WANANCHI KONDOA WAIOMBA SERIKALI IWAREJESHEE SEHEMU YA ARDHI YAO PORI LA AKIBA MKUNGUNERO
Mmoja
wa wakazi wa kijiji cha Ikengwa, Nade Laida, akibubujikwa machozi
wakati wa mkutano kati ya wanakijiji na msafara wa Waziri wa Maliasili
na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangala kutokana na kile kilichoelezwa kuwa
mwanamke huyo ni mmoja wa waathirika wa mgogoro baina ya Pori la Akiba
Mkungunero na wananchi wa vijiji vinavyozunguka pori hilo picha na Woinde Shizza, Kondoa.
Na Woinde Shizza
Wakazi wa vijiji 11 kwenye kata sita waishio jirani
na Pori la Akiba la Mkungunero lililoko Wilayani Kondoa mkoani Dodoma,
wameiomba Serikali iwarejeshee eneo la kilometa 12 kuanzia kwenye vijiji vyao
kwenda ndani ya Pori hilo ambalo wanadai limechukuliwa kinyemela na Wizara ya
Maliasili na Utalii na kuathiri maisha yao yanayotegemea kwa kiasi kikubwa
kilimo na ufugaji.
Wakazi wa vijiji vya Ikengwa, Keikei Tangini,
Keikei na Kisondoko,kwa niaba ya wenzao wa wanaozunguka pori hilo wametoa maombi hayo mbele ya Waziri wa Maliasili na Utalii
Dkt. Hamisi Kigwangala wakati alipofanya ziara katika vijiji hivyo
vinavyozunguka Pori hilo la Akiba ili kutatua mgogoro wa muda mrefu baina ya
Pori hilo na wananchi wanaolizunguka.
Wananchi na viongozi wa vijiji hivyo wameeleza kuwa
uwekaji wa mipaka ya Pori hilo haukuwa shirikishi na kwamba maeneo makubwa ya
vijiji yaliyokuwa yakitumiwa na wananchi kwa shughuli zao za kilimo, ufugaji na
makazi yametwaliwa na kusababisha mgogoro huo.
Malalamiko mengine ya wananchi hao ni kunyanyaswa
na watumishi wa Pori la Akiba Mkungunero kwa kupigwa, kunyang'anywa mifugo yao,
na baadhi yao kudai kuumizwa na baadhi ya wenzao kuuawa kwa risasi na askari
wanaolinda Pori hilo.
Kwa Upande wake Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,
ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini Dkt. Ashatu Kijaji, ameiomba
Serikali kutumia busara na kurejesha eneo lililochukuliwa kimakosa kutoka kwa
wananchi ili waweze kujiendeleza kiuchumi na kuishi kwa amani na utulivu.
"Najua wewe ni mwadilifu ndio maana umeaminiwa
na Mhe. Rais, najua utawatendea haki wananchi wa vijiji hivi ili nao wajione ni
wananchi halali katika Taifa lao huru la Tanzania tukienda hatua kwa hatua bila
kuvunja sheria za nchi" alisisitiza Dkt. Kijaji
Amefafanua kuwa maeneo yaliyochukuliwa na Pori hilo
yalikuwa yakitumiwa na wananchi kwa muda mrefu na kwamba mchakato wa kupandisha
hadhi eneo hilo kutoka Pori Tengefu hadi kuwa Pori la Akiba la Mkungunero
haukuwashirikisha wananchi.
Akijibu Hoja za Wananchi hao, Waziri wa Maliasili
na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangala, pamoja na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa uhifadhi
kwa ustawi na maendeleo ya nchi, aliwahakikishia wananchi hao kwamba Serikali
itatafuta njia ya bora ya kuumaliza mgogoro huo kwa maslahi ya pande zote
mbili, wananchi na Serikali.
"Ni lazima tutafute mahali ambapo tutabalance,
maslahi ya umma na maslahi mapana ya Taifa zima na niwahakikishie kuwa
tutafanyakazi hiyo kwa uadilifu, uzalendo mkubwa, lakini zaidi kwa kuzingatia
maslahi yenu wananchi wenzetu" Alisisitiza Dkt. Kigwangala.
Awali, Meneja wa Pori hilo, Emmanuel Birasso,
alieleza kuwa mchakato wa kuanzisha Pori hilo la Akiba Mkungunero ulifuata
taratibu za kisheria za uanzishwaji wa mapori ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha
wananchi jambo ambalo linapingwa na wananchi hao.
Alieleza kuwa mpaka sasa takriban kilometa 118 za
mpaka wote wa Pori umesimikwa alama za mipaka na kuwaondoa watu wanaodaiwa
kuvamia Pori hilo pamoja na kuimarisha ulinzi na doria.
Pori Tengefu la Mkungunero (Game Controlled Area)
lilipandishwa hadhi na kuwa Pori la Akiba la Mkungunero mnamo mwaka 1996 kwa
Tangazo la Serikali (GN) namba 307, likiwa na ukubwa wa kilometa za mraba
743.95.
0 Comments:
إرسال تعليق
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia