WANAWAKE WASIMAMIA VYEMA MAJUKUMU YA UONGOZI:

 


 

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

 

“ASILIMIA 77.77 ya wajumbe wa kamati ya shehia yangu ni wanawake na asilimia 22,22 tu ni wanaume na maendeleo yanaonekana’’, si maneno ya mtu mwengine bali ni ya sheha wa shehia ya Jadida Wete Juma Ali Juma.

 Kamati yake ina wajumbe tisa (9), wanawake saba na wanaume wawili (2), ambapo mwanzo alikuwa na kamati ya wajumbe 12, wanawake wawili na wanaume 10.

 Mwaka 2020 aliivunja kamati hiyo baada ya kuona maagizo anayoyatoa, hayafikiwi kama walivyoyapanga, jambo ambalo lilizorotesha maendeleo ya shehia.

 Mwaka 2019, alihudhuria mkutano ulioandaliwa na Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA)- Zanzibar, Gombani Chake Chake na kuelezwa kuwa wanawake wana haki sawa ya kuongoza kama walivyo wanaume.

 ‘’Mimi dhana hiyo niliijaribu kwenye shehia yangu na kweli sasa wanawake ndio ninaowategemea pale ninapotoa maagizo kwa ajili ya kuwafikishia wananachi,’’anasema.

 Anasema, hawajahi kufeli kwenye shehia yake, kwa kuwa na idadi kubwa ya wajumbe wanawake na anafikiria kupunguza tena idadi ya wajumbe wanaume.

 “Wajumbe wanaume ni wazito kufika kwa wakati kwenye vikao, pili fedha wameweka mbele, lakini hata unapowapa kazi, nao huwapa watu wengine wafanye, lakini kwa wanawake ni tofauti,’’anasema.



 Sio shehia ya Jadida pekee, ambayo masheha wanaume wamewaamini wajumbe wanawake, hata shehia ya Mtemani ina wajumbe 13, ikiwa na wanawake tisa, sawa asilimia 63.23 na wanaume wanne sawa na asilimia 30.76.

 Sheha wa shehia hiyo Mrisho Juma Mtwana anasema, sababu ya kuongeza idadi ya wanawake, ni baada ya kuona shehia ya Jadida inafanikiwa kikazi.

 ‘’Nilimfuata sheha mwenzangu wa Jadida, nikamuuliza siri ya mafanikio yao, akaniambia ni kuwapunguza wajumbe wanaume na kuongeza wanawake”, anasema.

 Kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2021, aliamua kuwapunguza wajumbe kutoka 15 wa zamani na kuwa 13, ambapo wanawake amewaweka tisa na wanaume wanne.

Tangu afanye mabadiliko hayo, sasa anafurahia utendajiwa kazi wao na hasa anafurahishwa zaidi, anapokuwa na mikutano ya jioni, jinsi wajumbe wake wanawake wanavyotumia mbinu ya kukusanya wananchi.

 ‘’Kama kuna sheha ana tatizo kwenye shehia yake, aangalie uwezekano wa kuwaweka wajumbe wengi wanawake kwenye kamati, anaweza kufanikwa kama nilivyo mimi’’, anasema.

 WAJUMBE WA SHEHIA HIZO

Wanasema, kamati ya sheha yenye wajumbe wengi wanaume imekuwa ikikosa ufanisi, kutokana na kuwaburuza wanawake hata kwa jambo lililo wazi.

 Asha Mussa Iddi na Maimuna Ali Khamis ambao ni wajumbe wa kamati ya shehia ya Jadida, wanasema licha ya kuwa sheha wao ni mwanamme, lakini wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa.

 ‘’Kwa mfano suala la utoro kwa wanafunzi, tulizungumza na wanawake wenzetu kwa kutumia lugha nzuri, walitufahamu na mwaka 2022 pekee wanafunzi 13 walirudi skuli’’, wanasema.

 Lakini hata wajumbe wa kamati ya shehia ya Mtemani Sauda Issa Haji na Asha Issa Ali, wanasema sheha amekuwa akiwaamini kutokana na kujituma kwao.

 ‘’Sisi sheha akitupa kazi huwa hailali, maana tunajiuliza, kwa nini wameachwa wanaume tena wasomi, nafasi hii tukapewa sisi, inabidi tufanye kazi kwa bidii’’, wanasema.



 Lakini mjumbe wa kamati hiyo Ali Makame Mkubwa anasema, licha ya kuwa idadi ya wajumbe wanawake ni kubwa, lakini ina mamtiki katika utendaji wa kazi zao.

 WANANCHI WA SHEHIA HIZO

Khadija Ussi Haji na mwenzake Asiya Sharif Hassan wa shehia ya Jadida na wenzao wa shehia za Mtemani, Nussra Mohamed Omar na Mtumwa Ilayas Kombo, wamesema kamati zao sasa ziko hai na zinafanya kazi vizuri.

 ‘’Inafurahisha, kwa mfano tunapokuwa na usafi wa shehia, hawa wajumbe wa shehia zetu ambao wengi ni wanawake, huwa ndio wa mwanzo, sasa na sisi tunahamasika’’, wanasema.

 Wanasema kama kuna tasisi mfano TAMWA ndio waliowaelimisha masheha wao na sasa kuwa na kamati zilizohai, baada ya kuingia wanawake kwa asilimia kubwa.

 ‘’Kumbe wanawake wanaweza, sasa lazima kuwe na sheria hasa iwalazimishe masheha, wajumbe wawe sawa kwa sawa kati ya wanawake na wanaume, maana matunda yanaonekana”, awanashauri.

 HALI HALISI YA WILAYA YA WETE KWA WAJUMBE WANAWAKE

Wilaya ya Wete, bado hali hairidhishi sana, maana kati ya wajumbe wote 359 kutoka shehia 36 wilayani humo, wajumbe wanawake ni 132 sawa na asilimia 36.76 huku wanaume wakiwa  227 kwa asilimia 63.23.

 Hili linaweza kuchangiwa kwa karibu na uhaba wa masheha wanawake kwenye wilaya hiyo, kwani wapo 10 tu sawa na asilimia 27.77 na wanaume ni 26 sawa na asilimia 72.22.

 MASHEHA WANAWAKE WILAYA YA WETE

Sheha wa shehia ya Mtambwe Kaskazini, Shufaa Asaa Muombwa, anasema anao wajumbe 11, lakini wote ni wanaume.

 ‘’Mara tatu nimeshachagua wajumbe saba wanawake, lakini wanazuiliwa na waume zao na wengine hukumbana na vitisho vya wananchi”, anasema.

 Ndio maana kuanzia mwaka 2021 mwishoni akamua kuwa na wajumbe 11 sawa na asilimia 100, kwani wote ni wanaume, ingawa anangalia namna na kuwa na wanawake hapo baadae.

 ‘’Napata shida ninapo wapa maagizo hawa wajumbe wangu, huwa wazito kuyatekeleza, inabidi wakati mwengine niingie na mimi, lakini kama wanawake wakiondolewa vikwazo, nitafanikiwa’’, anasema.

 Sheha wa shehia Bopwe Ramia Said Rashid, anasema kamati yake imeaundwa na wajumbe tisa, wanawake wakiwa watano sawa na asilimia 55.55 na wanaume ni wanne sawa na asilimia 44.44.

 ‘’Mimi nina nia ya kupunguza idadi ya wajumbe wanaume ili ufanisi uongezeke, maana zipo shehia kama za Mtemani na Jadida zinakwenda vizuri’’, anasema sheha.

 WANAHARAKATI WANASEMAJE?

Mwanaharakati wa haki za wanawake na watoto Tatu Abdalla Mselleh, anasema idadi ndogo ya wajumbe wanawake kwenye kamati za masheha, halina uhusiano na uhaba wa masheha wanawake.

 ‘’Wivu wa kupindukia, masheha kutowaamini wanawake, au mifumo ya utamaduni inaweza kuwa kichecheo kikubwa kwa wanawake kutopewa nafasi hizo au kuzikataa,’’anaseme.

 Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hya Mussa Said, anasema wapo wanawake hupewa nafasi za ujumbe wa sheha, lakini kutokana na vikwazo wanavyopewa, huzikataa nafasi hizo.

 ‘’Kwa mfano mwanzoni mwa mwaka 2022 yupo mwanamke alipewa usheha, lakini kwa vikwazo vya mume wake aliusamehe, sasa mfano kama huu huwakumba hata wajumbe wanawake wa kamati,’’ anasema.

 Sifuni Ali Haji kutoka Jumuiya mwevuli ya asasi za kiraia Pemba ‘PACSO’ anasema, bado wapo baadhi ya wanaume wamekuwa wakitumia vitisho kwa wanawake kuogopa kushika uongozi.

 ‘’Hata ukija kwenye vyama, ukiweka nia ya kugombea kama ubunge au uwakilishi, umeanza kujitengenezea maadui, hivyo hata huko kwenye wajumbe wa shehia, wanawake wanasumbuliwa,’’ anasema.

 Mohamed Hassan Ali, Mwenyekiti wa jumuiya za asasi za kiraia mkoa wa kaskazini Pemba, anasema bado baadhi ya viongozi wanaume hawajawaamini wanawake.

 ‘’Kwa mfano wilaya ya Wete ina shehia 36, lakini masheha wanawake ni 10, kwa nini hapa isiwe idadi sawa na Mkuu wa mkoa na katibu tawala wilaya wote wanawake’’, anahoji.

 VIONGOZI WA SERIKALI

Mkuu wa wilaya ya Wete Dk. Hamad Omar Bakari anasema, masheha hawafungwi na idadi ya wajumbe wa shehia kutokana na ukubwa wa shehia zao. 

‘’Sisi hataka kama watawachagua wanawake wote, hakuna tatizo muhimu mambo yaende, kama ambavyo maagizo yanakuja kila siku, maana wananchi wanachotaka ni kutekelezewa shida zao’’, anasema.

 Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib anasema, kubwa ni kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi na kisha kuzitendea haki. 

Akizungumza kwenye kongamano la kutimiza miaka miwili lililofanyika ukumbi wa zamani wa baraza la wawakilishi Wete, Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, alisema mawaziri wanawake wameongoza kwa kufanya vizuri.

 ‘’Na kwa siku sijazo nitaongeza idadi yao, katika nafasi mbali mbali za uongozi iwe mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa wilaya na mkoa’’, anasema.

Dk. Mwinyi kwa sasa, alishamteua Katibu mkuu kiongozi mwanake kwa mara ya kwanza, tangu Zanzibar ifanye Mapinduzi miaka 58 iliyopita.

 KATIBA

Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kwenye kifungu cha 21 (1) kimeeleza wazi kwamba, kila mzanzibari anayohaki ya kushirikia katika shughuli za utawala wa nchi.

 Kifugu hicho kikazidi kufafanua kuwa iwe ni moja kwa moja au kupitia wawakilishi waliochaguliwa kwa hiari, lakini wanawake wamekua wakikoseshwa haki hii, jambo ambalo sio sahihi.

 Hata Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kwenye Ibara 21, nayo imeeleza haki ya kila mtanzania kushiriki kwenye shughuli za utawala na pia suala la kuchagua na kuchaguliwa.

 Hapa utaona kwamba, wanachama wa vyama vya siasa wamekuwa wakiwang’ng’ania wanaume kama vile kuna kifungu ndani ya katiba za vyama vyao au ya nchi inayowalazimisha hivyo.

 ATHARI YAKE

Mwanaharakati wa haki za wanaweke, Dina Juma Makota kutoka Jumuiya ya PEGAO wanaotekeza mradi wa miaka minne wa kuwajengea uwezo wanawake kuadai haki, zao anasema ni kukosa kujiwakilisha.

 Ali Khamis Juma mwenye ulemavu wa viungo, anasema ikiwa wanawake hawamo kwenye kamati za shehia, shughuli za kimaendeleo zinazorota kwa kiwango kikubwa.

Sheha wa shehia ya Pembeni Saumu Ali Hamad anasema, wao hushindwa kuyatekeleza maagizo ya wilayani, kwani baadhi ya maeneo, wanaume hawafiki kutoa taarifa.

 Mjumbe wa kamati ya shehia ya Gando Hamisa Iddi Kassim anasema, masheha wanaweza kushindwa kwenye kazi zao, maana suati yao ina umuhimu wake kwenye vikao.

 NINI KIFANYIKE

Masheha wanasema, ili idadi ya wajumbe wanawake iongezeke kutoka ya sasa132, kati ya wajumbe 359 sambamba na kuendelea kutolewa elimu, ili uelewa uwe mpana kuhusu uongozi kwa wanawake.

 Masheha wanawake, wamesema kama wanaume watawafungulia minyororo wanawake na kuwaamini, idadi ya wajumbe kwenye kamati za masheha itaongezeka. Wajumbe wa shehia wanasema kama shehia nyingine zitajenga utamaduni wa kuzitembelea shehia zilizofanikiwa, idadi ya wajumbe wanawake itakua zaidi.

Mkuu wa wilaya ya Micheweni Mgeni Katib Yahya, anasema masheha waamue kuwatea wajumbe wanawake, wale wenye uwezo, ili wengine waige.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post