Mkurugenzi
wa Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Morrice Oyuke
akizungumza na wadau mbalimbali wakati wa kujadili Mpango Mkakati wa
Takwimu za Kilimo leo jijini Dar es salaam. Mpango huo utaiwezesha Ofisi
ya Taifa ya Takwimu kukusanya takwimu sahihi zinazokidhi viwango vya
ndani na vile vya kimataifa.
Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani (FAO) nchini Tanzania Bi. Diana Tampelman akizungumza na waandishi wa habari kupongeza hatua iliyofikiwa katika kukamilisha Mpango mkakati wa Takwimu za Kilimo nchini Tanzania na kueleza kuwa hatua hiyo inaendana na Mpango wa Dunia ulioanzishwa mwaka 2010 kwa lengo la kuboresha takwimu za kilimo maeneo ya vijijini.
Baadhi
ya washiriki wa mkutano wa Kijadili Mpango Mkakati wa Takwimu za Kilimo
wakifuatilia masuala mbalimbali wakati wa mkutano huo leo jijini Dar es
salaam.Picha na Aron Msigwa - MAELEZO.
======= ==== =====
Ofisi
ya Taifa ya Takwimu (NBS) inakamilisha Mpango mkakati wa Takwimu za
Kilimo wa mwaka 2014/15 mpaka 2018/19 utakaoiwezesha Ofisi hiyo
kuendesha zoezi la ukusanyaji wa takwimu za kilimo nchini kila baada ya
miaka 5.
Akizungumza
wakati wa mkutano uliohusisha wadau mbalimbali wa kupitia na kujadili
rasimu ya mwisho ya mpango huo leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa
Takwimu za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Morrice Oyuke amesema
kuwa mpango huo utaiwezesha Ofisi ya Taifa ya Takwimu kukusanya takwimu
sahihi zinazokidhi viwango vya ndani na vile vya kimataifa.
Amesema
mpango mkakati huo unalenga kuboresha shughuli za ukusanyaji wa
takwimu za kilimo hapa nchini kwa kujenga mfumo mmoja wa utoaji wa
takwimu za Kilimo kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuliko ilivyo sasa
na kubainisha kuwa taarifa zote za shughuli za kilimo nchini zitaingizwa
kwenye mfumo wa serikali.
“Hapa
tumekutana wadau mbalimbali kutoka serikalini kwa maana ya wizara
husika na wawakilishi kutoka mashirika ya maendeleo, lengo letu ni
kupitia na kujadili rasimu hii ya mwisho itakayotuwezesha kujenga uwezo
wa ndani wa ukusanyaji wa takwimu za kilimo kuanzia ngazi ya kijiji
mpaka taifa’’ Amesema
Amefafanua
kuwa mpango huo utaiwezesha Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bara na ile ya
Mtakwimu Mkuu Zanzibar kupata takwimu za shughuli zote za kilimo kuanzia
wazalishaji wenyewe, hali ya kilimo, mazao, masoko pia kutoa mwelekeo
wa nini kifanyike kuboresha sekta hizo kupitia takwimu zitakazokusanywa.
Aidha,
amesema kuwa vipaumbele vya mpango huo vimeshaainishwa na kuwekwa mbele
ya wadau ili kuwezesha upatikanaji wa nyenzo na uwezo wa kutekeleza
mpango huo.
Kuhusu
kufanikisha mpango huo Bw. Oyuke amesema kuwa jopo la taifa la
wataalam limeundwa likihusisha wataalam kutoka Ofisi ya Taifa ya
Takwimu na ile ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar, Wizara husika za Kilimo,
Chakula na Ushirika,Mifugo na Uvuvi, TAMISEMI, Maliasili na Utalii
pamoja na wataam kutoka mashirika ya maendeleo.
Kwa
upande wake Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani(FAO) nchini
Tanzania Bi. Diana Tampelman amepongeza hatua iliyofikiwa katika
kukamilisha Mpango mkakati huo nchini Tanzania na kueleza kuwa hatua
hiyo inaendana na Mpango wa Dunia ulioanzishwa mwaka 2010 kwa lengo la
kuboresha takwimu za kilimo maeneo ya vijijini.
“Tunapongeza
hatua hizi na tutaongeza nguvu zetu katika mpango huu ili kupata
uhalisia wa shughuli za kilimo Tanzania kuhusu nani kazalisha nini na
kwa kiwango gani ingawa watu wanaweza kushindwa kuona umuhimu wake
lakini tunajua kuwa taarifa hizi ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi”
Amesema Diana.
Naye
mtaalam kutoka Wizara ya Kilimo na Maliasili Zanzibar Bw. Mzee Mohammed
Mzee akiwasilisha mada kuhusu Hali ya Takwimu za kilimo nchini amesema
kuwa kwa kipindi kirefu takwimu za kilimo zimekuwa zikipatikana kupitia
Wizara na Taasisi zenye dhamana ya usimamizi wa sekta ya kilimo na
kusababisha upatikanaji wa takwimu zinazotofautiana kutokana na njia
zilizotumika wakati wa ukusanyaji wa takwimu hizo.
“Kisheria
Ofisi ya Taifa ya Takwimu hapa nchini ndio yenye dhamana ya kukusanya
na kusambaza takwimu, suala la ukusanyaji wa takwimu lina njia zake,
kumekuwa na shida ya ya njia za ukusanyaji wa takwimu hizi na wakati
mwingine takwimu kutofautiana ,kukamilika kwa mpango mkakati huu
kutaliondoa tatizo hili” Amesema.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia