KUTOKA UTUMISHI WA SERIKALI HADI UJASIRIAMALI

 Na Woinde Shizza,Arusha

'takwimu za usawa wa kijinsia katika ajira zinaonyesha kwamba kufikia mwaka wa 2014 Watanzania milioni 2.1 walikuwa wameajiriwa katika sekta rasmi.

Mwaka 2014, Tovuti ya BBC ilichapisha takwimu za usawa wa kijinsia katika ajira zinaonyesha kwamba kufikia mwaka wa 2014 Watanzania milioni 2.1 walikuwa wameajiriwa katika sekta rasmi, ikiwa ni pamoja na serikalini na sekta binafsi.  

Hata hivyo takwimu rasmi za serikali  zinaonesha kwamba zaidi ya 60% ya wanawake walio kati ya umri wa miaka 18 hadi 24 yaani million 13.9 wanajishughulisha na shughuli zisizo rasmi yaani biashara ndogondogo na kilimo.

 Hii maana yake ni kwamba ni asilimia 0.75 tu ya wanawake walioko katika umri wa kufanya kazi ndio wapo katika sekta rasmi.

 Kwa maneno mengine, idadi kubwa ya wanawake walioko katika umri wa kufanya kazi nchini Tanzania ni wajasiriamali

Wanawake hawa wanajihusisha na shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kubuni bidhaa mbalimbali huku wengine wakifanya biashara katika vikundi au mtu mmoja mmoja. 

Hata hivyo, kilio cha ajira kinaongezeka nchini, baadhi ya watu wamekua wakiacha ajira rasmi na kuhamia kwenye biashara.

 Magreti Wilfred ni mwanamke  mfanyabiashara ambaye aliamua kuachana na ajira yake ya ualimu wa shule ya msingi serikalini na kuamua kuingia kwenye uwekezaji.

 Magreti anawekeza katika biashara mbalimbali ambazo zimempelekea kuajiri watu wakiwemo vijana na wanawake mbalimbali katika mkoa wa Arusha.

Magreti ni mwanamke mweye umri wa miaka (49), mkazi wa Njiro jijini Arusha ambaye ni mzaliwa wa Kilimanjaro. 

Magreti alipata elimu yake ya msingi katika shule ya msingi Lukani na baadae kupata elimu ya sekondari katika shule ya sekondari ya Boloti zoti zikiwa mkoani humo. 

Mara baada ya kuhitimu wazazi wake walimpeleka katika chuo cha ualimu cha Ekenfodi kilichopo mkoani Tanga.

Magreti alifanya kazi ya kufundisha kwa muda wa miaka mitano, baada ya hapo aliamua kuachana na kazi hiyo na kujiajiri. 

Alianza kwa kufanya biashara ndogondogo kwa kipindi kirefu hadi kufikia hatua ya kuwa na biashara zaidi ya moja na kuweza kuajiri watu wengine.

CHANZO CHA KUAMUA KUJIAJIRI  NI NINI?

Ili kuelewa nini kilichomsukuma kuacha ajira rasmi yenye mafao na kujiajiri, nilimtafuta Magreti atueleze ilikuaje?

 Magreti anaeleza sababu iliompelekea kuachana na kuajiriwa serikali kuwa ni hamasa ya kutimiza ndoto zake ambazo alikuwa nazo kwa kipindi kirefu. 

Ndoto hiyo, ilikuwa ni kufungua biashara na kuajiri wengine kutokana na biashara yake

“siwezi sema kuwa niliacha kazi serikalini kwa kuwa mshahara ni mdogo… hapana bali nilikuwa na nia ya kufungua biashara yangu ambayo nitakuwa nikiifanya kwa uhuru na bila kubanwa. 

Huku serikalini nilikuwa nabanwa sana na muda hali ambayo ilikuwa inapelekea hata kushindwa kufanya kazi zangu binafsi.

 Hali hiyo ilinipelekea kuacha huko na kuanza kujiajiri kwa kufuata ndoto zangu za kuwa na biashara bila yangu ambayo itaniweka huru na sitabanwa tena na ajira ya serikalini”

LENGO LAKE HASA NI NINI?

Magreti anaenda mbali zaidi na kubainisha kuwa lengo kubwa la kuanza kufanya ujasiriamali kwanza kabisa ni kuweza kujiingizia kipato kikubwa kitakacho weza kumsaidia kuendesha maisha yake binafsi na ya familia yake.

 Pili ana lengo la kuajiri wanawake wenzake na kuwapa elimu zaidi ya faida za kujiajiri na kujitafutia fedha wenyewe. 

Pia amekuwa akiwashauri baadhi ya wanawake waliofika nyumbani kwake kupata ushauri jinsi ya kuanzisha biashara pamoja nakujiajiri ili waweze kujikwamua kiuchumi

Mama huyu pia amekuwa akitoa elimu kwa wanawake ya faida za kujiajiri kwa kuwapa ushauri wafanyakazi wake ambao wamefanya nae kazi kwa kipindi cha muda mrefu kuhifadhi fedha ndogo ambazo wanazipata katika mishahara yao kwa ajili ya kuandaa mtaji watakao tumia kufungua biashara zao.

YEYE BINAFSI ANAFANYA BIASHARA GANI NA ALIANZAJE?

Magreti amekua akijishughulisha na biashara mbalimbali ikiwemoya ufugaji  wa kuku  wa nyama na mayai, biashara ya vyungu vya kupandia maua, biashara ya maua, biashara ya nguo za maharusi pamoja na biashara ya urembo mbalimbali wa majumbani.

Anaenda ndani zaidi na kutueleza kuwa alianza na bashara ya ufugaji wa kuku wa nyama ambapo alianza na vifaranga 200 lakini sasa mtaji wake ni mkubwa zaidi na anaweza kuingiza hata vifaranga 2,000 kwa wakati mmoja.

“kazi hizi sifanyi mwenyewe yaani za kuhudumia bali nina vijana ambao nimewaajiri ambao ndio nashirikiana nao kuhudumia wanyama, kutengeneza vyungu na dukani.

 Kwa kweli nimekuwa chachu ya wanawake wengi maana wapo wanao niona ninavyo chacharika wananifata na kuniomba ushauri.

 Na wengine wanataka kufanya biashara kama yangu, nimekuwa sio mchoyo wakija nawashauri na kuwaeliza’’ alifafanua.

MWANAMKE AMBAYE AMEVUTIWA NA KUANZA BIASHARA.

Maisha ya MAgreti yanaendana na maelfu ya wanawake wajasirimali wengine nchin Tanzania. Katika tamasha la wanawake wajasiliamali wajulikanalo kama 'Purple planet' lililofanyika jijini Dar es Salaam, hivi karibuni, na kujumuisha wanawake zaidi ya elfu mbili kutoka nchini  ili kuonyesha shughuli wanazozifanya.

Juliana Nyanda kutoka asasi hiyo anasema sasa ujasiriamali wa wanawake sio ule mdogo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma kwa sababu zamani unaweza kusema kuwa hawakupata fursa ya kupata elimu ndio maana waliingia kwenye ujasiriamali lakini sasa wajasiriamali wengi ni watu waliopata elimu nzuri pia.

Asasi hiyo isiyokuwa ya kiserikali ya Purple Planet inawawezesha wanawake kupitia mitandao na kuwapa mafunzo,ushauri na muongozo wa kufanya kile wanachopenda kukifanya na wanafanikiwa .

Ili kujua zaidi kuhusu msaada wa Magreti kwa wanawake wengine, nilizungumza pia na Qeen Lema. Huyu ni mwanamke ambaye alivutiwa na dada Magreti, anaeleza kuwa yeye alikuwa ni mama wa nyumbani alikuwa hafanyi kazi yoyote. 


Hata hivyo, siku moja alibahatika kukutana na Magreti ambapo waliongea mengi na mwishowe aliamua kumtembelea kwake.

 Baada ya safari hiyo, alianza kufatilia namna Magreti anavyofanya kazi na ndipo akavutia zaidi.

 Kwa sasa Queen amejiajiri kwa kufuga kuu 400 wa nyama na ana imani atafanikiwa kama vile mwalimu wake alivyofanikiwa

UNA WOGA WA KUFANYA BIASHARA?

Wanawake wengi wamekuwa wana woga wa kuanzisha biashara yaani kujiajiri.  

Ni vyema wanawake wale ambao wameweza kufanikiwa katika biashara zao wakajitangaza zaidi na namna walivyopata mafanikio yao.

 Hii itawapa motisha wanawake wengine ambao wana woga waweze kutoka kwenye woga na kuanza kuchukua hatua.

Kwa upande mwingine, Eimu ya ujasiriamali itolee zaidi kwa wanawake ili wapate hamasa ya kujiajiri. Taasisi za kifedha kama vile benki, microfinance na mashirika mbalimbali watoe elimu na msaada zaid kwa wanawake kufanya ujasiriamali.



Baadhi ya kuku  anazozifuga  magreti

Pia maafisa biashara watoe elimu kwa wanawake katika kata, vitongoji na mitaa juu ya faida ya kufanya biashara, bila kusahau kuwaeleza maana halisi ya biashara ili wanapoaanza wasipate hasara kubwa itakayo wakatisha tama ya kufanya biashara.

 Kwa upande wake, Serikali ianzishe somo la biashara kuanzia ngazi darasala tano pale mtoto anapoanza kujielewa aweze kujua biashara ni nini.

 Hii itasaidia kuongeza ajira kwani mtoto anakuwa amejipanga tangu mdogo kuwa asipo ajiriwa serikalini ataenda kujiajiri mwenyewe.


  kwa mujibu wa takwimu za usawa wa kijinsia katika ajira zinaonyesha kwamba kufikia mwaka wa 2014 Watanzania  ambao  miongoni mwao walikuwa ni wanawake milioni 2.1 walikuwa wameajiriwa katika sekta rasmi , ikiwa ni pamoja na serekalini na sekta binafsi, kwa mujibu wa kituo cha taifa cha takwimu nchini 

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia