JOHN TANAKI AHAMASISHA WANANCHI KUPIGA KURA KWA AJILI YA MAENDELEO
Na Mwandishi Wetu, Arusha
John Tanaki, aliyewahi kuwa mtia Nia wa ubunge Jimbo la Arumeru Magharibi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), amewahimiza wananchi wa kata ya Kiranyi kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya 29 Oktoba mwaka huu.
Aliyasema haya wakati wa uzinduzi wa kampeni za udiwani wa CCM katika kata hiyo ambapo alisema kuwa kila raia ana haki ya msingi ya kuchagua viongozi wake, na kwamba kushindwa kushiriki katika zoezi la uchaguzi ni kupoteza haki hiyo muhimu.
“Kura yenu ni haki yenu ya msingi, msikubali kuiacha, kwa sababu mnapoteza nafasi ya kuamua mustakabali wenu,” alisema Tanaki, akisisitiza kuwa uchaguzi ni fursa ya wananchi kuamua hatima yao na maendeleo ya jamii.
Aidha, Tanaki aliwasihi wananchi kupiga kura kwa wagombea wa CCM, ikiwemo Rais, wabunge na madiwani, kwa lengo la kuleta maendeleo katika kata na taifa kwa ujumla.
Aliongeza kuwa kulinda amani ni jukumu la kila raia Aliwaeleza wananchi kwamba ukosefu wa amani unasababisha wafanyakazi kushindwa kufanya kazi zao, wafanyabiashara kuathirika, na wananchi wenyewe kutateseka.
Mgombea huyo pia alibainisha umuhimu wa kulinda amani iliyowekwa na muasisi wa taifa, hayati Mwalimu Julius K. Nyerere, akisisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo endelevu.
Alisisitiza kwamba kipindi cha uchaguzi ni wakati wa mshikamano wa wananchi, kuchagua viongozi watakaodumisha amani na kuendeleza maendeleo, na kuondoa migawanyiko ya kisiasa na kijamii.
Tanaki alimalizia kwa kuhimiza mshikamano wa kitaifa na mshikamano wa kisiasa katika kata ya Kiranyi, akisisitiza kuwa mshikamano huo unaweza kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi na kuchagua viongozi watakaoweza kuleta maendeleo endelevu.

0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia