Ticker

6/recent/ticker-posts

NCHIMBI :LOWASA ALIKUWA MCHAPAKAZI WA KWELI

 Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Balozi Emmanuel John Nchimbi, amesema watu wanaweza kupishana katika maelezo ya kumwelezea Hayati Edward Ngoyai Lowassa katika mambo mbalimbali, lakini jambo moja ambalo haliwezi kubishaniwa ni jinsi alivyokuwa mchakapakazi wa kweli, katika nafasi zake zote alizowahi kuwa nazo, katika kuwatumikia Watanzania wote.



Dkt. Balozi Nchimbi amesema kupitia uhodari wake wa kuchapa kazi katika kutimiza wajibu wake kwa nchi, Hayati Lowassa alikuwa kiongozi mwenye uthubutu na uwezo wa kufanya maamuzi magumu kwa ajili ya kutafuta ufanisi na kupata matokeo chanya ya haraka kwa ajili ya maendeleo ya watu.


Dkt. Balozi Nchimbi amesema hayo leo Ijumaa, Februari 16, 2024 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kufika kuwapatia pole wafiwa, kusaini kitabu cha maombolezo na kutoa heshima za mwisho, nyumbani kwa Hayati Lowassa, katika Kijiji cha Ngarash, wilayani Monduli Mkoa wa Arusha, akiongeza kuwa kutokana na sifa za kiuongozi alizokuwa nazo, kifo cha kiongozi huyo ni pigo kubwa kwa nchi.


“Lowassa alikuwa mchapakazi kweli kweli. Alikuwa mtu wa maamuzi magumu. Watu wanaweza wakapishana katika kila maelezo wanayotoa kuhusu Lowassa lakini hakuna hata mtu mmoja anayeweza kuwa na ujasiri wa kusema alikuwa mvivu, au alikuwa hapendi kufanya kazi au hakuwa na mapenzi na nchi yake, hakuna. Alikuwa mchapakazi wa hali ya juu. Hakupoteza muda hata mara moja kuacha kufanya kazi kwa ajili ya Watanzania.


“Alikuwa mzalendo, mnyenyekevu na aliyependa watu wote bila kuwabagua. Moja ya uamuzi mgumu unaoendelea kukumbukwa ni hatua ya kiongozi huyo aliyoichukua ya kujiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008,” amesema Dkt. Nchimbi.


Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Nchimbi amesema taarifa za msiba huo wa Waziri Mkuu Mstaafu Lowassa, ilikuwa ni mojawapo ya habari mbaya kwake kuwahi kuzipata.


“Nimepoteza rafiki, kaka na mlezi. Lakini pia nimeona jinsi ambavyo chama changu kimepoteza mtu. Nimeona pia jinsi ambavyo nchi yetu imepoteza mtu. Nimeona jinsi ambavyo vyama vingine vilivyokuwa karibu naye vimepoteza mtu muhimu kwao. Pigo hili nililihisi binafsi na niliona ambavyo linaathiri nchi yetu. Ni pigo kubwa sana kwa nchi yetu,” amesema Dkt. Nchimbi.


Akisisitiza namna ambavyo Hayati Lowassa anapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika jamii, Dkt. Nchimbi amemwelezea jinsi alivyokuwa na haiba ya kuchangamana na watu katika jamii, akijenga urafiki na watu mbalimbali bila kubagua hadhi au hali ya mtu, hivyo viongozi wanapaswa kujifunza kupitia kiongozi huyo kuishi maisha ya uadilifu na unyenyekevu na kuwa tayari kuwatumikia watu wote bila ubaguzi.


“Alikuwa mnyenyekevu sana, kwa nafasi alizoshika, aina ya marafiki aliokuwa nao…alikuwa na marafiki ambao haangalii nafasi zao, vyeo vyao na hata katika eneo hili tulilopo (kijijini kwao Lowassa), wako watu wametoka mikoa mbalimbali nchini, watu wa kawaida kabisa ambao walikuwa marafiki wa Lowassa,” amesema Dkt. Nchimbi.


Hayati Lowassa, ambaye aliwahi kushika nafasi mbalimbali katika Chama Cha Mapinduzi na Serikali, ikiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyefariki dunia Februari 10, mwaka huu, anatarajiwa kuzikwa huko Monduli, Jumamosi, Februari 17, 2020, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kudhuria na kuongoza maelfu ya waombolezaji waliotoka maeneo mbalimbali ya nchi na nje ya nchi, kumuaga na kumsindikiza kiongozi huyo katika safari yake ya mwisho duniani.

Post a Comment

0 Comments