Mkuu wa wilaya ya Babati Crispine Meela
Na Woinde Shizza,Babati
Maofisa ugani na makampuni ya usambazaji wa pembejeo Wilayani Babati
mkoani Manyara, wametakiwa kuwaelimisha wakulima aina ya mbegu na
mbolea bora zinazofaa kulingana na udongo wa eneo husika na kuachana
na kilimo cha mazoea.
Mkuu wa wilaya ya Babati Crispine Meela aliyasema hayo katika
kikao cha kamati ya pembejeo kilichokuwa kikijadili utekelezaji wa
mpango wa usambazaji wa pembejeo kwa mwaka 2015/2016 na changamoto za
utekelezaji huo.
Alisema kumekuwepo na dhana potofu kwa baadhi ya wakulima ya matumizi
ya mbolea katika ardhi kuwa yanaharibu udongo na mbegu mpya
zisizozoeleka kwa wakulima hazifai kutumika hivyo wataalamu wakitoa
shamba darasa watawaelimisha wakulima ipasavyo.
“Suala la pembejeo ni suala nyeti kwani ni mpango wa serikali wa
usambazaji wa ruzuku za vocha za pembejeo kwa wakulima na pia kilimo
ni uti wa mgongo wa Taifa letu hivyo tunapaswa kuwa makini katika
hilo,” alisema Meela.
Alisema wilaya hiyo imepokea vocha za sh1 milioni 1 ambapo makampuni
ya usambazaji wa pembejeo hizo kwa kupitia mawakala wao watawasambazia
wakulima wa maeneo husika na kuwawezesha kupata aina zote tatu za
mbegu, mbolea ya kupandia na kukuzia kwa wakati mmoja.
Alikemea baadhi ya makampuni kupitia mawakala wa usambazaji wasio
waaaminifu wanaoendelea kutoa aina moja ya mbegu na makampuni hayo
yazingatie sheria na kanuni za mkataba waliowekeana na halmashauri,
kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.
Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Babati Hassan
Lugendo alitaka zoezi la usambazaji wa pembejeo kuharakishwa kuwafikia
wakulima kwa wakati ili kuepuka malalamiko ya ucheleweshaji wa ruzuku
za vocha hizo.
Ofisa kilimo, umwagiliaji na ushirika wa mji wa Babati, Daniel Luther
alisema kati ya aina ya vocha 3,000 zilizotolewa ni vocha 821 pekee
zimekwishapatiwa wakulima kutokana na changamoto za wakulima
kupendelea kuchukua mbegu bila mbolea.
Luther alitaja sababu nyingine zilizosababisha kutochukuliwa vocha
nyingi ni kuchelewa kuanza kwa msimu wa kilimo katika maeneo mengi na
uelewa mdogo wa wakulima katika kutumia aina mpya ya mbegu na mbolea.