Na: Calvin Gwabara – Arusha.
Mwandishi Mkuu wa sheria nchini Tanzania Bwana Onorius John Njole amewakumbusha Mawakili wa serikali nchini kuzingatia Katiba ya nchi wanapoandika sheria au wanapotoa ushauri wa kisheria kwa serikali katika jambo lolote.
Mwandishi Mkuu wa sheria nchini Tanzania Bwana Onorius John Njole akiwasilisha mada yake mbele kwenye mkutano huo jijini Arusha. |
Mwandishi huyo Mkuu wa Sheria ameyasema hayo wakati wa mafunzo ya pili ya mwaka ya Mawakili wa serikali nchini yanayoendelea Jijini Arusha na kuwakutanisha zaidi ya Mawakili 300 kutoka kila kona ya Tanzania.
“Katiba iongoze ushauri wowote mnaoutoa kwa Serikali katika jambo lolote linalohitaji ushauri wa kisheria kutoka kwenu kama Mawakili wa Serikali, lakini pia huwezi kuwa mshauri mzuri wa kisheria kama hujui mambo ya Muungano” alisisitiza Njole.
Aliongeza “Pamoja na kuwa mnatoa ushauri na Tafsiri kwa mujibu wa sheria kwa Serikali lakini lazima kuzingatia Sera, Mazingira na Ajenda za nchi na dunia kwa wakati huo”.
Mwandishi huyo Mkuu wa Sheria nchini amesema kwa sasa Serikali inahamasisha uwekezaji kwahiyo unapoletewa jambo utoe ushauri wakati unajua kuwa linakinzana na sera ya wakati huo sio vyema kuishia kusema kuwa sheria hairuhusu bali toa ushauri wa nini kifanyike kurekebisha sheria husika kama litakuwa na maslahi mapana kwa Taifa.
Bwana Njole amewasa mawakili hao wa serikali wanapotoa ushauri kwa kusema jambo fulani ni hatarishi kwa maendeleo ya nchi, basi ni vyema pia kusema namna ya kuzitatua ili tupate tija lifanyike kwa tija bila kuleta athari kwa nchi.
“Nyinyi kama Washauri wa Serikali kwenye masuala ya kisheria kwenye maeneo yenu lazima umjue mnayempatia ushauri, acheni kuandika maneno magumu na kuzunguka zunguka kwa maneno mengi, weka ushauri wako mwanzo tuu wakati mnashauri Mawaziri, Makatibu wakuu na viongozi wengine maana wana kazi nyingi hawawezi kuanza kusoma taarifa ndefu sana” alihimiza bwana Njole.
Akichangia mada hiyo Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Devisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumu, Mhe. Sirillius Matupa amewataka mawakili wa serikali hao wanapotoa ushauri wa Kisheria kama Wakili wa Serikali kuhakikisha ushauri wanaoutoa haupigi kelele.
“Mnapopewa jukumu la kutoa ushauri wa kisheria kwa serikali kuhusu jambo lolote hakikisheni ushauri mnaoutoa haupigi kelele, maana tumeshuhudia nyakati fulani unapokea ushauri kutoka kwa mtaalamu wa sheria lakini kunakuwa na malalamiko na maneno mengi sana kuhusu ushauri huo na hivyo kusababisha mtoa maamuzi kupata shida kwenye kuutumia” alisema Mhe. Jaji Mstaafu Matupa.
Mafunzo hayo ya siku tano yanawakutanisha mawakili wa serikali kutoka kwenye maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuwakumbusha mambo mbalimbali ambayo wanapaswa kuyazingatia wakati wanatekelez majukumu yao ili waweze kutoa mchango chanya kwenye maendeleo ya taifa.
MATUKIO KATIKA PICHA KWENYE MKUTANO WA BESPOKE2025
0 Comments
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia