Waziri wa
Maji, Profesa Jumanne Maghembe ameshangazwa na utitiri wa watu
wanaotaka kugombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu 2015, akisema nafasi hiyo
ya juu nchini haifanani na mashindano ya urembo ambayo mtu yeyote
anaweza kujaribu.
Mbunge
huyo wa Mwanga alisema watu hao wanaojitokeza kuwania urais hawaelezi
wanataka kulifanyia nini Taifa na akashauri wasioweza kueleza hoja zao
wasichaguliwe kushika nafasi hiyo.
“Urais
unahitaji kuwa na sifa, dira na ajenda kwa Taifa,” alisema Profesa
Maghembe wakati wa mahojiano maalumu na gazeti hili mjini hapa.
Kauli ya
Profesa Maghembe imekuja wakati Taifa likijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu
utakaofanyika Oktoba, 2015, huku chama chake, CCM kikikabiliwa na kazi
ngumu ya kumpata mrithi wa Rais Jakaya Kikwete ambaye anamaliza muda
wake.
Hali kama
hiyo iliikumba CCM wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka
1995 wakati takriban watu 20 walipojitokeza kutaka kuingia Ikulu na
baadaye mwaka 2005 wakati wa uchaguzi uliomuweka madarakani Rais
Kikwete.
Ndani ya
CCM, mjadala huo sasa umekumbwa na hoja ya umri baada ya makada vijana
kujitokeza kutangaza nia ya kumrithi Rais Kikwete kupambana na wanasiasa
wakongwe, baadhi wakiwa ni wale waliojiandaa kwa muda mrefu.
Hata
hivyo, Profesa Maghembe alipuuza mjadala huo wa umri wa mtu kugombea
urais akisema kuwa hauna msingi na kwamba sifa kuu ya mgombea urais ni
ajenda ya kuliletea Taifa maendeleo endelevu.
“Umri
hauwezi kuleta tofauti katika uongozi wa nchi. Ni kama kusema jiwe liwe
rais,” alisema mwanasiasa huyo mkongwe, ambaye amefanya kazi wizara
tofauti tangu Januari 2006 aliposhika uwaziri kwa mara ya kwanza.
Alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inataka mgombea urais awe na umri wa kuanzia miaka 40 na kuendelea.
“Hivyo
haisemi kuwa ukishakuwa na miaka 70 huwezi kuwa rais ama haisemi ukiwa
na miaka 40 unafaa zaidi kuwa rais. Inategemea huyo mtu anayegombea
anataka kuwafanyia nini Watanzania,” alisema.
Waziri
huyo wa saba tangu Wizara ya Maji ianzishwe, alisema kugombea urais
kunategemea ajenda aliyonayo mtu na hata watu wanapokwenda kumchagua,
lazima waangalie ana ajenda gani. “Ikulu si mahali pa kukimbilia, mimi
hata sijui wanakimbilia nini kwa sababu lazima mtu uwe na ajenda. Na
kama mnasikia mtu anasema mimi nataka kuwa tu rais, huyo hafai kabisa,”
alisema.
“Lazima
mtu anayetaka kuwa rais atueleze uchumi sasa unakua kwa asilimia saba na
umekuwa hivi kwa karibu miaka 10 lakini ni jambo linalofanya umaskini
uwe mkali kabisa na usiishe ni kutokana na shughuli inayofanywa na watu
wengi ya kilimo, kuwapatia kipato haikui kama sekta nyingine.
Alitoa
mfano sekta ya usafirishaji ambayo inakua kwa zaidi ya asilimia 28 na
sekta ya utalii kwa zaidi ya asilimia 18, lakini sekta ya kilimo inakuwa
kwa asilimia 4.2 tu wakati ndiyo inabeba karibu asilimia 77 ya
Watanzania.
“Lazima
hali hii ibadilike huko tunakokwenda. Sasa huyu rais atuambie
ataibadilishaje. Mtu anasema anataka aende Ikulu akae hata saa moja tu,
sasa saa moja unafanya nini? Hata nusu saa wewe unataka kwenda hapo
kufanya nini?” alihoji.
Alisema
kwa kipindi hiki ni lazima mtu anayetaka urais awaeleze Watanzania
atawezaje kuivusha nchi katika uchumi wa kati, vinginevyo haifai kushika
nafasi hiyo.
“Naona
watu wengi wanatangaza, mimi nataka kuwa rais, mimi nataka kuwa rais.
Ehhh unatakuwa rais (anaitika ehh), Watanzania unawaondoaje hawa
asilimia 77 waungane na wengine ili baada ya miaka yako 10 tuwe katika
uchumi wa kati?” alisema.
Alisisitiza
mtu ambaye anataka kuwa rais lazima awe na sifa na ajenda. “Lazima
atueleze ajenda yake nini? Siyo kwamba si unaniona mimi hata wakipiga
picha nafaa kuwa rais, hata kidogo,” alisema na kuongeza;
“Urais
siyo kama mashindano ya Lundenga ya kupeleka warembo kwenda
kuwashindanisha hata kidogo. Is Very important (ni muhimu sana), mimi
nadhani ndiyo sifa ya msingi.”
WANAWAKE NA URAIS
Profesa
Maghembe alisema haamini kwamba wanawake bado hawawezi kushika nafasi
hiyo ya juu serikalini. Wapewe fursa washindwe wenyewe.
Kwa mujibu wa Profesa Maghembe, wanawake wenye sifa ya kuwania urais na kushinda wapo na wakiweza wajitokeza ili wapigiwe kura.
“Unajua
kuna wengine wanasema ni mapema. Lakini tangu lini saa hizi saa nane
mchana unasema ni mapema, unataka wangoje usiku! Wamama wapo lakini na
muda wa kutangaza nia bado upo,” alisema na kuongea:
“Pia
tunaangalia hawa waliotangaza nia wataifanyia nini Tanzania. Kama wako
ambao wanaweza kufanya hiyo kazi, mnaingia huko, siyo marathon.”
HATMA YA UBUNGE WAKE
Profesa
Maghembe alisema kuwa kazi yake ya ubunge anaipenda sana na kwamba ni
kazi inayohitaji nguvu, ubunifu na kuwa tayari kukabiliana na changamoto
za maendeleo.
“Na ni
kazi ambayo inahitaji nguvu, ubunifu na inahitaji kuwa tayari
kukabiliana na changamoto za maendeleo. Kazi hiyo naipenda sana na bado
nina nguvu na nia ya kuifanya. Kwa hiyo katika uchaguzi mkuu ujao
nitagombea katika jimbo langu la Mwanga.
“Kwa hiyo
mimi siwezi kusema kuwa nikipata upinzani ni kitu kama unfair (siyo cha
haki) hivi, hata kidogo. Ni kitu ambacho ni sehemu ndani ya Chama Cha
Mapinduzi,” alisema.
Profesa Maghembe alisema ushindani ni kitu ambacho anafahamu kitakuwapo.
“Kila
wakati ushindani unakuwa mkubwa zaidi, nimepita katika chaguzi tatu na
kila wakati upinzani unakuwa mkali zaidi. Nategemea katika mwaka 2015
ushindani utakuwa ni mkubwa zaidi lakini nategemea nitashinda kwa
kishindo zaidi,” alisema.
Alisema hakuna kosa kwa watu kushindana katika chaguzi na ni haki yao ya uanachama.
Alipoulizwa
mambo matatu yanayomfanya kutegemea kushinda kwa kishindo katika
uchaguzi ujao, Profesa Maghembe alisema mojawapo ni utekelezaji wa ilani
ya CCM na miradi ya maendeleo imetekelezwa.
“Wananchi
matatizo yao yametatuliwa kwa kiwango kikubwa sana na tupo karibu nao,
kuwasikiliza na kuona kuwa tunaelekea wapi,” alisema.
Alisema
pia wananchi huangalia historia ya kipindi ambacho umeongoza na katika
jimbo lako wamekuwa wakipiga hatua kila kipindi na kutokana na hayo
utashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao.
NAFASI YA UPINZANI
Profesa
Maghembe alisema “Njaa ya wananchi wengi ni maendeleo, hivyo kile chama
kinachowaahidi Watanzania kuwaletea maendeleo kitaendelea kushinda
wakati wote,” alisema na kuongeza:
“Kile
kinacholeta matumaini ya mkate wao wa kila siku, kuwapatia watoto shule
kuendeleza vyuo vikuu, huduma nzuri za afya, maji na kuhakikisha mazao
kuingia sokoni ili wapate bei nzuri kitaendelea kutawala Tanzania kwa
muda mrefu.”
Alisema bado vyama vingi nchini vinaona kuwa kusimama majukwaani, kutoa sauti kubwa na ukali mwingi ndiyo kutawala nchi.
Alisema
vyama vitakapofika kwa wananchi katika ngazi ya chini na kutoa mpango
mbadala ya kuleta maendeleo nchini ndiyo vitaweza kuwa na ushindani.
Alisema hivi sasa vyama vya upinzani havina ushindani na CCM. “Wakina
Sangara, operesheni delete, kudelete haiboreshi shule,” alisema.
KATIBA
Katika
hatua nyingine, Profesa Maghembe alibainisha kuwa Mchakato wa Mabadiliko
ya Katiba unaendelea vizuri, ila kinacholeta mgogoro ni kitendo cha
Tanzania kuingia kwenye mchakato huo wakati bado Katika yake ya mwaka
1977 haijapoteza sifa.
Amesema Katiba hiyo iliyotuongoza kwa miaka 50 iliyopita bado ni nzuri, ndiyo maana kuna maoni tofauti juu ya mchakato wenyewe.
Alisema
Katiba iliyopo imewatumikia vizuri lakini wakasema kuna fursa nzuri ya
kutengeneza Katiba nzuri zaidi ya kuwatumikia vizuri zaidi kwa miaka
zaidi ya 100.
“Watanzania tumekuwa kama wale watu ambao wana koti halijachakaa, zuri tu lakini wakapeleka kwa fundi liwekwe kiraka,” alisema.
“Hapo
ndiyo tatizo, kwa sababu katika nchi, Katiba ni matokeo ya vita,
wamepigana vita sasa wamechoka wanataka tuongee amani, tunaandika
Katiba,” alisema na kuongeza:
“Sasa
sisi tunaandika Katiba mpya tukiwa na amani. Hatuna tatizo kubwa kwamba
watu wanapoongalia changamoto hawaliongelei hilo kama tatizo kwa sababu
tunayo Katiba nzuri ambayo imetubeba kwa miaka 50.”
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia