ARUSHA YAADHIZIMISHA SIKU YA USAFI WA MAZINGIRA KWA ZOEZI LA USAFI JIJINI
Na Woinde Shizza Arusha
Wananchi pamoja na viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha wamejitokeza kwa wingi kushiriki zoezi la usafi katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Usafi wa Mazingira Duniani, yanayoadhimishwa kila Septemba 20.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa zoezi hilo, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Kayombo, alisema maadhimisho ya mwaka huu yamelenga kuzipa taka thamani kwa kuzirejeleza na kuzitumia upya badala ya kuzitupa.
“Tunataka twende kwenye lengo la kuhakikisha kwamba si kila kitu kinatupwa. Karatasi, maboksi, plastiki, chupa zote zinaweza kurejerezwa na kutumika tena. Hii ndiyo dhana kuu ya maadhimisho ya siku hii ya kimataifa,” alisema Kayombo.
Zoezi la usafi lilianzia Mianzini na kuishia soko la stendi kuu ya mabasi ya jiji hilo, huku wananchi na viongozi wakiwa bega kwa bega katika kuondoa taka. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Arusha nayo ilishiriki kwa kusafisha soko la Ngaramtoni.
Hata nje ya maadhimisho haya, jiji la Arusha limejiwekea utaratibu wa kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, hatua inayotajwa kupendezesha mandhari ya jiji hilo maarufu kwa vivutio vya utalii.
Waandishi wa Nukta Habari walipita katika maeneo ya pembezoni mwa jiji ikiwemo soko la Kilombero, Mbauda na Morombo na kushuhudia hali ya usafi huku wananchi wakiendelea kufanya usafi.
Baadhi ya wananchi walioshiriki katika zoezi hilo walisema kuwa utaratibu huo unapaswa kuendelezwa ili jiji libaki safi kila wakati.
“Nashukuru zoezi limeenda vizuri, hakuna changamoto yoyote. Naona zoezi hili liendelee kwa sababu linaacha mazingira yetu safi,” alisema Zaina Bakari.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Debora Manase, aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kusafisha jiji, huku akisisitiza umuhimu wa kuzipa taka thamani ili kulinda afya za wakazi wa jiji.

0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia