MAADILI YA KI-AFRIKA YAHIMIZWA, WAZAZI WATAKIWA KUWAELIMISHA WATOTO
Na Woinde Shizza,Arusha
Mkurugenzi
wa Tanzania Platforms Network, Edward Malecela, amewataka wazazi nchini
kutoacha jukumu la kuwaelimisha watoto wao kuhusu maadili ya Kiafrika
na madhara ya tabia zisizo sahihi zinazoletwa na utandawazi kupitia simu
na mitandao ya kijamii.
Akizungumza
kwenye mahafali ya darasa la saba katika shule ya Oola Pre and Primary
School iliyopo kata ya Esilale, wilayani Monduli, Malecela alisema
wazazi hawapaswi kuogopa kuwaeleza ukweli watoto wao kwa hofu ya mila za
zamani.
“Kwa mfano baba
anaweza kumshauri binti yake, vivyo hivyo mama akamshauri mtoto wa
kiume. Ni lazima wazazi tuwe wazi, tuwafundishe watoto maadili pasipo
kuwaficha ili wajue faida na hasara za mambo wanayokutana nayo,” alisema
Malecela.
Aliongeza kuwa
mbali na kutoa elimu ya maadili, taasisi yake pia inajihusisha na
ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kutoka familia za kifugaji, kutoa elimu
juu ya mazingira, haki za binadamu na afya ya uzazi. Pia, alisema
taasisi hiyo inashirikiana na volunteers kutoka mataifa mbalimbali
wanaosaidia katika masuala ya kijamii, afya na magonjwa yasiyoambukizwa
kama kisukari na saratani.
Alisisitiza umuhimu wa elimu ya ujasiriamali na haki za wanawake wakati wa semina maalumu kwa kina mama iliyofanyika sambamba na mahafali ya darasa la saba katika shule ya Mchipuo wa Kiingereza, Oola Pre and Primary School, iliyopo kata ya Esilale, wilayani Monduli.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa shule hiyo, Samweli Oola, alisema shule hiyo
imehitimisha darasa la saba kwa mara ya saba tangu ianzishwe, ambapo
jumla ya wanafunzi 49 wamehitimu mwaka huu.
Alibainisha
kuwa shule hiyo imekuwa ikiwasaidia wazazi wa jamii ya kifugaji kwa ada
nafuu, ikiwemo mfumo wa kulipia kwa mifugo au mazao.
“Tunawaalika
wazazi kuwaleta watoto wao hapa. Hawatajutia, maana tunafundisha elimu
bora na maadili mema ya Kiafrika yatakayowasaidia katika maisha yao ya
baadaye,” alisema Oola.
Mmoja
wa wahitimu, Methew Laisheri, alieleza shukrani zake akisema awali
aliacha shule kwa ajili ya kufuga mifugo, lakini ushawishi wa walimu
ulimrudisha shuleni na sasa amehitimu akiahidi kuendelea na masomo
zaidi.
Mgeni rasmi katika
mahafali hayo, mgombea ubunge wa Monduli, Joseph Isack maarufu
‘Kadogoo’, aliwapongeza walimu na uongozi wa shule hiyo kwa kutoa elimu
bora, huku akiahidi kuwa mlezi wa shule hiyo.
Aliwataka
wananchi kuendelea kuiombea nchi kipindi cha kampeni na kujitokeza kwa
wingi kupiga kura Oktoba 29, ili uchaguzi uwe wa amani na utulivu.








0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia