ST. JUDE THADEUS SCHOOL ACADEMY YAFANYA MAHAFALI, YAPONGEZWA KWA UFAULU WA JUU



Na Woinde Shizza , Arusha

Shule ya ST. Jude Thadeus School Academy imefanya mahafali ya sita kwa darasa la awali na mahafali ya tatu kwa darasa la saba tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018 ikiwa na wanafunzi 12, na sasa ikiwa na jumla ya wanafunzi 481.

Akizungumza katika mahafali hayo, Mkuu wa shule hiyo, Balthazar Lasway, alisema shule imepata mafanikio makubwa kitaaluma ambapo kwa mara ya kwanza mwaka 2023 darasa la saba lilitoa matokeo bora yenye alama A-12 na B-6, na wastani wa ufaulu ukiwa A.

Aidha, Lasway aliwataka wazazi kuendelea kuwapeleka watoto wao shuleni hapo kutokana na ubora wa elimu na kiwango kizuri cha ufaulu kinachotolewa, huku akitaja changamoto zinazowakabili ikiwemo upungufu wa kompyuta kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi kufuatana na kasi ya sayansi na teknolojia duniani, pamoja na baadhi ya wazazi kushindwa kufuatilia maendeleo ya watoto wao kitaaluma na kimalezi.

Mkuu huyo pia aliwaasa wahitimu kuwa mabalozi wazuri wa shule popote waendapo, wakiepuka makundi hatarishi yanayoweza kuwasababisha kupotoka kitabia, ikiwemo utumiaji wa video zisizofaa, dawa za kulevya na mahusiano ya mapema ambayo huathiri maisha na afya zao.




Kwa upande wake, mgeni rasmi wa mahafali hayo, Afisa Utalii wa Hifadhi ya Ziwa Manyara, James Nahonya, aliwapongeza wahitimu 28 (wavulana 15 na wasichana 13) kwa kukamilisha masomo yao ya msingi.

Alisisitiza umuhimu wa kuendelea na masomo kwa bidii, akibainisha kuwa elimu ndiyo silaha ya maisha, huku akiwataka wanafunzi kuendelea kulinda na kuishi kwa maadili mema waliyojengewa na walimu wao, sambamba na kumwamini Mungu katika kila hatua ya maisha.

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia