ST. PADREPIO GIRLS YAFANYA MAHAFALI YA PILI, YASISITIZA MAADILI NA IMANI KWA MUNGU
Na Woinde Shizza, Arusha
Shule ya Sekondari ya Wasichana ya St. Padrepio Girls imefanya mahafali yake ya pili ambapo jumla ya wanafunzi 59 wamehitimu masomo, huku viongozi wa shule hiyo na wageni waalikwa wakisisitiza malezi bora, maadili mema na kumcha Mungu kama msingi wa mafanikio ya watoto.
Akizungumza katika mahafali hayo, Mkuu wa Shirika la Dada Wadogo wa Mtakatifu Francis, Sr. Bridget Kokiambo, alisema shirika hilo linapokea watoto bila kujali wanatoka wapi na linawalea kwa kuzingatia maadili, usafi, upendo wa mazingira ya shule na kumcha Mungu.
“Tunawafundisha watoto kuishika sala na kuelewa kuwa sala ni kila kitu ,Maisha hayafanikiwi bila kumuweka Mungu mbele, Tunashirikiana na wazazi kuhakikisha watoto wanakua katika maadili 5 na tunawachukulia kama watoto wetu bila kujali uwezo wa kifedha wa mzazi,” alisema Sr. Kokiambo.
Aliongeza kuwa shirika hilo linawalea watoto kisaikolojia, kiakili na kiroho kwa lengo la kuwajenga wawe watu kamili ,Alisisitiza kuwa mtoto anayelelewa kwa maadili na nidhamu hawezi kushindwa kwenye masomo na maisha kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari St. Padrepio Girls, Sr. Juliana Kwangu, alisema maandalizi ya mahafali hayo yanaonyesha mshikamano mkubwa kati ya walimu, wazazi na wanafunzi, akieleza kuwa wamejitahidi kuwafundisha wanafunzi kimaadili na kitaaluma ili wawe na matokeo bora.
“Walimu wetu wanajituma na kuwapenda wanafunzi ,Tunaamini watafanya vizuri kwenye mitihani yao ,tunawaomba wazazi kushirikiana nasi kwa kuwa maadili mema yanatokana na mshikamano wa ‘mafiga matatu’,mwalimu, mzazi na jamii,” alisema Sr. Juliana.
Aliwataka wazazi kuwa na muda wa kufuatilia mwenendo wa watoto wao, kujua wanafanya nini na wako na nani, akisema malezi mazuri yanajenga taifa lenye maadili bora.
Mgeni rasmi wa mahafali hayo, Josephine Bitesigine kutoka Hospitali ya ALMC, aliwataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawalea watoto katika misingi ya maadili mema ili kuzuia mmomonyoko wa maadili unaoikabili jamii.
“Mmomonyoko wa maadili ni changamoto kubwa ,tunapaswa kuwafundisha watoto maadili mema na kuwaombea daima, Malezi bora ni jukumu la kila mmoja wetu,” alisema Bitesigine.
Mahafali hayo yaliambatana na burudani mbalimbali za wanafunzi pamoja na kupongezwa kwa walimu kwa mchango wao kati
ka mafanikio ya shule.



0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia