Leo nitazungumzia hatua na mbinu za kutambua
kipaji. Kabla ya kuzama kwenye somo lenyewe, hebu turejee kwanza kwenye
fasili na ufafanuzi wa neno kipaji:
Kipaji ni umahiri wa kipekee alioweka Mungu ndani
ya akili ya mtu unaoongoza usadifu wa viungo na fikra zake kufanya jambo
fulani kwa upekee kabisa.
Ni uwezo wa kipekee wa kuzaliwa nao uliojengeka
kwa binadamu unaompa nguvu mtu kufikiri kiutofauti au kufanya jambo kwa
umahiri mkubwa. Ni umaizi ndani ya michepuo ya akili ya mtu
inayomuongoza kufanya kitu au kufikiri kwa tija na upekee. Ni talanta
ambazo mtu anazaliwa nazo pasina kusomea. Elimu inasaidia tu kupalilia
na kukuza vipaji vya mtu ili avitumie kwa mafanikio makubwa.
Vipaji vinajidhihirisha kwenye umaizi wa kiakili,
kufikiri, kubuni, kuvumbua, kusanifu au vinaweza kuwa kwenye utumiaji wa
viungo vya mwili kama kucheza, ufundi, usanii wa fani mbalimbali na
mifumo wa kijamii na uwezo wa mwili kutenda. Kipaji ni tunu toka kwa
Mungu. Haijalishi unakitumia au hukitumii kitabaki kuwa ni chako daima.
Nilisema wiki iliyopita kuwa kosa kubwa
tunalofanya watu wengi ni kuishi kwa kuiga maisha ya watu wengine kana
kwamba wewe ni nakala (fotokopi) ya wengine. Nilisisitiza pia kuwa watu
mashuhuri na waliofanikiwa ni wale waliogundua na kutumia kikamilifu
vipaji vyao.
Wasani na wanamichezo wengi ni miongoni mwa watu
maarufu na matajiri duniani japokuwa wengi hawana elimu kubwa kiasi cha
kushangaza, walichofanya ni kutumia vipaji na vipawa vyao kikamilifu.
Sasa basi tunajuaje kama mtu una kipaji fulani? Haya ndiyo mambo yanaweza kumsaidia binadamu kutambua kipaji alichonacho:
Moja, uwe na shauku na jitihada ya kujaribu
kufanya vitu vingi pasipo kuchoka. Nilisema wiki mbili zilizopita kuwa
kipaji ni kama sukari iliyowekwa kwenye chai pasipo kukorogwa. Lakini
ikikorogwa ladha ya chai utaisikia.
Vivyo hivyo, tunahitaji kujaribu kufanya mambo
mengi tangu tukiwa watoto hadi ukubwani bila kuchoka. Watoto wana
jitihada kubwa za kujaribu mambo mengi. Hapo ndipo huanza mchakato wa
kuvumbua vipaji vyao.
Mara nyingi wazazi huanza kubashiri vipaji vyao
kwa kuangalia jitihada za watoto kujaribu na kufanya vitu kwa umahiri na
upekee. Ukiwa na kipaji cha kuimba lakini haujawahi kujaribu kuimba
huwezi kujua kama una kipaji hicho.
Ukiwa na kipaji cha kucheza mpira lakini hujawahi kucheza mpira huwezi kujua kama una kipaji hicho