WABUNGE WA EALA WATEMBELEA NAMANGA, WASIKILIZA KERO ZA MADEREVA NA WAJASIRIAMALI

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Veronica Nduva akitoa maelekeo wakati alipotembelea eneo la maegesho ya magari makubwa ya mizigo linapojegwa wakati wa ziara hiyo
Na Woinde Shizza , Arusha
Ziara ya wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) katika mpaka wa Namanga imekuwa fursa ya kusikiliza kero za wananchi, ikiwemo madereva wa malori na wajasiriamali wadogo wanaofanya biashara katika eneo hilo.
Wabunge hao, wakiwa wameambatana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Veronica Nduva, walisema lengo la ziara yao lilikuwa kuona kwa macho changamoto zinazokwamisha biashara na usafirishaji mpakani, na kusikiliza maoni ya wananchi wanaoishi na kufanya shughuli zao katika eneo hilo.
Madereva wa malori walieleza changamoto wanazopitia zikiwemo ucheleweshaji wa vibali, ukosefu wa huduma za msingi katika maeneo ya maegesho na tozo kubwa ambapo Eliya Mnyuka, dereva mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 10, alisema wanalazimika kuegesha magari kwenye maeneo yasiyo salama bila maji wala vyoo huku wakitozwa shilingi 15,000 kwa maegesho yasiyo na huduma.
“Wakati mwingine tunakaa siku tatu hadi wiki nzima tukijisaidia vichakani huku maofisa wa forodha wakitoa visingizio kama mtandao upo chini hivyo kupeleka kufeli Hali hii inaleta usumbufu na gharama zisizokuwa za lazima,” alisema Mnyuka.
Joseph Mgavano, dereva kutoka Iringa, aliongeza kuwa ukaguzi wa magari na namba za chasis unaochukua muda mrefu unachelewesha safari na kuathiri biashara. ,alishauri magari yasiyo na mizigo yaruhusiwe kupita muda wote bila kikomo cha muda wa usiku.
Wajasiriamali wadogo nao walieleza matatizo yao. Sing’ati Paulo, muuzaji wa shanga na vito vya asili, alisema mtaji mdogo na ukosefu wa soko ni changamoto kubwa, huku Joyce Kabati akiomba serikali kuwapatia maeneo bora ya kufanyia biashara na mitaji nafuu ili kunufaika na wageni wanaopita Namanga.
Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva, alisema serikali za nchi wanachama zina wajibu wa kuondoa vikwazo visivyo na tija vinavyokwamisha biashara na usafirishaji, akisisitiza umuhimu wa kuboresha mazingira ya sekta hizo kwa maendeleo ya uchumi wa Jumuiya.
Ray James, Afisa Biashara wa Longido, alibainisha kuwa maegesho ya sasa ni ya dharura kwani maegesho ya zamani ambayo ni Kimokoa yako kwenye ukarabati na yatakapokamilika yataweza kuhudumia zaidi ya malori 200 na kutoa huduma zote muhimu.
Ziara hiyo ilimalizika kwa wabunge wa EALA kushiriki maadhimisho ya Siku ya Wanawake, ambapo waligawa taulo za kike kwa wanafunzi wa shule jirani kama sehemu ya kuhamasisha afya na elimu kwa watoto wa kike.
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia