Huduma ya chakula cha mtaani ndiyo tegemeo la tabaka la kati la wafanyakazi wengi wanaofanya kazi katikati ya miji na kuishi katika maeneo yaliyo nje ya miji hiyo.
Asilimia kubwa ya biashara hii hufanywa katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu, katikati ya jiji, vituo vya usafiri ikiwa ni kinyume na utaratibu wa Serikali za Mitaa.
Serikali zimejaribu kuwahamishia mama na baba lishe hao katika masoko yenye miundombinu safi na salama zaidi lakini juhudi hizo hazizai matunda yanayotarajiwa kutokana na wafanyabiashara hao kurejea kule kule walikozoea kwa sababu ya biashara zao kuonekana kwa urahisi na kupata wateja.
Hatua za kuwaondoa kwa shuruti katika maeneo yao na kukamata vifaa vyao vya kazi inayosababisha kusimama kwa shughuli zao kwa muda mfupi na baadaye kurejea, kumewafanya kutokuwa tayari kuboresha vifaa vyao vya kazi jambo ambalo linaathiri usalama wa chakula.
Kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa mama lishe
Hadi sasa, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limetengeneza vioski 11 vya mfano ambavyo ni rafiki kwa mazingira ya wauzaji chakula na vyenye uwezo wa kuchukua kati ya watu wanane hadi 12.
Kwa kuwa sasa zaidi ya mama lishe 527 wanaendesha shughuli zao katika majiji ya Dar es Salaam na Dodoma, wamepatiwa mafunzo ya upangaji wa chakula, usimamizi wa biashara na kanuni za usalama wa chakula na usafi.
Aidha, vifaa vya jikoni (aproni na vyombo vya jikoni) 1,050 viligawiwa kwa mama lishe katika mikoa hiyo miwili ili kuboresha usalama wa vyakula vya mitaani.
FAO inatekeleza ajenda ya chakula mijini kupitia mradi wa Agri-Connect unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) ili kusaidia nchi katika kukabiliana na changamoto za mfumo wa kilimo wa chakula kama vile masuala ya usalama wa chakula na menyu zisizo na uwiano wa lishe.
Mpango huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa wizara zinazohusika na kilimo na afya, pamoja na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Dodoma (SIDO) na Serikali za mitaa za mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam.
Ili kuwezesha uuzaji na usafirishaji wa bidhaa za kilimo, mifugo, samaki, na vyakula vya mitaani, FAO itabuni na kuzindua programu tumishi ya simu ya Mfumo wa Upatikanaji na Ufikishaji Chakula (FLAS). Watanzania wataweza kupatiwa mapendekezo ya lishe bora kutokana na Miongozo ya Chakula na Ulaji (FBDGs).
Mwenyekiti wa Umoja wa Mama/Baba Lishe wilaya ya Temeke, Mariami Mtesa (kushoto) akimweleza Ofisa Mwandamizi kutoka Umoja wa Ulaya (EU) aina mbalimbali ya vyakula vya asili katika tamasha lililofanyika Dar es Salaam hivi karibuni.