MABEYO AWATAKA VIONGOZI WA NGORONGORO KUIMARISHA UTALII NA UHIFADHI
Na Woinde Shizza,Arusha
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Jenerali mstaafu Venance Mabeyo, amewataka viongozi wapya wa mamlaka hiyo kuongeza ushirikiano na menejimenti katika kuboresha huduma za utalii, uhifadhi na maendeleo ya jamii ili kukuza uchumi wa taifa.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuwapandisha vyeo makamishna wasaidizi waandamizi wa hifadhi hiyo, Mabeyo aliwataka viongozi hao kuwa wachapakazi, waadilifu na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Viongozi waliopandishwa vyeo ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi Brown O. Shimwela, anayeongoza Idara ya Fedha, na Kamishna Msaidizi Mwandamizi Dkt. Amani Makota, anayesimamia Idara ya TEHAMA na Takwimu, ambao walihitimu mafunzo maalum ya Jeshi la Uhifadhi.
Mabeyo alisema kuwa ushirikiano kati ya viongozi hao wapya na menejimenti ya Ngorongoro ni muhimu katika kuboresha miundombinu ya utalii, kuongeza ubunifu wa huduma kwa wageni na kuibua mazao mapya ya utalii yatakayoongeza mapato ya taifa.
“Ni lazima tuboreshe huduma kwa wageni, ikiwemo miundombinu, vivutio vya malikale na hifadhi, pamoja na kutumia TEHAMA kuimarisha mifumo ya usimamizi na takwimu kwa maendeleo endelevu ya taifa letu,” alisema Mabeyo.
Alisema kuwa hatua hiyo ya kuimarisha menejimenti ya NCAA ni ishara njema ya mageuzi endelevu katika uhifadhi, kwani inaendana na dira ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan
Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Abdul-Razaq Badru, alisema makamishna hao wapya wataongeza nguvu kazi katika utekelezaji wa majukumu ya mamlaka, ikiwemo kusimamia uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii kwa ufanisi zaidi.
Badru aliongeza kuwa sekta ya utalii ni kinara katika kuchangia pato la taifa, hivyo mamlaka hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa utalii kuibua na kutangaza mazao mapya yatakayovutia watalii wengi zaidi ndani na nje ya nchi.
Aidha, alisisitiza kuwa NCAA itaendelea kuimarisha ushirikiano na jamii zinazozunguka hifadhi katika kuhakikisha uhifadhi unakwenda sambamba na maendeleo ya wananchi, hususani katika nyanja za elimu, afya na uchumi wa jamii.
Kwa upande wake mmoja wa kamishina alietunukiwa cheo Amani Makota ambaye ni mkuu wa kitengo cha Tehama Katika hifadhi ya Mamlaka ya ngorongoro alisema kuwa wanahakikisha wanaboresha mifuko ya taasisi hiyo ,na watatoa taarifa muhimu sahihi na kwa wakati ili kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi.
About Woinde Shizza





0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia