Melami (34) ni mama mwenye mtoto mmoja anayeishi jijini Dar es Salaam anayeendesha familia yake kupitia biashara ya chakula pembezoni mwa barabara ya Sam Nujoma jijini humo.
Alifundishwa na mama yake kupika, lakini hakuwahi kuambiwa juu ya umuhimu wa usalama na usafi wa chakula.
Alitambua umuhimu wa hayo siku ambayo wateja wake walipolalamika kuugua matumbo kutokana na usalama mdogo unaotokana na uandaaji mbovu wa chakula baada ya kuhudhuria mafunzo yaliyoandaliwa na COUNSENUTH kwa niaba ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) juu ya elimu ya msingi ya lishe na usalama na usafi wa chakula kupitia Mradi wa Motisha kwa Baba na Mama Lishe Kuandaa Mlo Kamili na Salama.
“Kupitia mafunzo hayo niliweza kueleza changamoto nazozipatia na nikaomba nifikiriwe pale ninapohitaji msaada wa kuboresha biashara yangu,” alisema Melami.
Upimaji wa chakula
Kabla ya mradi, anasema alikuwa anaweka ugali au wali mwingi na mboga chache, lakini baada ya mafunzo ameweza kuwawekea wateja wakemachaguo mengi. “Badala ya kuwahudumia ugali au wali na maharage, sasa wanaweza kuchagua na aidha kuku, samaki au nyama,” anaeleza.
Uboreshaji wa mazingira ya biashara
Melami amefanya maboresho katika mazingira ya biashara yake. Alianza na kioski cha mbao na baadaye alipata hema linaloweza kuzuia jua kutoka kwa kampuni moja binafsi iliyompatia msaada.
Ndoto yake siku moja ni kumiliki mfano wa kibanda kinachosambazwa kupitia mradi wa pamoja wa FAO, Serikali na Umoja wa Ulaya (EU) wa Agri-Connect kwa mama na baba lishe.
"Kioski cha kuuza chakula cha mitaani kwa baba/mama lishe kinavutia kwa sababu kimechorwa picha za vyakula na pia kuna jumbe zinazoongoza uelewa wa jamii kuhusu lishe bora,” anaeleza.
Balozi wa lishe
Melami tangu hapo ameanza kubadilika kwa kuvaa apron safi, mtandio kichwani, viatu vya kutumbukiza, na kuweka kucha safi na fupi. Anatunza kumbukumbu ya matumizi na mauzo na kukokotoa faida baada ya kuondoa gharama za uendeshaji.
Sasa hivi ni balozi wa lishe ambaye anafundisha wateja wake juu ya mlo kamili, usalama wa chakula na usafi.
“Sasa hivi sipokei malalamiko ya mara kwa mara ya wateja, wateja wanaongezeka pamoja na mauzo yanazidi kupanda,” anasema Melami.