AICC HOSPITAL KUPIMA KISUKARI BURE
Kituo cha Kimataifa cha
Mikutano cha Arusha kupitia hospitali yake ya AICC kitaendesha kampeni ya
kupima kisukari bure kwa wakazi wa Arusha ili kusaidia wananchi kutambua kama
wana ugonjwa wa kisukari au wapo katika hatari ya kuugua ugonjwa huo.
Kampeni hiyo itafanyika
kesho (terehe 26-07-2012) katika hopitali ya AICC iliyopo jijini Arusha ambapo
madaktari wa hospitali ya AICC kwa kushirikiana na madaktari wa wanaohudhuria
mkutano wa Shirikisho la Madaktari wa Kimataifa pamoja na madaktari kutoka
Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania wataendesha zoezi la upimaji huo.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa
AICC, Bwana Elishilia Kaaya, amesema kuwa mbali na kupima kisukari, madaktari hao
pia watatoa ushauri wa namna bora ya kuishi na jinsi ya kuzuia madhara ya
kisukari kwa wale watakao kuwa wamekutwa na ugonjwa huo.
“Hospitali ya AICC inatambua umuhimu wa afya
za wakazi wa Arusha na Watanzania kwa ujumla na ndio maana tumeona ni vema
kufanya kampeni hii ya kupima kisukari. Napenda kutumia fursa hii kuwaalika
wakazi wote wa Arusha na vitongoji nyake kufika kwa wingi kwani mbali na kupima
pia itatolewa elimu na ushauri kutoka kwa wataalamu hao.” alieleza Kaaya.
Kwa mujibu Mkurugenzi
Mwendeshaji, upimaji huo utaenda sambamba na mkutano wa kwanza wa Shirikisho la
Madaktari wa Kisukari wa Kimataifa ambao kwa mara ya kwanza unafanyika hapa
nchini. Mkutano huo utafanyika katika kituo cha AICC ambapo madaktari
wanaohudhuria mkutano huo na wale kutoka Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania
watatoa huduma ya upimaji katika zoezi hilo.
“Tunaamini baada ya kampeni
hii wananchi watakuwa wamepata ufahamu juu ya hali ya afya zao na kutumia vema
ushauri wa madaktari kwa ajili ya kujikinga na kuzua athari za ugonjwa huo”,
alielezea Kaaya.
Mbali na kuendesha kampeni
hii, hospitali ya AICC imeanzisha kitengo maalumu cha kisukari ambapo kila wiki
madaktari hutoa huduma za matibabu na ushauri kwa wagonjwa wa kisukri.
Ugonjwa wa kisukari
umekuwa ukiongezeka kwa kasi duniani ambapo taarifa za Shirika la Afrya Duniani
(WHO) zinaonesha kuwa hadi kufikia mwaka 2011 watu milioni 366 walikuwa
wanaugua ugonjwa wa kisukari na mwaka 2030 idadi inakadiriwa kufika milioni
552. Barani Afrika watu milioni 14 na nusu wanaugua ugonjwa huo huku idadi
ikitarajiwa kufika milioni 28 mwaka 2030 ikiwa ni ongezeko la asilimia 90.

0 Comments:
إرسال تعليق
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia