Ticker

6/recent/ticker-posts

WAKULIMA MOSHI VIJIJINI WASEMA N2AFRICA IMEWATOA GIZANI NA KUWAPELEKA KWENYE MWANGA

Na Mathias Canal, Kilimanjaro

Wakulima wa mazao ya jamii ya mikunde hususani maharagwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini Mkoani Kilimanjaro wamesifu mbegu bora aina ya Lyamungo 90, Jesca na Uyole Njano zinazotolewa kwa wakulima na Taasisi ya Kimataifa ya utafiti wa mazao ya kilimo cha Kitropiki (IITA) kupitia Mradi wa N2AFRICA.

Mradi huo unaotekelezwa kwa wakulima 11 katika vijiji sita vya Wilaya hiyo umekuwa na mafanikio makubwa kwao kutokana na mafunzo waliyopatiwa ya kulima kisasa kwa kutumia mbegu kidogo na mavuno makubwa pamoja na kutumia mbolea. 

Wakulima hao wanasema awali kabla ya mradi huo walikuwa wanalima kwa kuchanganya zaidi ya mazao ya aina mbili tofauti katika shamba moja, kutotumia mbolea na kulima pasipo kufuata njia za kitaalamu jambo ambalo liliwapelekea kupata mazao kidogo ambayo hayakuwa na ufanisi mkubwa katika kuimarisha uchumi wao.

Wanasema Kupitia mbinu bora walizojifunza kwa wataalamu kutoka katika Mradi wa N2AFRICA wamebadili mfumo wa maisha kwani kwa sasa wanapata mazao ya kutosha na kuwafanya kuhamia katika kilimo chenya tija kwa ajili ya chakula na biashara.

Janeth Godwin Shao, Achibold Masimba, Mary Mbuya na Fredy Urio wakazi wa kijiji cha Kiruweni , Elizabeth Paschal,na Ester Mbando wakazi wa kijiji cha Mawanjeni Kata ya Mwika Kusini wanasema kabla ya Mradi wa N2AFRICA walikuwa wanapanda mazao shambani badala ya kupanda mbegu jambo lililofifisha upatikanaji wa mazao mengi.

Waliomba mradi huo kuongeza zaidi ufanisi baada ya kufanikiwa katika kuwanufaisha wakulima kupitia zao la maharagwe sasa waongeze mafunzo kwa wakulima ili kutoa mbegu za mazao mengine kama vile kunde na choroko.

Moja ya malengo muhimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, ni kuitoa Tanzania katika kundi la nchi masikini zaidi duniani  na kujenga uwezo zaidi wa kiuchumi kupitia kilimo utakaoifanya iwe miongoni mwa nchi zenye kipato cha kati kimataifa.

Mtaalamu wa Kilimo katika Kijiji cha Mawanjeni Kata ya Mwika Kusini Elizabeth Josiah alisema kwa sasa Zao la maharagwe linapendwa na wakulima wengi kwa sababu linachukua muda mfupi kukomaa, halina gharama kubwa katika uzalishaji wake na lina bei nzuri sokoni karibu nyakati zote hata wakati wa mavuno (yaani msimu wake). 

Alisema kuwa Mkulima anaweza kulima maharagwe kwa matumizi ya chakula nyumbani kwake au kwa biashara reja reja au kwa jumla.

Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Kata ya Mwika Kusini Wilfred Ngile alisema Urahisi wa kulima maharage na faida zake lukuki ni kivutio kwa watu wengi sana kwa sasa huku akisema kuwa lakini bila kufuata muongozo wa kitaalam ni ndoto kwa mkulima kupata mavuno anayotarajia.

Alisema mafanikio wanayoyapata wakulima sio ya wataalamu bali ni mafanikio yao wenyewe kutokana na kutumia njia bora kutokana na maelekezo wanayoyapata kutoka kwa wataalamu.

Aidha, aliongeza kuwa mafanikio hayo yanatokana na Mbegu bora zilizofanyiwa tafiti na Taasisi ya Kimataifa ya utafiti wa mazao ya kilimo cha Kitropiko (IITA) na kutambulika kisheria ambazo ni pamoja na Uyole Njano, Lyamungu 90, na Jesca.

Naye Afisa Mazao wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini Bi Joyce Kessy alizitaja changamoto zinazowakabili wakulima kuwa ni pamoja na uzalishaji mdogo kwani wanazalisha chini ya tani moja kwa hekta ambapo unachangiwa na sababu za kurudia mbegu, kutotumia mbegu za viwandani, kupanda bila kuacha nafasi, na kupanda zao moja kwa kuchanganya na mazao mengine.

Hata hivyo alisema kuwa mara baada ya Mradi wa N2AFRICA kuanzishwa katika Wilaya ya Moshi Vijijini hamasa imekuwa kubwa kwa wananchi kuhitaji mbegu na mbolea kutoka taasisi ya IIAT hivyo ameiomba taasisi hiyo kuongeza utoaji wa mbegu kwa wakulima wote na kutoa mafunzo.

Alisema kuwa mradi huo umesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha  sekta ya kilimo nchini Tanzania jambo ambalo limerahisisha utendaji wa serikali kupitia Wizara ya Kilimo.

Alisema kuwa wakulima wanajifunza zaidi kwa vitendo kuliko nadharia hivyo aliiomba Taasisi hiyo ya IITA kupitia Mradi wa N2AFRICA kuvifikia vijiji vyote na kuwanufaisha wananchi kwa mafunzo ya vitendo zaidi.

Katika awamu ya kwanza ya Mradi huu ilianzishwa mwaka 2009 na kutekelezwa katika nchini DR Congo, Ghana, Kenya, Liberia, Malawi, Nigeria, Rwanda, Sierra Leone na Zimbabwe ambapo  Awamu ya pili ilianza Januari 2014 na kufanyika katika nchi tano za Ethiopia, Ghana, Nigeria, Tanzania, na Uganda.

Janeth Godwin mkulima wa maharagwe Kijiji cha Kireweni Kata ya Mwika Kusini akielezea jinsi alivyonufaika na mbegu za maharagwe zilizotolewa na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa mazao ya kilimo cha Kitropiki (IITA) kupitia mradi wa N2AFRICA
Wakulima wa zao la maharagwe walipowapokea wataalamu kutoka IITA katika kata ya Mwika Kusini, Wilaya ya Moshi Vijijini
 Achibold Masimba mkulima wa maharagwe Kijiji cha Kireweni Kata ya Mwika Kusini akielezea jinsi alivyonufaika na mbegu za maharagwe zilizotolewa na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa mazao ya kilimo cha Kitropiki (IITA) kupitia mradi wa N2AFRICA
 Elizabeth Paschal mkulima wa maharagwe Kijiji cha Kireweni Kata ya Mwika Kusini akielezea jinsi alivyonufaika na mbegu za maharagwe zilizotolewa na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa mazao ya kilimo cha Kitropiki (IITA) kupitia mradi wa N2AFRICA
Mtaalamu wa kilimo kijiji cha Mawanjeni Kata ya Mwika kusini Elizabeth Josiah akielezea jinsi wakulima wanavyonufaika na kilimo cha maharagwe
Ester Mbando (kulia) Mkulima wa maharagwe Kijiji cha Mawanjeni Kata ya Mwika Kusini akielezea jinsi alivyonufaika na mbegu za maharagwe zilizotolewa na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa mazao ya kilimo cha Kitropiki (IITA) kupitia mradi wa N2AFRICA
Mkulima wa zao la maharagwe Kamili Minja akionyesha jinsi alivyonufaika na kilimo cha maharagwe na hatimaye kununua mbuzi saba wa maziwa.
Mkulima wa zao la maharagwe  Joseph Towo kutoka Kijiji cha Rauya Kata ya Marangu Mashariki akielezea jinsi alivyonufaika na mbegu za maharagwe zilizotolewa na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa mazao ya kilimo cha Kitropiki (IITA) kupitia mradi wa N2AFRICA
Wanufaika wa mradi wa N2AFRICA wakielezea namna walivyonufaika na kilimo cha maharagwe
Fredy Urio akisimulia changamoto alizokabiliana nazo kabla ya mradi huwa kuwasili kijijini kwao na kuwa na manufaa kwa wakulima
Afisa kilimo Kata ya Mwika kusini Wilfred Ngileakielezea jinsi wakulima walivyonufaika na Mradi wa N2AFRICA katika kata hiyo
Mkulima wa zao la maharagwe Kamili Minja akionyesha jinsi alivyonufaika na kilimo cha maharagwe na hatimaye kununua mbuzi saba wa maziwa.
Mkulima wa zao la maharagwe Kamili Minja akielezea jinsi alivyonufaika na kilimo cha maharagwe na hatimaye kununua mbuzi saba wa maziwa. Wengine ni wataalamu kutoka IITA na Mhariri wa Mtandao wa www.wazo-huru.blogspot.com Ndg Mathias Canal
Mkulima wa zao la maharagwe Kamili Minja akionyesha shamba lake jinsi lilivyostawi kutokana na mafunzo ya kilimo bora kwa kutumia mbegu bora za maharagwe

Post a Comment

0 Comments