafanyakazi wa Idara ya mifugo wapo pale lakini mifugo hainenepeshwi.
Je, hii si hujuma kwa sekta ya mifugo na wafugaji hasa wa wilaya ya Maswa?
Mheshimiwa
Spika, si hilo tu bali
pale Ipala wilaya ya Nzega Mkoa wa Tabora kuna kituo cha treni kilichokuwa
kikitumika kupakia ng’ombe kwenda Dar es Salaam. Eneo hilo lilikuwa limetengwa
rasmi kwa ajili ya mifugo na kuna miundombinu ya kupakia mifugo kwenye treni,
jambo la ajabu ni kwamba serikali imeligeuza eneo lile kuwa hifadhi ya misitu.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwa wafugaji wanaoishi eneo hilo
waachiwe eneo litumike kwa malisho na miundombinu iliyopo.
Mheshimiwa
Spika, aidha, kitendo
kinachofanywa na Wakuu Wilaya na Wakurugenzi wa Halimashauri kuwahamisha
wafugaji kwa nguvu katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kuwalipisha
mamilioni ya fedha wafugaji hao (Mfano mfugaji mmoja wa mikumi alitozwa faini
ya shilingi milioni 42.78 kwa kukamatwa ng’ombe wake, mfugaji wa chunya million
19 n.k) nao ni ushahidi wa dhahiri kwamba Serikali hii ya CCM haina dhamira ya
dhati katika kuhakikisha wafugaji na ufugaji unakuwa na tija katika nchi yetu.
Mheshimiwa
Spika, wafugaji wa asili
ya kisukuma,kimasai,wairaq na wabarbaig katika wilaya za Kilombero, Ulanga,
Kilosa, Mbarali, Chunya, Kilindi, Handeni,Mpanda, Rufiji n.k wamepata matatizo makubwa sana na wengine
wameuawa na vyombo vya dola, kosa lao kubwa ni kuwa na mifugo mingi
iliyosababisha wahame toka mikoa ya kanda ya ziwa kwa sababu za malisho. Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge, je kosa la ndugu zetu hao
ni kuwa na utajiri wa mifugo mingi au nini hadi wanadharauliwa na kunyanyaswa
na kufanywa kuwa watanzania wa daraja la nne katika nchi yao?
Mheshimiwa
Spika, kutokana na ukweli kwamba Wizara imeshindwa
kuwatetea na kuwalinda wafugaji wa asili, hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani
inaitaka Serikali iwaeleze wafugaji ni wizara gani itakayosikiliza na kutatua
matatizo yao?
Mheshimiwa
Spika, kama ambavyo imekuwa
ikitokea katika maeneo ya Ranchi zilizokuwa za mkoa wa Kagera, Rukwa, Morogoro,
Tanga, Pwani watu waliopewa 4000 ha au ekari 10,000 za maeneo ya Ranchi za
Taifa kama wawekezaji, watu hao wameshindwa kuziendeleza ranchi hizo kwa vile wengine
hawana hata mifugo ya kuweka katika maeneo hayo. Kukosa mifugo ya kuendeleza
eneo hilo kwa makusudi watu hao huona kuwa mbadala unaobakia ni kupangisha
maeneo hayo kwa wawekezaji kutoka nchi jirani.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inaona lingekuwa ni jambo la busara kama ushirika wa wafugaji au
mwekezaji mmoja mmoja kupewa ekari 1000 ikiwa eneo lote la ekari 10,000 lingegawanywa ili kurahisisha
uwekezaji wake na kufanya kuwa endelelevu. Kwa eneo dogo uwezekano wa kupata
mkopo toshelezo kwa uwekezaji toka benki zetu na asasi zingine za fedha ni
rahisi kwani hata investiments risks inakuwa ni ndogo na inakuwa imesambaa kwa
wawekezaji wengi.
Mheshimiwa
Spika, wakati Waziri
akijibu swali Na. 26 kuhusu maeneo ya Ranchi za Mkoa wa Kagera, “Je,
kwa nini Serikali isiyarudishe maeneo hayo kwani waliopewa wanayakodisha kwa
wafugaji toka nchi jirani? Je, ni
Watanzania gani kwa majina waliogawiwa maeneo kwenye ranchi hizo? Mheshimiwa
Spika, orodha ya majina ya Wawekezaji Watanzania waliogawiwa maeneo hayo ya
ranchi ipo, nitaomba kukutana na Mheshimiwa Mbunge baada ya hapa ili nimkabidhi
orodha hiyo”.
Mheshimiwa Spika, hadi sasa hivi majina hayo ya wamiliki, Waziri
ameshindwa kuitoa kama alivyoahidi ndani ya Bunge, hoja ni kama kweli wamiliki
ni watanzania ni kwanini wanashindwa kuweka majina hadharani? Hivyo basi, Kambi
Rasmi ya Upinzani inamtaka Waziri kutoa kwa wabunge majina hayo ya wamiliki na
uraia wao hadharani.
Mheshimiwa
Spika, ili kuiwezesha sekta
ya mifugo kutoa mchango stahiki kwa Taifa hili ni lazima uboreshaji katika
sekta ya mifugo wetu ufanyike kwani wanachokosa wafugaji wetu ni Ardhi na elimu
ya ufugaji yenye mafanikio kutokana na kutumia mbinu za zamani za kuzalisha
mifugo. Changamoto kubwa katika sekta hii ni kukosekana kwa mbinu za kisasa,
vifaa na madawa ya uhakika kuhudumia wanyama. Aidha, mifugo mingi inatunzwa
kienyeji na matokeo yake kukosa soko la kimataifa kama zilivyo nchi nyingine.
Kama elimu ya kutosha itatolewa na kuruhusu wawekezaji wa ndani katika sekta ya
mifugo changamoto hizo zitapungua kwa kiasi kikubwa na hivyo kutoa nafasi ya
ongezeko la bidhaa zitokanazo na mifugo.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inasema wawekezaji wa ndani, kwa maana kwamba wafugaji wa asili wao
mtaji wao mkubwa ni mifugo na NARCO wao mtaji wao ni utaalam na miundombinu
iliyopo tayari. Hivyo basi, ni rahisi wa ubia huo kati ya wafugaji wa asili na
NARCO kuleta tija zaidi kuliko mwekezaji toka nje.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na
kuongezeka kwa idadi ya watu, kipato na ukuaji wa miji kwa nchi zinazoendelea
Duniani, Tanzania ikiwa ni mojawapo, mahitaji ya bidhaa za mifugo nayo yamekuwa
yakiongezeka pia. Takwimu zinaonyesha kuwa
Tanzania pekee itaongeza mahitaji mara nne kwa mwaka 2030. Hivyo ni jukumu
la Serikali sasa kulieleza Bunge hili ni kwa vipi Wizara imejipanga kukabiliana
na changamoto ya ongezeko hilo la mahitaji ya nyama kwa muda huo?
Mheshimiwa
Spika, hivi sasa ni 2% tu
ya mifugo yote inayozalishwa na kufugwa kibiashara, hivi sasa Tanzania ina machinjio ya kisasa manne (4) ambayo
hayatoshelezi kwani mahitaji ya nyama safi na salama yanaongezeka kila siku. Aidha, inaonyesha kuwa chini ya 1% ya nyama yote
iliyosindikwa ndiyo inazalishwa hapa nchini na sehemu yote iliyobaki inaagizwa
na kuingizwa nchini kutoka Kenya. Vile vile taarifa hiyo inaonyeshwa kuwa zaidi
ya tani 700 ya nyama safi inaaagizwa toka nje ya nchi kila mwaka wakati
mahitaji ya nyama ndani ya nchi na Kanda yetu ya ushirikiano yanazidi
kuongezeka[2].
Mheshimiwa
Spika, Tanzania ni nchi
ya pili nyuma ya Ethiopia kwa kuwa na mifugo wengi katika Bara la Afrika, sasa
kwa hali ya kawaida tu inakuwaje nchi yetu inaagiza nyama kutoka nje ya nchi?
Mheshimiwa
Spika, Tanzania ina
rasilimali kubwa ya maliasili ikiwemo ardhi, malisho na idadi kubwa ya mifugo.
Kati ya jumla ya hekta milioni 94 za rasilimali ya ardhi, hekta milioni 60 ni
nyanda za malisho zinazofaa kwa ufugaji. Kwa sasa kuna ng’ombe milioni 21.3,
mbuzi milioni 15.2 na kondoo milioni 6.4.
Mifugo wengine ni pamoja na nguruwe milioni 1.9, kuku wa asili milioni 58[3].
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa taarifa
ya utekelezaji wa mpango na bajeti ya mwaka 2012/2013 na makadirio ya mapato na
matumizi kwa mwaka 2013/2014 kiambatanisho Na.3 kinaonyesha kuwa kwa mikoa 21
wilaya 69 na vijiji vilivypimwa 479 eneo la malisho ambalo linasadikiwa kuwa
limetengwa kwa ajili ya wafugaji kuwa ni hekta milioni 1.28. Hii ni sawa na
asilimia 2.13 ya hekta million 60 za nyanda za malisho katika nchi hii.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inamtaka Mhe Waziri awaeleze wafugaji kwa ng’ombe milioni 21.3 na
mbuzi na kondoo milioni 21.5 wanatakiwa wachungwe kwenye eneo la ukubwa gani?
Mheshimiwa
Spika, uzalishaji wa
mifugo umegawanyika katika mifumo mikuu miwili ambayo ni ufugaji huria na
ufugaji shadidi. Mfumo wa ufugaji shadidi japo sio mkubwa nchini, unatiliwa
mkazo zaidi katika kuendeleza ufugaji na uwekezaji kwani unachangia zaidi
kwenye uchumi wa soko.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande mwingine, mfumo wa ufugaji huria
ambao hufanywa na wakulima-wachungaji na wachungaji -wahamaji, ni mfumo
unaotegemea upatikanaji wa malisho na maji kwa msimu na matokeo yake
husababisha wafugaji kuhamahama. Mfumo huu unakabiliwa na matatizo ya utunzaji
duni wa mifugo, matumizi duni ya teknolojia za kisasa, kuhodhi mifugo wengi
zaidi ya uwezo wa ardhi na ukosefu wa mazingira mazuri ya masoko.
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa
tafiti uliofanywa na asasi ya kiraia ya Tanzania Pastoralists, Hunters and Gatherers
Organization- (TAPHGO)
kuhusu mfumo wa biashara ya mifugo Tanzania inaonyesha kwamba sekta ya ufugaji
Tanzania inachangia asilimia 18 ya pato la Taifa, uzalishaji wa nyama kwa mwaka unakadiriwa
kuwa ni tani 259,800, kwa mifugo inayofugwa kwa ajili ya nyama pekee huchangia
tani 181,800.
Mheshimiwa
Spika, aidha mchango wa
wafugaji ambao pia ni wakulima huchangia asilimia 98 ya uhitaji wote wa nyama
hapa nchini, huku asilimia 2 hutoka kwenye ranchi za taifa. Wakati mbuzi na
kondoo huchangia tani 75,800. Thamani ya nyama inayozalishwa inakadiriwa kuwa ni shilingi bilioni 727.44,
kati ya hizo shilingi bilioni 537.94 zinachangiwa na nyama ya ng’ombe na
zilizobaki shilingi bilioni 189.5 ni kwa mbuzi na kondoo.
Mheshimiwa
Spika, katika hotuba ya
Rais wakati wa kufungua mkutano wa
uwekezaji kwa shabaha ya kuibua maendeleo ya Mkoa wa Mara kwa kutumia
rasilimali na utajiri uliopo mkoani Mara “Lazima
tuanze kutekeleza misingi ya ufugaji wa kisasa na tujipange vizuri kwa
uwekezaji kwenye sekta hii. Naomba tutenge maeneo maalum ya ufugaji wa kisasa.
Kwa mfano, tukigawa maeneo ya ukubwa wa hekta 2,000 kila moja na tukawagawia
watu kwa ajili ya kufuga kisasa. Watakaopewa maeneo hayo wahimizwe na kusaidiwa
wayaendeleze kwa malisho na huduma muhimu za maji, majosho pamoja na za
matibabu kwa mifugo. Maeneo hayo yakatumiwa kunenepesha ng’ombe wa nyama
tunawezesha kuwepo kiwanda cha nyama kitakachonunua toka kwao mifugo ya
kuchinja. Kiwanda hicho kitatengeneza soko la uhakika kwa wafugaji”.
Mheshimiwa
Spika, kauli hiyo ya Mhe
Rais imekuja muda ambao tayari maeneo mengi mazuri yaliyokuwa yanamilikiwa na
Serikali tayari yamekwishachukuliwa, na kama utaratibu ambao tumejaribu
kuutolea maelezo kwa kuangalia Ranchi za Mkoa wa Kagera jinsi gani migogoro
iliyopo haimaliziki kutokana na ukweli kwamba wahusika wakuu katika migogoro
hiyo ni watendaji wa Serikali.
Mheshimiwa
Spika, Changamoto kubwa
inayoikabili tasnia ya mifugo ni namna ya kufikia viwango vya ubora wa mifugo
na mazao yake vitakavyokidhi mahitaji ya soko la kikanda na kimataifa.
Mheshimiwa
Spika, katika kuonyesha
kuwa watendaji wanashindwa kutenganisha kati ya machinjio ya kisasa na viwanda
vya kusindika ni pale, Waziri alipokuwa anajibu swali namba 27 kwa mujibu wa
Hansard, “Je, hivi sasa kuna viwanda vingapi vya nyama na vinasindika kiasi gani
cha nyama?” Jibu la Waziri lilikuwa “Mheshimiwa Spika, Tanzania
inahitaji viwanda ama machinjio makubwa takribani 16 yenye uwezo wa kuzalisha
nyama tani 133 kwa siku kwa kila kiwanda au kila machinjio”
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inasisitiza tena ni kwa njia zipi utekelezaji wa Ilani unaweza
kufikiwa kama tafsiri ya kiwanda cha kusindika nyama na machinjio inaonekana
kuwa ni kitu kimoja?
Mheshimiwa
Spika, kwa hali ya kawaida
ng’ombe wa asili hutoa maziwa 0.5ltr kwa siku wakati yule wa kisasa anatoa kati
ya lita 7-30ltrs kwa siku kutegemea na matunzo na elimu ya ufugaji aliyonayo
mfugaji. Hivyo basi ili mfugaji wa
ng’ombe za asili aweze kupata lita 30 za maziwa kwa siku atahitaji kuwa na
ng’ombe 15. Mbali na mambo hayo yote ambayo yataenda na uwiano huo lakini jambo
la muhimu kwa mfugaji wa asili ni kwamba madawa yanayohitajika kwa chanzo, kuosha na kutibu magonjwa ni zile
zile kwa ng’ombe wote wa asili na wa kisasa.
C. HUDUMA
ZA UGANI
Mheshimiwa
Spika, ili sekta hii ya
mifugo iweze kuleta tija inayokusudiwa huduma ya ugani ni muhimu sana, lakini
kwa mtindo wa utendaji kazi kwa watoa huduma hiyo ulivyo ni dhahiri tija
inayotegemewa ni vigumu kupatikana.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na watoa
huduma kutokuwa na idadi maalum ya wafugaji wanaowahudumia, eneo maalum na
hivyo kuweza kuwajibika kwa matokea yatakayopatikana katika eneo husika ni
tatizo kubwa sana.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inaona itakuwa ni vyema kama kila afisa ugani atakuwa na orodha kamili
ya wafugaji anaofanya nao kazi katika eneo maalum, kwani utaratibu huo
utarahisisha upatikanaji wa kumbukumbu sahihi na pia kuweza kupima utendaji wa
afisa huyo.
Kwa mfano kwa maafisa ugani wanaofanyakazi mkoa wa
Kagera ambao ni watumishi wa Serikali
(Ndg. Patrick, Kashankoro, Kanyambo na Mutabazi), hawa wote wanamiliki vitalu
vya Ranchi. Hoja ni je utaratibu wa watendaji wa Serikali kujimilikisha mali za
wananchi unaendelea hata kwenye ngazi ya chini? Na mgongano wa maslahi katika
suala hili unashughulikiwa vipi?
D. SEKTA YA NGOZI
Mheshimiwa
Spika, wakati waziri kivuli wa fedha akiwasilisha maoni ya
Kambi ya Upinzani kwenye muswada wa fedha, tarehe 16.08.2012 alisema yafuatayo “Mheshimiwa Spika, katika kifungu cha 12 cha muswada, serikali inatoa pendekezo la kufanyia
marekebisho sheria ya kodi ya mauzo ya nje ya nchi sura 196 kwa kuweka jedwali
jipya ambalo linaongeza viwango vya tozo kwenye ngozi ghafi inayosafirishwa
kwenda nje ya nchi. Kama serikali ina mpango madhubuti wa kuendeleza sekta ya
viwanda nchini na kuleta tija kiuchumi ni dhahiri kuwa inatakiwa kusitisha
uamuzi huu.
Mheshimiwa Spika, kwenye
hotuba yetu ya bajeti tulipendekeza kuwa serikali izuie kabisa ngozi ghafi
kusafirishwa nje ya nchi na badala yake ijikite kutafuta uwezekano wa kuitumia
ngozi hiyo hapa nchini na kuanzisha viwanda vya kutengeneza bidhaa zitokanazo
na ngozi hiyo. Hata Kamati ya fedha na uchumi ilikuwa na mapendekezo hayahaya.
Hii ni kutokana na manufaa makubwa ya kiuchumi wanayopata wenzetu hasa nchi ya
Ethiopia.
Mheshimiwa Spika,
hata katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki wenzetu wa Uganda na Rwanda nao
wamezuia ngozi ghafi kuuzwa nje ya nchi. Mapendekezo haya ya serikali yakibaki
kama yalivyo hayataifanya serikali kupata mapato yanayostahili kwa sababu
wafanyabiashara wengi wanatoa takwimu zisizo sahihi kuhusu mauzo halisi
watakayokuwa wanauza nje ya nchi (under invoicing).
Mapato
ambayo serikali inahofia kuyapoteza kwa kupiga marufuku uuzaji wa ngozi ghafi
nje ya nchi yatapatikana tena kwa kiasi kikubwa kutokana na ajira
zitakazopatikana katika viwanda vya kusindika ngozi, kodi ya mapato kama vile
PAYE n.k. Ni wakati muafaka sasa tuchukue hatua hii kwani hata nchi ya
Pakistani ambao ndio wanunuzi wa ngozi yetu wamepiga marufuku kabisa uuzaji wa
ngozi ghafi nje ya nchi yao”.
E. SEKTA
YA MAZIWA
Mheshimiwa
Spika, Taarifa ya uwezo wa
viwanda na hali halisi ilivyo sasa hivi Inayonyesha kuwa hadi sasa hivi kuna
viwanda 35 vyenye uwezo wa kusindika zaidi ya lita 1000 kwa siku kwa kila
kimoja. Kati ya hivyo ni viwanda 28 tu ambavyo vinazalisha hadi sasa na vingine
7 ama vimefungwa au kusimamisha uzalishaji. Kuna baadhi ya viwanda vinatumia
hadi zaidi ya 80% ya uwezo wake na vingine chini ya 16%. Kwa vile kuna viwanda
visivyozalisha kabisa, wastani wa matumizi ya uwezo wa kusindika ni 12% tu.
Mheshimiwa
Spika, Uwezo wa jumla wa
viwanda vyote ni kusindika, lita 428,500 kwa siku lakini hali halisi ni
kusindika lita 52,330 kwa siku. Hali hii inaonyesha kuwa juhudi kubwa
zinahitajika ili kuwezesha sekta ya viwanda vya maziwa kuwa na uwezo wa
ushindani na kutoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa taifa.
F.
MATATIZO YANAYOATHIRI USINDIKAJI WA MAZIWA
Mheshimiwa
Spika, Matatizo
yanayovikabili viwanda vya maziwa ni mengi na yanahitaji uchunguzi wa kina
katika kila kiwanda ili kutoa ushauri kwa kila kiwanda husika, lakini matatizo
yaliyotajwa na viwanda vyote ni kama yafuatayo:
1.
Ukosefu
wa maziwa ya kutosha.
Mheshimiwa
Spika, Ingawa Tanzania inakadiriwa
kuzalisha lita 1,400 milioni za maziwa kila mwaka kiasi cha maziwa
yanayopatikana kwa ajili ya kusindika ni kidogo sana. Hali hii inatokana na
maziwa mengi kuzalishwa na wafugaji wa jadi ambayo kiasi kikubwa kinatumika na
wafugaji wenyewe, uzalishaji ni wa msimu na ukusanyaji ni mgumu. Wafugaji hawa
ndio huzalisha 70% ya maziwa yote nchini.
Upungufu wa maziwa ya kusindika ambao huwa zaidi
wakati wa kiangazi unachangiwa na sababu nyingi ambazo ni:
a.
Gharama
kubwa na ugumu wa kukusanya maziwa ya wafugaji
waliosambaa maeneo
ya mbali
b.
Ushindani
na wachuuzi wadogo wadogo.
c.
Faida
ndogo kutokana na matumizi kidogo ya uwezo wa viwanda.
d.
Uzalishaji
wa msimu ambapo maziwa mengi hupatikana msimu wa mvua na kidogo sana wakati wa
kiangazi na hivyo kushindwa kutosheleza[4]
Mheshimiwa
Spika, katika kuhakikisha
kuwa viwanda vya maziwa vilivyopo vinapata maziwa ya kutosha, Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali kuhakikisha kwamba
maziwa yanayozalishwa na wafugaji wadogo au wa asili yanauzwa kwenye vituo
maalum vya kukusanyia maziwa, na pia maziwa yasiuzwe kwa wanunuzi bila ya
kuyasindika. Kufanya hivyo kutaondoa kwanza matatizo ambayo yanayoweza kutokana
na magonjwa ya kuambukizwa kati ya mifugo na binadamu (zoonotic deseases).
Mheshimiwa
Spika, pia liwe ni jukumu
la Halmashauri kulinda soko la maziwa yaliyosindikwa, na kwa njia hiyo wafugaji
wadogo na wale wa asili maziwa yao yatakuwa na uhakika wa soko badala ya sasa
ambapo wakati wa msimu wa mvua maziwa yanakosa soko na hivyo kumwagwa.
Mheshimiwa
Spika, kwa kuwa maziwa kuuzwa moja kwa moja na
wafugaji wadogo na wakubwa ni upotevu wa mapato, hivyo basi Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kuwa, liwe ni jukumu la Halmashauri kutunga kanuni ndogo za kuhakikisha viwanda
vya maziwa vinalindwa kwa kupata maziwa muda wote ili kiwanda kiweze kulipa
kodi kwa halmashauri.
2. Matatizo ya kimfumo na sera
Mheshimiwa
Spika, mbali ya matatizo
hayo pia kuna matatizo ya kimfumo na sera. Katika kundi hili kuna
matatizo kama urasimu katika vyombo vya kudhibiti ubora kama TBS, kuwa na
vyombo vingi vya uthibiti, wadau kutoshirikishwa katika maandalizi ya sera,
migogoro kati ya wafugaji na wasindikaji na vyama vya wadau visivyo imara.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali kuwepo uwajibikaji kwenye vyombo vya udhibiti na
vyombo hivi madhumni yake, yawe ni kuwezesha na siyo kukwamisha. Inapendekezwa
kuwa shughuli zote za udhibiti wa sekta ya maziwa zifanywe na Bodi ya Maziwa
tofauti na sasa ambapo vyombo vingi hufanya hivyo. Aidha, Bodi ya Maziwa
iliyoanzishwa kisheria iwezeshwe kufunya shughuli zake kwa kupewa rasilimali
zinazotakiwa tofauti na sasa ambapo Bodi ipo kwa jina tu.
Mheshimiwa
Spika, aidha, wadau washirikishwe katika
utayarishaji wa sera zinazohusu sekta ya maziwa, kwani sasa wanaohusishwa ni
wale wenye viwanda vya maziwa, je wafugaji wa asili wanahusishwa vipi?
3.
Matatizo
mengineyo:
Mheshimiwa
Spika, Haya ni kama
kipato kidogo cha wananchi, wawekezaji kuwa na miradi mingi kwa pamoja, sekta
ya maziwa kutokuwa na mvuto kwa wawekezaji, ukosefu wa vyombo vya mikopo ya
muda mrefu na riba ndogo na kutokuwa na maeneo maalum yenye miundombinu ya
kutosha ya kujenga viwanda.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi
Upinzani inaitaka pia Serkali itafute njia ya kuimarisha vyama vya kitaifa vya
wadau (TAMPA, TAMPRODA) ili viwe kweli vya kitaifa na vyenye uwezo wa
kushirkiana na Serikali kundeleza sekta.
Mheshimiwa
Spika, nguzo ya 7 aya ya
7.2.3 ya kilimo kwanza inayosema kwamba “Kuainisha
na kuimarisha uwezo unaohitajika kwa kuendeleza sekta ya mifugo- Kwa mwaka 2010 serikali pamoja na TPSF ilitakiwa Kukarabati viwanda
vyote vya maziwa vilivyopo nchini na kuanzisha vituo vya kukusanyia maziwa”. Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge na wadau kwenye sekta hii
ya maziwa utekelezaji wa nguzo hii ya Kilimo kwanza imetimizwa kwa kiasi gani?
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa Mpango
wa Maendeleo wa miaka mitano inaonyesha ili sekta ya Mifugo iweze kuleta tija
tarajiwa ilitakiwa kwa mwaka wa fedha 2013/14 ipewe shilingi bilioni 275.98
kama fedha za maendeleo. Lakini kwa masikitiko makubwa mwaka huu
wa fedha Wizara imetengewa jumla ya shilingi bilioni 8.97. Kambi Rasmi
ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge ni kwanini imeshindwa kutekeleza
matakwa ya mpango wa maendeleo ambao ulipitishwa na Bunge?
G. SEKTA
YA UVUVI
Mheshimiwa
Spika, Tanzania inamiliki
maeneo makubwa ya maji ambamo rasilimali za uvuvi hupatikana kwa wingi. Maeneo
hayo ni pamoja na Ziwa Vctoria, Ziwa Tanganyika Ziwa Nyasa, Mabwawa
(Nyumba ya Mungu, Mtera na mengine mengi ya
asili), mito (Rufiji, Ruvu, Kilombero n.k.), malambo na maeneo oevu ambayo yana
fursa kubwa ya uvuvi hapa nchini. Aidha, kuna Bahari ya Hindi ambayo ina maeneo
mawili ya Bahari ya Taifa (Territorial Sea) na Ukanda wa Uchumi wa Bahari
(Exclusive Economic Zone - EEZ).
Sekta ya uvuvi inatoa mchango mkubwa katika
kuwapatia wanachi ajira, lishe, kipato, na kuingizia nchi fedha za kigeni.
Uvuvi nchini huendeshwa na wavuvi wadogo takriban 200,000 ambao huvua asilimia
zaidi ya 90 ya samaki wote wanaovuliwa nchini. Zaidi ya wananchi 4,000,000
hujishughulisha na kujikimu kutokana na shughuli zinazoendana na uvuvi hapa
nchini.
Mheshimiwa
Spika, Kutokana na
uharibifu uliopo katika uvuvi umesababisha kuwepo kwa upungufu mkubwa wa
rasilimali ya uvuvi, hususan katika Ziwa Victoria ambalo huongoza kwa
upatikanaji wa samaki aina ya Sangara ambao wamepungua kutoka tani 676,000
mwaka 2006 hadi tani 331,000 mwaka 2009. Hali hii imetokana na sababu
zifuatazo:-
a.
Ongezeko
la kasi ya matumizi ya zana haramu pamoja na ongezeko la idadi ya wavuvi kutoka
92,529 mwaka 2000 hadi 105,016 mwaka 2008;
b.
Ongezeko
la vyombo vya kuvulia samaki kutoka vyombo 30,171 (2000) hadi vyombo 52,174
(2008); na
c. Ongezeko kubwa la mahitaji ya samaki na mazao yake
katika soko la samaki ndani na nje ya nchi na hivyo kuwa kichocheo kikubwa cha
samaki wachanga kuvuliwa. Kwa upande wa Bahari ya Hindi, mathalani rasilimali
ya kambamiti imepungua kiasi cha kusababisha uvuvi wake kwa meli kubwa kufungwa
hadi sasa. Aidha, rasilimali ya Kambamiti (Prawns) imepungua kutoka tani 1,320
kwa mwaka 2003 hadi kufikia tani 205 mwaka 2007[5].
Mheshimiwa
Spika, pamoja na uwepo wa
ongezeko la mahitaji ya samaki na mazao yake katika soko, wavuvi wamekuwa
wakiilalamikia Serikali kuwa inakwamisha au kuwahujumu kwa uchomaji wa nyavu za wavuvi ambao hata hawaelewi ni kwanini
wanauziwa nyavu zisizostahili kwa mujibu wa Watendaji. Lakini ukweli ni kuwa
nyavu zote kustahili au kutostahili inategemea unavua samaki wa aina gani na
nyavu hizo zinatumika namna gani, hivyo basi kitendo cha kuchoma nyavu (Zana za
uvuvi) za wavuvi bila ya kuhakiki matumizi yake na bila ya kutoa nyavu (zana
mbadala) ni hujuma kwa sekta hii ya uvuvi na wavuvi wenyewe. Kumekuwepo na
tabia ya kufunga ziwa au kusitisha shughuli za uvuvi kiholela, bila taarifa au
sababu za kisayansi zinazotolewa kwa wavuvi.
Mheshimiwa
Spika, Mfano wa tabia hii
yenye kujenga hisia ya chuki za wananchi kwa Serikali yao ni Ziwa Basotu. Hili
ziwa limeingizwa kwenye mitego, chambo na chuki/ulipazaji visasi vya kisiasa tu
kumewekupo na shinikizo la ulipazaji kisasi ya kisiasa kwa kufungiwa ziwa mara
kwa mara ili wataabike, wasipate kitoweo na kipato na kuvuruga mfumo wao wa
maisha ya kila siku lakini sio ukweli wa hali halisi kuwa kuna uvuvi usiofaa. Je,
haya ndo mandeleo ya sekta ya uvuvi? Hivi jambo la kisayansi linaendeshwaje kisiasa?
Nadhani haya si maendeleo tuliyotarajia kwa mujibu wa ilani za CCM za mwaka
2005-10 na 2010-15 bali ni hujuma na
upandikizwaji wa mbegu mbaya za chuki ya kisiasa tu.
Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Waziri awaeleze
wananchi wa BASOTU kwanza ni nani mwenye mamlaka ya kusitisha uvuvi katika ziwa
na hatua zipi ambazo pia zinashirikisha wadau zinapaswa kufuatwa?
a. UFUGAJI
WA SAMAKI
Mheshimiwa Spika, shughuli za ufugaji wa
samaki unafanywa na wafugaji wadogo. Hata hivyo, ufugaji wa samaki lazima
ishindane na shughuli zingine za vijijini kwa eneo la ardhi, maji, nguvu kazi
na vyakula. Hali hii hupelekea umuhimu wa kutathmini gharama na faida ya
ufugaji samaki na mchango wake kwa maisha ya wakazi wa vijijini kulingana na
shughuli zao zingine.
Mheshimiwa Spika, zaidi ya hayo, ufugaji wa
samaki hukabiliwa na matatizo na changamoto zingine kama ukosefu wa sera
thabiti ya ufugaji samaki; mabadiliko katika sera za uchumi; ukosefu wa
teknolojia bora; upungufu wa vifaranga bora; miundombinu duni ya usafiri;
utafiti usiokidhi mahitaji; ukosefu wa takwimu za uzalishaji; upungufu wa
taarifa sahihi za utunzaji wa bwawa la samaki.
Mheshimiwa Spika, ili kuwa na uwezo wa kufanya
shughuli kwa mafanikio, ni muhimu kuwa na takwimu ya utendaji na shughuli husika.
Vivyo hivyo, ili kuendesha shughuli za ufugaji samaki kibiashara, mfugaji
analazimika kuchukua na kutunza takwimu kwa hatua zote au shughuli yoyote
anayoifanya ikiwemo ya kutunza matumizi na mapato ya fedha.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo
wa Miaka mitano, sekta ya Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2013/2014 ilitakiwa itengewe
jumla ya shilingi bilioni 60.896 ili
sekta nzima ya uvuvi iweze kuleta tija stahili pamoja na faida zingine ni
kwamba kama uwekezaji kwa mujibu wa mpango hadi 2015. Makusanyo ya Serikali kwa
mwaka katika sekta hii yalitakiwa kukua kutoka shilingi bilioni 6.58 hadi
shilingi bilioni 12.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaitaka Serikali iwaeleze watanzania ni kwanini Serikali imekinzana na
mpango wa Maendeleo ambao ulipitishwa na Bunge?
H. MAPITIO YA
BAJETI YA UTEKELEZAJI KWA WIZARA
Mheshimiwa Spika, Ukiangalia mwenendo wa bajeti
ya wizara kwa miaka minne inaonyesha kuwa bajeti ambayo imekuwa ikitolewa kwa
wizara hii imekuwa ikishuka, mwaka wa fedha 2010/2011 zilitengwa shilingi
bilioni 58.8, mwaka 2011/2012 zilitengwa shilingi bilioni 57.2, mwaka wa fedha
2012/2013 zilitengwa shilingi bilioni 54.6 na kwa mwaka huu wa fedha 2013/2014
zimetengwa shilingi bilioni 47.18
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani
inatoa tafsiri ya kupungua huko kwamba ni fundisho kwa watendaji wizara
kuangalia fursa za mapato ambazo zipo katika wizara hiyo zifanyiwe kazi na
ziweze kuwekezwa kwa maendeleo ya sekta hizi mbili-(Mifugo na Uvuvi), na kwamba
kutokana na ukweli ulipo wa fursa hizo wizara imelala na hata kusimamia sheria
na kanuni zilizopo za kuhakikisha mirabaha ya uvuvi inalipwa imeshindwa na
wajanja wanavuna raslimali yetu bila nguvu yoyote ya ziada.
I.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inasema kwamba, wizara hii kwa kipindi kirefu
imekuwa kama nyumba isiyokuwa na msimamizi kiasi kwamba raslimali za nchi hii
zimekuwa zikigawiwa, zikivunwa na kutumiwa bila kufuatwa kwa sheria na kanuni,
mfano mmojawapo ni ugawaji wa mashamba ya Ranchi za Taifa na kilichofuata ni nchi
kuingia kwenye migogoro mikubwa kati ya wafugaji na wakulima.
Mheshimiwa Spika, katika kuonyesha kuwa
Serikali imeshindwa kuthamini sekta ya mifugo kwa ujumla, mwaka 1981, Morogoro
Muasisi wa nchi hii Mwalimu J.K Nyerere alisema “tumetenga, kwa mfano, maeneo
maalum kwa ajili ya mazao kama pamba, kahawa, tumbaku na katani lakini
hatujatenga maeneo kama hayo kwa ajili ya mifugo.Tumetenga maeneo maalum kwa
ajili ya pundamilia (hifadhi za taifa) lakini wafugaji wananing’inia hewani
tu”.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani
inaona kama kungekuwa na umakini katika serikali hii ya CCM ni dhahiri kuwa
makosa ambayo yalikuwa yametendeka huko nyuma ulikuwa ni muda mwafaka wa
kurekebisha makosa katika sekta hii ya mifugo na hivyo yanayopelekea wafugaji
kuwa wahamiaji au watu wasiohitajika katika nchi yao kama ilivyo sasa.
Mheshimiwa Spika, mwisho lakini kwa umuhimu
mkubwa ni shukrani kwa wanachama na wapenzi wote wa Wilaya ya Maswa kwa
ushirikiano mkubwa wanaonipa katika kujenga na kuimarisha chama chetu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba
kuwasilisha.
………………………………………..
Slyvester Mhoja Kasulumbayi (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-
Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
[1]
Sera ya Taifa ya Mifugo, Desemba 2006
[2] SAGCOT Investment Partnership Program-Opportunities
for investors in the livestock sector- 11 October 2012
[4] Taarifa
ya tathmini ya hali ya viwanda Vya kusindika maziwa tanzania oktoba 2006. N.R. Mbwambo, C.M.D.
Mutagwaba, M. Tsoxo na A.E. Temba
[5] Maazimio ya mkutano
wa wadau wa sekta ya uvuvi uliyofanyika kwenye ukumbi wa chuo cha benki kuu, mwanza
kuanzia tarehe 16–18 desemba, 2009
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia