MBUNGE ANNE KILANGO ATANGAZA KUHAKIKISHA ANAKULA SAHANI MOJA NA FEDHA ZA MIRADI YA MAJI.

 

 




Ziara ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso katika Jimbo la Same mashariki mkoani Kilimanjaro imeanza kuzaa matunda baada ya jimbo hilo kupata fedha zaidi ya Bilioni 3 kutekeleza miradi mbalimbali ya maji.


Kukamilika kwa miradi hiyo itapelekea baadhi ya maeneo ambayo hayakuwahi kufikiwa na huduma ya maji safi na salama tangu Tanzania kupata uhuru kufikiwa na huduma hiyo ya maji safi na salama.



Katika kuonyesha umuhimu wa huduma hiyo kwa wananchi Mbunge wa Jimbo la Same mashariki, Anne Kilango Malecela amefanya ziara ya kutembelea miradi hiyo na kujionea shughuli zinazoendelea.


MRADI WA MAJI BENDERA.



Kata hii ya Bendera ni miongoni mwa maeneo ambayo hayajawahi kupata huduma ya maji tangu Uhuru hali iliyopelekea Mbunge Kilango kumpigia magoti Waziri wa Maji kutatua tatizo hilo.


Kwa mujibu wa Meneja wa RUWASA wilaya ya Same, Mhandisi Alphoce Mlay amesema kuwa mradi huo ambao utagharimu milioni 500 ambazo ni fedha za uviko 19 huku akidai kuwa mradi huo umeibuliwa na Mbunge Anne Kilango.



Mhandisi Mlay amedai kuwa mradi huo utahusisha ulazaji wa mabomba km 22, ujenzi wa tanki pamoja na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji katika kata hiyo na unarajiwa kukamilika mwishoni mwa Septemba mwaka huu.


"Kukamilika kwa mradi huo kutawahudumia wananchi wapatao 4000 ambapo awali tulikuwa na changamoto ya upatikanaji wa mabomba lakini kwa sasa changamoto hiyo imeshapata utatuzi" alisema Mhandisi Mlay.



Kwa upande wake, Mbunge Anne Kilango Malecela amesema kuwa kuomba kwa mradi huo ni baada ya kuona mradi mkubwa wa Maji Same-Mwanga- Korogwe hautawanufaisha wananchi wa Jimbo la Same mashariki.


Anne Kilango anasema kuwa, Jimbo hilo linakabiliwa na changamoto kubwa ya maji hali iliyopelekea kufika kwa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na kumfikia kilio ambapo Mei 5 mwaka jana alimtuma Katibu Mkuu wa Wizara ya maji kufika Jimbo hapo na kujionea ukubwa wa tatizo na badae Julai 7 mwaka jana Waziri mwenyewe alifika na kuahidi miradi ya maji.



Mbunge huyo, amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo ambaye ni Jamta Construction Co. Ltd kuhakikisha anakamilisha mradi kwa wakati ili wananchi wanufaike na mradi ambalo ndilo lengo la Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hasani.


Aidha Mbunge huyo ametumia nafasi hiyo kumuomba Meneja wa RUWASA wilaya ya Same pindi gari la kuchimba visima vya maji ardhini litakapofika katika wilaya hiyo Jimbo hilo lipewe kipaombele kutukana na changamoto kubwa inayowakabili wananchi.


MRADI WA MAJI KATA YA KIHURIO.



Ziara hiyo ya Mbunge Anne Kilango Malecela ilimfika katika mradi wa Maji kata ya Kihurio unaogharimu Milioni 247 ukijumuisha uboreshaji wa miundombinu ya maji na upanuzi pamoja na ujenzi wa vituo 7 vya kuchotea maji.


Baadhi ya wananchi katika kata hiyo wamekuwa wakilazimika kutumia maji ya mto ambayo maji yake sio safi na salama ambapo alifurahishwa kukuta wananchi wa kijiji cha Igulundi wapatao 1200 wanapata maji safi na salama kupitia mradi huo.



Mbunge Anne alipokea changamoto kutoka kwa wananchi ya kupasuka kwa mabomba tangu kuanza kwa mradi huo kutokana na presha kubwa ya maji na kumtaka Meneja Ruwasa kuitafutia ufumbuzi changamoto hiyo.


"Tunakwenda kumaliza changamoto ya maji kwa kiasi kikubwa katika kata ya Kihurio kupitia mradi huu lakini wananchi mnaoomba kuunganishiwa maji majumbani ni lazima mkubali kufungiwa dira za maji hii itasaidia kupunguza matumizi yasiyo na ulazima" alisema Anne Kilango.



Mbunge huyo aliitaka Ruwasa kubadilisha mabomba yaliyochakavu katika mradi huo ambayo yamekuwa yakipasuka na kufunga mapya kisha kuufanyia majaribio mradi huo kabla ya kuwakabidhi wananchi kuusimamia.


MRADI WA MAJI KIJIJI CHA KIRORE KATA YA MIAMBA.



Mbunge Anne Kilango alifika katika mradi wa Maji wa Kirore ambapo Serikali imetoa milioni 51 kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo kwa kushirikiana na nguvu za Wananchi.


Fedha hizo zilitolewa na Serikali kwa ajili ya ununuzi wa vifaa pamoja na ujenzi wa tanki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi maji Lita za ujazo 50,000 pamoja na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 7 huku wananchi wakijitolea nguvu kazi ya kuchimba mitaro na kufukia mabomba.



Kwa mujibu wa Meneja Ruwasa wilaya ya Same, Mhandisi Alphoce Mlay amesema kuwa mradi huo umekuwa ukisuasua kutoka na wananchi kujitokeza nguvu kazi (msaragambo) kwa wiki mara moja.


Amesema kuwa, ofisi ya Ruwasa uliomba fedha Serikali awamu ya pili Milioni 20 kwa ajili ya kumalizia mradi huo ambapo kwa mwaka huu wa fedha wameipata fedha hiyo.



Wananchi wa kijiji hicho walionyesha kutoridhishwa na chanzo cha maji hayo kutoka Lomwe ambapo ni kata ya Lugulu wakihofia kuibuka kwa mgogoro wa kugombea maji na kuwaomba wataalam wa Ruwasa kuona uwezekano wa mradi huo kuchukulia chanzo chake Mikimbo.


Mbunge Anne Kilango Malecela, alimtaka Meneja wa RUWASA kufanya tathimini na kujionea chanzo hicho cha Mikimbo kama kitafaa ili kuepuka kuwepo na migogoro ya kugombea maji baina ya kata hizo mbili na kupelekea mradi huo kutofikia malengo yaliyokusudiwa na Serikali.


MRADI WA MAJI KATA YA VUJE WENYE THAMANI YA BILIONI 1.52.



Mradi huu ambao ni mkubwa kwa Jimbo la Same mashariki unatarajiwa kuhudumia vitongoji 5, kaya 900 na wananchi wapatao 4000 ambapo kwa sasa umefikia asilimia 70.


Mradi huo utajumuisha ujenzi wa ofisi ya Jumuiya ya maji yenye vyumba vitatu kwa ajili ya shughuli za ofisi na ukumbi mmoja kwa ajili ya vikao, tenki lenye ujazo wa Lita 150,000.



Meneja wa Ruwasa wilaya ya Same, Mhandisi Alphoce Mlay amesema kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika Disemba 18 mwaka huu ambapo kwa sasa zoezi la uchimbaji mitaro kwa ajili ya kulaza mabomba kwa urefu wa kilomita 61 shughuli imeshakamilika mkandarasi anachosubiria ni msamaha wa Kodi ili aweze kuingiza mabomba.


Amesema kuwa, eneo hilo lilikuwa na changamoto kubwa ya maji ambapo waliandaa andiko na kumfikishia Mbunge Anne Kilango Malecela alilolipeleka kwa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na kutoa fedha.



Mbunge Anne Kilango Malecela amesema kutokana na fedha nyingi ambazo Serikali imeziweka katika kata ya Vuje katika mradi wa Maji hayupo tayari kuona tatizo la maji likiendelea.


Amewaahidi wananchi kuhakikisha anafuatilia mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati na kuwanufaisha.


Mbunge huyo pia amemtaka Meneja wa Ruwasa wilaya ya Same kufanya ziara katika kijiji cha Vuje kujionea malalamiko ya wananchi kuhusu mradi huo na kuyapatia ufumbuzi kabla ya Mkandarasi hajakamilisha ujenzi.



MKUU WA WILAYA YA SAME, EDWARD MPOGOLO AIBUKIA KWENYE ZIARA.



Mkuu wa wilaya ya Same, Edward Mpogolo amefika kijiji cha Kirore kata ya Miamba na kukuta Mbunge Anne Kilango Malecela akizungumza na wananchi wa kijiji hicho.


Akizungumzia katika mkutano huo, Mpogolo Mbunge wa Jimbo la Same mashariki amekuwa akipambana kuhakikisha Serikali inapeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika Jimbo hilo.



Amesema kuwa, kulikuwa na changamoto ya barabara kupitika kwa tabu ndani ya Jimbo hilo lakini kupitia juhudi kubwa zinazofanywa na Anne Kilango kwa sasa barabara nyingi zinapitika muda wote.


Mpogolo amesema kutokana juhudi hizo Jimbo hilo limepata zaidi ya Bilioni 4 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwataka wananchi kumuunga Mbunge huyo pamoja na Rais Samia Suluhu Hasani katika kuwaletea maendeleo.

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

إرسال تعليق

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia