NABII MKUU ATOA MCHANGO WA MILIONI 50 KWA MAPOKEZI YA RAIS SAMIA


Na Woinde Shizza, Arusha 

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, amemualika Nabii Mkuu, Mhe. Dkt. GeorDavie kushiriki katika mapokezi ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, atakayezuru mkoa huo kuanzia Oktoba 2, 2025.

Nabii Mkuu alipokea mwaliko huo kwa heshima kubwa na kumpongeza Rais Samia kwa uongozi wake unaoendelea kuleta matumaini kwa Watanzania, huku akisisitiza mshikamano wa kitaifa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.



Katika hatua hiyo, Dkt. GeorDavie alitoa mchango wa shilingi milioni 50 kwa ajili ya maandalizi ya mapokezi ya Rais Samia, akieleza kuwa mchango huo ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za chama na serikali katika kuimarisha umoja wa kitaifa



Akizungumza baada ya kupokea mchango huo kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Ndugu Musa Matoroka, aliushukuru uongozi wa kanisa la Nabii Mkuu na kusisitiza kuwa msaada huo ni kielelezo cha mshikamano baina ya dini na siasa.

Matoroka alibainisha kuwa mchango huo utasaidia maandalizi ya mapokezi ya Rais Samia, hususan kuhakikisha wananchi wanashiriki kwa wingi na kwa utaratibu mzuri, jambo litakalowezesha mkoa wa Arusha kuonyesha mshikamano wake kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa.

Kwa upande wake, Nabii Mkuu alimkaribisha Rais Samia kwa mikono miwili mkoani Arusha na kumtakia heri katika kampeni zake zinazoendelea katika mikoa mbalimbali, akibainisha kuwa viongozi wa dini wana wajibu wa kusali na kuliombea taifa wakati huu wa uchaguzi.

Makala alisema maandalizi ya mapokezi hayo yamekamilika na kuwataka wananchi wa Arusha kujitokeza kwa wingi kumpokea Rais Samia, ambaye mbali na shughuli za chama pia atazungumza na wananchi kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Ziara ya Rais Samia mkoani Arusha inatarajiwa kuvuta hisia za wananchi wengi, huku viongozi wa kisiasa, dini na jamii wakishiriki kwa pamoja kumpokea kiongozi huyo ambaye pia ni mgombea urais wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao.


About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia