BENO MALISA AFUNGUA MAONYESHO YA KUSINI FESTIVE


 


Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, amefungua rasmi Maonyesho ya Kusini Festive, akiwataka wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji kuyatumia kama fursa ya kujitangaza, kujifunza na kukuza uchumi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Beno Malisa alisema maonyesho hayo yamekusanya wadau mbalimbali wa biashara, kilimo, ufugaji na teknolojia kutoka ndani na nje ya nchi, hivyo ni jukwaa la kipekee la kubadilishana uzoefu na kujenga mtandao wa kibiashara.

“Maonyesho haya yanasaidia kuibua fursa mpya za uwekezaji, kuongeza thamani ya bidhaa zetu na kutangaza vivutio vya utalii vya Nyanda za Juu Kusini,” alisema Malisa.

Kwa upande wake, Katibu wa Maonyesho hayo alisema kuwa nia ya maonyesho haya ni kuunganisha wazalishaji, wafanyabiashara, wawekezaji na watumiaji wa bidhaa na huduma kwa pamoja, ili kuongeza tija na ubora wa uzalishaji, kufungua masoko mapya na kukuza kipato cha wananchi.

Aidha, aliongeza kuwa maonyesho hayo yameandaliwa kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi juu ya mbinu bora za uzalishaji na matumizi ya teknolojia za kisasa katika kilimo, ufugaji na biashara.


Miongoni mwa taasisi na kampuni zilizoshiriki maonyesho hayo ni Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Benki ya CRDB, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), mashirika ya kilimo kama TARI, pamoja na kampuni binafsi za mbolea na zana za kilimo.

Mmoja wa wananchi aliyeshiriki maonyesho hayo alisema kuwa tangu yalipoanza kufanyika, yamechangia kwa kiasi kikubwa kuinua uchumi wa Wilaya ya Kyela, hususan Kata ya Matema Beach, ambako wageni na watalii wamekuwa wakifika kwa wingi na kuchochea biashara za wenyeji.

Mfanyabiashara wa eneo la Matema Beach, Bi. Neema Mwakyusa, alisema maonyesho hayo yameongeza mahitaji ya huduma za malazi, chakula na usafiri, na hivyo kuongeza kipato cha wajasiriamali wadogo.

“Kwa sasa hoteli zetu zinajaa, tunauza chakula kwa wingi na hata vijana wa bodaboda wamepata wateja wengi zaidi. Haya maonyesho yameleta neema kubwa kwa Matema,” alisema  Neema.

Aidha Kampuni ya Kibo Seed imeendelea kuonyesha dhamira yake ya kuunga mkono wakulima baada ya kushiriki kikamilifu katika Maonesho hayo ambapo , Afisa Kilimo wa Kibo Seed, Elia Titus, alisema kampuni hiyo inalenga kuwaelimisha wakulima kuhusu matumizi ya mbegu bora zenye tija ili kuongeza uzalishaji na kipato cha mkulima.

“Tupo hapa kuhakikisha wakulima wanapata elimu ya kutosha kuhusu aina bora za mbegu, mbinu za kilimo cha kisasa na namna ya kuongeza mavuno. Tunataka kuona wakulima wakipata matokeo bora na kuboresha maisha yao,” alisema Titus.



Aidha, Titus aliwahimiza wakulima wa kanda ya kusini kutumia fursa ya maonesho hayo kutembelea banda la Kibo Seed na kupata ushauri wa kitaalam pamoja na bidhaa mpya zinazofaa kwa hali ya hewa ya mikoa ya Mbeya, Njombe, Ruvuma na Songwe.

Maonesho ya Biashara ya Kanda ya Kusini yanatarajiwa kuendelea kwa muda wa wiki moja, yakihusisha makampuni na taasisi mbalimbali za umma na binafsi zinazotoa huduma na bidhaa kwa sekta ya kilimo na biashara.

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia