Nyerere afariki, nakumbuka wakati mwili wake ulipoteremshwa kutoka kwenye ndege maalumu kutoka Uingereza tarehe 14 Oktoba 1999, wananchi wa rika zote waliokuwa wamekusanyika katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es Salaam ambao sasa unaitwa 'Mwalimu Nyerere International Airport", walionekana kugubikwa kwa simanzi kubwa na wengi wao walishindwa kujizuia, walibubujikwa na machozi kwa uchungu.
Nakumbuka pia msafara ulivyokuwa mrefu, siyo wa magari tu yaliyofika hapo uwanjani, bali halaiki ya wananchi ambao waliamua kuufukuza msafara uliokuwa na mwili wa mpendwa wetu Mwalimu Nyerere ambaye sasa ametuachia historia isiyoweza kufutika akilini mwa wengi.
Mwisho wa yote mwili ulifika nyumbani kwake maeneo ya Msasani kabla ya kuuweka kwenye uwanja wa Taifa kwa ajili ya kila aliyekuwa na nafasi kwenda kuuaga.
Msiba wa Mwalimu Nyerere ilikuwa kama muujiza, ingawa kila mtu alijua binadamu wote lazima wafikie muda wa uhai kukoma, kwa kifo cha Mwalimu, wengi walipatwa na butwaa, wakashangaa, wengine wakazirai wakijua kwa dhahiri kuwa kinara na mwokozi wa wanyonge hatakuwepo tena.
Misiba inatokea karibu kila siku, si wote wanaofariki wanawagusa jamii kubwa ya wananchi, lakini kifo cha Mwalimu kiliwagusa wengi kuanzia mijini hadi vijijini, jina la Nyerere ni ishara ya ukombozi na mfano wa amani na utulivu ambao nchi hii imekuwa mfano kwa mataifa mengi duniani.
Kutokana na ukubwa wa nchi hii, baadhi ya wananchi walioko katika vitongoji mbalimbali vya nchi hii, na hasa wale wazee waliovuta miaka mingi ya kuishi, bado wanaamini kuwa Nyerere yupo na anaendelea kuongoza.
Hilo linawezekana kuwa ni kutokana na kukosa mwamko wa kutaka kujua nini kinatokea katika dunia ya utandawazi uliopo.
Nia yangu si kuelezea wasifu wa Mwalimu Nyerere, nia ni kutaka kujua kama ni kwa kiasi gani Watanzania wa sasa wanaelewa nadharia yake katika uongozi wake wa zaidi ya miaka ishirini akiwa Rais wa Tanzania.
Nadharia ambayo imeandikwa katika kumbukumbu yake ndani ya vitabu vingi, inayotafsiri maisha ya wananchi tangu kabla ya Uhuru kupatikana wakati wa utawala wa chama kimoja na baadaye hadi kuingia katika mfumo huu wa vyama vingi.
Yapo maeneo mengi ambayo tayari yamekiukwa, ambayo Mwalimu Nyerere aliyapiga vita kwa bidii zote. Suala la rushwa ni moja ya vipaumbele ambavyo Mwalimu aliviwekea mikakati ya kutokomeza, na akaagiza kwa msisitizo kuwa nchi inayoongozwa kwa sera za rushwa, ni nchi isiyofuata utawala bora na wa kidemokrasia.
Na akatoa wito kwa taasisi zote kukemea na kupambana kwa nguvu zote vitendo vya rushwa, akisema hakuna mahali duniani ambapo haki itatendeka wakati wananchi wake wananunua haki zao za msingi kutokana na kukithiri kwa rushwa.
Inasikitisha sana kuona baadhi ya viongozi wanaotegemewa kuwa wapambanaji wa rushwa, wao wenyewe sasa ni watuhumiwa wakubwa wa masuala ya rushwa. Wapo waheshimiwa wabunge ambao walituhumiwa kujihusisha na rushwa na ambapo Spika wa Bunge Bi. Anne Makinda alilazimika kuchukua hatua ya kuunda tume ya kuchunguza tuhuma za waheshimiwa hao.
Mwalimu alitoa miongozo ya namna ya kupata viongozi bora, alikemea sana kuwa na michakato ya kuwapata viongozi kwa njia ya kupenyeza rushwa, lakini mambo yamebadilika, inavyoonekana sasa miongozo hiyo ya Mwalimu Nyerere imegeuzwa na kuonekana kama Mwalimu alihamasisha rushwa wakati wa chaguzi mbalimbali.
Zipo tuhuma nyingi za rushwa kwamba zimefanyika wakati wa chaguzi za hivi karibuni ndani ya Chama tawala, na kwa bahati mbaya zaidi chama hicho tawala kinachotuhumiwa kwa kukumbatia rushwa, mmoja wa waasisi wake ni Mwalimu Nyerere.
Sina uhakika kama wote wanaosema tumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kuyatekeleza yote aliyoyaagiza kama kweli ni kwa dhati au ni ‘danganya toto tu’, inasikitisha kuona hali ya udhaifu wa kupambana na rushwa miongoni mwa viongozi wetu inazidi kuota mizizi siku hadi siku.
Maadili ya utendaji kazi yamemomonyoka kwa kiwango kikubwa miongoni mwa watendaji waandamizi, ubinafsi ndio uliotawala sekta nyingi binafsi na za serikali, hayo yote si maagizo ya Mwalimu Nyerere, kama kweli tunamheshimu kwa dhati Mwalimu Nyerere, basi balaa zote zitakazotokea sasa ni sehemu ya laana kwa kutofuata wosia wa Baba.
Tusifanye dhihaka na kuwa wanafiki kwa kumtaja Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwa kumpa sifa nyingi za uadilifu na uongozi uliotukuka huku tukiendelea kufanya kinyume na alivyoagiza, tufikie mahali yuone aibu kwa matendo yetu.
Zipo choko choko nyingi za kutaka kubomoa miundombinu aliyoijenga Mwalimu, na hata wakati wa uhhai wake aliwahi kutabiri kuwa zipo dalili za kutaka kusambaratisha umoja uliopo, akaonya kuwa kama hali hiyo ikitokea, lazima matokeo yake yatawagusa wengi na ayhari zake ambazo zitakuwa mbaya, zitasambaa kwa kada zote.
Utaratibu wa kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ni mzuri, ambao unaotakiwa kudumishwa kwa kizazi hiki hadi kizazi cha mwisho, msingi utakaoweka kuthaminisha kitendo cha kumuenzi Nyerere hakuna isipokuwa kufuata maadili na maagizo aliyoyaacha, Tukikiuka hayo tutaambulia na kushuhudia nchi ikisambaratika. Tusifanye mzaha katika hili kwani tayari tumeshaona dalili za nyufa.
0 Comments:
إرسال تعليق
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia